Poleni sawa wagonjwa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, akiwaangalia wagonjwa katika Hospitali ya Makunduchi, akiwa katika ziara ya wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kulitafutia ufumbuzi wa haraka tatizo la ubakaji ambalo limeonesha kushika kasi katika Mkoa huo.

Dk Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Chuo cha Amali Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake katika Mkoa huo ambayo alizitembelea Wilaya zote mbili za Kaskazini A na Kaskazini B, pamoja na kuangalia miradi ya maendeleo iliyopo katika Wilaya hizo.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na tatizo hilo kushamiri katika Mkoa huo tayari alikwishatoa wito kufanyiwa utafiti suala hilo kwa kumtumia mtaalamu wa elimu ya mambo ya jamii (Sociology) lakini hatua bado hazijachukuliwa.

Kutokana na hatua hiyo Dk. Shein ametaka baada ya miezi mitatu awe ameshapewa taarifa juu ya tatizo hilo na kueleza kushangazwa na taarifa ya Mkoa huo aliyosemewa wakati wa kuanza ziara yake ambayo haikueleza chochote juu ya kadhia hiyo.

Dk. Shein alisema kuwa hatua iliyofikiwa juu ya tatizo hilo si nzuri hivyo kuna kila sababu ya kuwepo mashirikiano ya kutosha katika kulipiga vita suala hilo kwa pamoja na kuwataka Masheha, Madiwani na wazazi nao kushirikiana pamoja kulifanyia kazi.

Dk. Shein alimpongeza Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Mhe. Zainab Omar kwa kulisimamia kidete tatizo hilo kwa kuja na wazo la Mkono kwa Mkono katika kuhakikisha kesi zote zinazohusiana na tatizo hilo zinasimamiwa Wizarani kwake.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza umuhimu wa kupiga vita ukimwi katika Mkoa huo hasa katika Wilaya ya Kaskazini B ambapo takwimu zinaonesha maradhi hayo kushika kasi.

Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa tatizo hilo si la kulifanyia mzaha bali linahitaji kuendeleza mashirikiano na kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujikinga na janga hilo kwani kila mtu ana wajibu wa kumuelimisha mwenziwe.

Akieleza migogoro ya Ardhi, alisema kuwa Mkoa huo pia, umekabiliwa na tataizo hilo licha ya kuwa halikutajwa katika taarifa ya Mkoa aliyosomewa na kusisitiza kuwa matatizo hayo yamekuwa yakisababishwa na viongozi wa Mkoa, Wilaya, Wizara, Masheha na Madiwani na kuwataka viongozi hao wasijitose katika migogoro hiyo.

Dk. Shein aliusisitiza uongozi wa Mkoa huo kuwa kama alivyoueleza na kuutaka uongozi wa Mkoa wa Kusini wakati wa ziara yake kuwa wahakikishe matatizo ya ardhi wanayamaliza wenyewe haraka iwezekanavyo kwani wananchi wamekuwa na imani kubwa na serikali yao iliyopo madarakani.

Aidha, Dk. Shein aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini B kwa kukusanya vizuri mapato yake ambapo katika mwaka wa fedha wa 2010-2011 iliazimia kukusanya jumla ya Shilingi za Kitanzania Milioni 60 lakini hadi kufikia mwezi wa April 2011 imevuka lengo lake na tayari imeshakusanya jumla ya Shilingi za Kitanzania 91,394.

Dk. Shein pia, alieleza kutokana na kuvuja kwa mapato katika Halmashauri alisisitiza kwa kila yule ambaye anaharibu mapato katika Halmashauri atafanyiwa kazi kwani tabia hiyo haina tija na sio lengo la Mapinduzi na wala sio lengo la uongozi wa serikali uliopita na uliopo madarakani.

Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa mashirikiano kati ya Hospitali ya Kivunge na hospitali ya Makunduchi na kusifu hatua zilizofikiwa na hospitali ya Makunduchi kwa kujiandaa vizuri katika kufikiwa lengo la kuifanya hospitali hiyo kuwa ya Wilaya.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi huo wa Mkoa wa Kaskazini kwa kuendeleza vyema mradi wa Ujenzi wa skuli maalum za Sekondari katika Mkoa huo sanjari na kupongeza juhudi za maendeleo zinazochukuliwa na wananchi wa Mkoa huo zikiwemo zile za ufugaji, ushirika, kilimo na uvuvi.

Mapema Dk. Shein alifika Pwani Mchangani kuangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya wananchi waliochomewa moto mabanda yao ya biashara na kueleza kuwa kila Mtanzania ana fursa ya kuishi popote anapotaka ndani ya nchi hii kwani Katiba inaruhusu hivyo.

Dk. Shein aliwasisitiza wananchi hao kuendelea kuishi kwa uvumilivu pamoja na amani na utulivu na kueleza kuwa hao waliofanya hivyo hivi sasa wanamajuto.’Huwezi kumbagua mtu kwa jinsia, dini, kabila au mahala anapotokea”alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alieleza kuwa anaungana na wale wote waliokwenda kuwapa pole wananchi hao na kueleza kusikiktishwa kwake na tukio hilo na kusema kuwa vyombo ya sheria vinalishughulikia suala hilo huku serikali ikiendelea kutafuta njia za kuwasaidia zaidi wananchi hao ambao tayari wameshapewa eneo la makaazi ya kuishi. Dk. Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake kisiwani Pemba wiki ijayo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s