Kijana ahukumiwa kunyongwa

Jaji Mshibe Ali Bakari ni miongoni mwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Vuga Zanzibar akiwa katika hafla za uzinduzi wa filamu ya udhalilishaji wa wanawake iliyotayarishwa na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAPHELA) huko Jumba la Wananchi Forodhani Shangani

MAKAHAMA Kuu ya Vuga Zanzibar juzi imemhukumu kunyongwa hadi kufa Juma wa Juma Mohammed (45) Mkaazi wa Zanzibar baada ya kupatikana na hatia ya kumuuwa kwa makusudi mpenzi wake Monica Gervans Mtahondi.

Akisoma hukumu hiyo Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Joseph Kazi kwa niaba ya Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud alisoma hukumu hiyo ambayo kwa muda wote ilikuwa ikiendeshwa na Jaji Mahamoud kwamba mtuhumiwa amepatikana na hatia ya kuuwa kwa makusudi.

Mrajis huyo alisema kinyume na kifungu 180 na 181 sheria ya makosa ya jinai sura ya 13 mnamo febuari 10 2003 majira ya saa 4 usiku eneo la Hawai Meli 5 Mwera Juma wa Juma alimpiga kigongo na makozi Monica Gervans na kumsababishia kifo mpenzi wake huyo.

Baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na mashahidi 11 mahakama hiyo imesema imeridhika na ushahidi huyo na mtuhumiwa amepatikana na hatia na hivyo mahakama inamhukmu kunyongwa hadi kufa kutokana na kosa hilo.

Kesi hiyo iliendeshwa na waendesha mashataka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Zanzibar, Muumini Kombo na Rashid Abdallah Fadhil na kwa upande wa utetezi wa mtuhumiwa ikitetewa na Wakili wa kujitegemea Hamid Mbwezeleni.

Kesi za mauaji zimekuwa zikiogezeka katika miaka ya hivi karibuni katika Mahakama Kuu ya Zanzibar lakini ni mara chache watuhumiwa kuhukumiwa kifo kutokana na kesi nyingi kukosekana ushahidi wa kutosha kutokana na utamaduni uliozoeleka kwa jamii kukataa kutoa ushirikiano wanapoitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Wakati nchi nyingi duniani zikiwa tayari zimefuta adhabu ya kifo bado Tanzania ikiwemo Zanzibar inaendelea na adhabu hiyo katika sheria zake licha ya wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu kuipigia kelele sheria hiyo ifutwe kwa madai ni kati aya sheria kadhamizi na zenye kudhalilisha.

Akizungumza na waandishi wa habari Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado haijafuta adhabu ya kifo hadi sasa hivyo hukumu zinazotolewa ni kuwa zimo kisheria.

Alisema ingawa adhabu ya kifo haijafutwa lakini hakuna utekelezaji wa adhabu hiyo kwa kuwa ili iekelezwe lazima kupatikane saini ya rais na hivyo watu wanaotiwa hatiani na adhabu hiyo huwa wanakabiliwa na vifungo.
“Zanzibar bado haijaifuta adhabu ya kifo lakini ili adhabu hiyo itekelezwe lazima kupatikane baraka za rais wa nchi ndipo itekelezwe na kama tunavyojua ni mika kadhaa sasa huwa hukumu hizi hutolewa lakini huwa hazitekezwi kwa kuwa utekelezaji wake ni mgumu”alisema Makungu ambaye ameteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu Hamid Mahmoud kustaafu.

Jaji Makungu alisema tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 hakuna rais hata mmoja wa Zanzibar aliyewahi kutia saini adhabu ya kifo hapa Zanzibar.

Aidha alisema zipo changamoto mbali mbali za wanaharakati wa haki za binaadamu kutaka kufutwa kwa adhabu hiyo lakini juhudi hizo hazijafanikiwa hadi sasa kwa kuwa bado serikali inazingatia zaidi suala hilo kabla ya kuchukua maamuzi.

Alisema kwa mujibu wa mijadala mbali mbali iliyofanyika nchini kuhusu adhabu ya kifo bado inaonesha kwamba wananchi wanataka kuwepo kwa adhabu ya kifo kutokana na maoni yao wanayotoa katika makongamano yanayoiishwa kuhusiana na kufutwa kwa adhabu ya kifo

“Inavyoonesha wananchi wanataka adhabu ya kifo iendelee maana hata kule Bara ilikuwepo mijadala ya aina hiyo ya kutaka kufutwa kwa adhabu ya kifo na kwa upande wa Zanzibar Marehemu Professa Haroub Othman alianzisha mijadala hiyo kupitia kituo ch ahuduma za sheria” alisema Makungu.

Akizungumzia suala la kuachiwa kwa watuhumiwa wa makosa mbali mbali, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi wengi hivi sasa Jaji Mkungu alisema ukosefu wa ushahidi wa kutosha ni moja ya tatizo linalokwamisha kesi mbali mbali nchini kuendelea kusikilizwa.

Tatizo liliopo hapa Zanzibar ni wananchi kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi kwa watuhumiwa mbali mbali wanaokabiliwa na makosa na hivyo kusababisha kes nyingi kukosa ushahidi na hivyo watuhumiwa kuchiwa kwa kuwa hakuna ushahidi wa makosa wanayoyakabili.

Alisema kitendo cha wananchi kushindwa kujitokeza kutoa ushahidi kwa watuhumiwa kwa kiasi kikubwa ni chanzo cha watuhumiwa kushindwa kutiwa hatiani kwa makosa yao na hivyo kuachiwa jambo ambalo hatimae mahakama hulaumiwa kutokana na kuwaachia huru watuhumiwa.

Jaji Makungu alisema tatizo la wananchi kukataa kwenda mahakamani kutoa ushahidi linasababishwa na mambo mbali mbali ikiwemo kuoneana muhali na kuoneana haya na kuogopa lawama kutoka kwa ngudu, jamaa na majirani kutokana na jiografia ya wazanzibari waavyoishi takriban wengi wao wana udugu wa damu.

Alisema katika utekelezaji wa utawala bora mahakama haiwezi kumtia hatiani mtu bila ya kupatikana kwa ushahidi wa kutosheleza kutoka kwa wahusika mbali mbali.

Jaji Makungu alisema kufuatia tatizo hilo katika jamii serikali imeona kuna haja ya wananchi kupewa elimu kupitia vyombo vya habari ambapo itasaidia kuwajulisha wananchi majukumu yao kwa upande wa mahakama na kuondowa malalamiko kama hayo ya kuachiwa watuhumiwa.

Alisema Mahakama kuu inakusudia kutoa elimu ya uraia kuhusu mahakama na majukumu yake na wajibu kwa wananchi katika kuisaidia mahakama kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili kupunguza malalamiko ya wananchi na kurejesha imani ya chombo hicho muhimu nchini.

Leave a comment