Mbijima afariki dunia


MCHEZAJI Mwandamizi wa timu ya soka ya Kipanga FC inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Steven Emmanuel Mbijima amefariki dunia.

Mbijima ambaye alikuwa mlinda mlango wa kikosi cha timu hiyo, amekutwa na mauti akiwa likizoni nyumbani kwao Mbeya baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa iliyotolewa na Afisi ya Habari ya JWTZ Zanzibar iliyoko Migombani, imesema marehemu Steven (32), alianza kuugua ugonjwa wa kutoka damu puani hivi karibuni ambapo alipatiwa matibabu na kupona, lakini akiwa likizoni Mbeya akijiandaa kurudi kazini Unguja, aliugua tena ghafla na kufariki Mei 28, mwaka huu.

Imeelezwa kuwa, marehemu Mbijima alianza kuchezea timu za daraja la tatu na baadae kujiunga na timu ya Red Sea ya Chukwani iliyoko daraja la pili Wilaya ya Magharibi kabla kunyakuliwa na Kipanga iliyoko daraja la kwanza mwaka 2006 akianzia nafasi ya kipa wa akiba.

Miaka mitano baadae, mchezaji huyo alipoimarika kiwango chake, aliweza kuwa mlinda mlango wa kwanza katika kikosi cha wanaulinzi hao, nafasi aliyodumu nayo hadi anafariki dunia.

Miongoni mwa timu alizowahi kuzichezea ni pamoja na Super Stars ya Chaani Mkoa wa Kaskazni Unguja pia katika nafasi ya golikipa.

Katibu Mkuu wa Kipanga FC Swali Maalim, amesema timu yake imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mchezaji huyo, kutokana na uzoefu wake katika soka.
Marehemu alizaliwa Juni 16, 1979 katika kijiji cha Mwaluma Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambapo alipata elimu ya kidato cha sita na baadae kujiunga na jeshi Kunduchi Dar es Salaam mwaka 2003 kabla kuhamishiwa Zanzibar katika kambi ya Bavuai Migombani, na ameacha mtoto mmoja.Mwenyezi Mungu amuweke marehemu pahala pema.

MWISHO

WAANDISHI WA MICHEZO WAUNDA UMOJA WAO

UMOJA wa waandishi wa habari za michezo Zanzibar unaoajiandaa kuunda jumuiya yao, unatarjiwa kukutana kesho katika ukumbi wa Idara ya Habaari Maelezo Mnazimmoja ulioko katika jengo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Baraza la Wawakilishi la zamani.

Wanahabari hao watakutana chini ya Mwenyekiti wa muda Maulid Hamad Maulid, kujadili mambo kadhaa yaliyojitokeza katika siku za hivi karibuni.
Miongoni mwa ajenda za mkutano huo utakaofanyika saa nne asubuhi, ni kujadili kauli za baadhi ya viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) zinazowashutumu waandishi wa vyombo mbalimbali kwa kutoa taarifa dhidi ya chama hicho, pale kinapoonekana kwenda kinyume na dhamana zake.

Aidha, waandishi hao watajadili kwa kina juu ya utaratibu mzima wa kuasisi jumuiya yao pamoja na kuitafutia usajili katika Ofisi ya Mrajis Zanzibar, kwa kuanzisha Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar.

Katkka siku za hivi karibuni, kumejitokeza kauli zinazotolewa na viongozi wa ZFA kwamba waandishi wa michezo wa Zanzibar hawajui taaluma yao, na kwamba ZFA iko tayari kuwatafutia nafasi za masomo ili wapate utaalamu.

Waandishi wote wa habari za michezo pamoja na wapiga picha, wameombwa kuhudhuria mkutano unaolenga kuwa na sauti moja katika utendaji wao na kujitetea pale wanapohujumiwa.

Katika hatua nyengine klabu 20 za soka katika jimbo la Mtoni Wilaya ya Magharibi, zimekabidhiwa vifaa vya michezo na Mwakilishi na Diwani wa jimbo hilo, vyenye thamani ya shilingi milioni tano.

Katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika juzi katika uwanja wa mpira wa Basra jimboni humo, Mwakilishi wa jimbo hilo Nassor Ahmed Mazrui, alisema msaada huo unalenga kuimarisha michezo jimboni humo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya klabu zilizopewa msaada huo, kocha wa timu ya Kajima, Hassan Akisa, alisema wamefarijika kutokana na msaada huo na kuwataka viongozi hao kuendeleza jitihada zao kwa ajili ya kuinua michezo kwa timu za jimbo hilo.

Vifaa vilivyotolewa ni jezi seti moja kwa kila timu, soksi, glovu pamoja na timu hizo kupewa mipira miwili kila moja, ambapo vilipokelewa na viongozi wa klabu hizo.
Klabu zilizofaidika na msaada huo ni Mtoni Rangers, Juventus, Zanzibar Islanders, Chumbuni, FC Lion, Mwanyanya, Kajima, Mtopepo, Brunei, Beach Boys, Mkuki, Spurs, Boys Chester, Mkunguni Stars, Mtopepo Bondeni, Mazrui, Kigamboni A na B, Mbirimbini na Kidukani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s