Uhalifu upunguzwe

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Id akikata utepe kufungua rasmi kituo cha kuhudumia kesi zote za udhalilishaji wa watoto kwenye hospitali kuu ya Mnazi mmoja mjini Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza mahakama kupunguza urasimu katika usikilizaji wa kesi za ubakaji ili kusaidia juhudi za kupambana na uhalifu huo visiwani humo.

Balozi Seif alitoa agizo hilo jana mjini hapa baada ya kuzindua kituo cha “Mkono kwa Mkono” ambacho ni mtandao ulioanzishwa na serikali kushughulikia malalamiko na kesi za udhalishaji wa watoto na wanawake huko Zanzibar .

Alisema Zanzibar hivi sasa inapita kipindi cha tatizo sugu la vitendo vya aibu, vya unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto na kwamba kuanzishwa kwa kituo hicho ni mpango wa makusudi wa kupambana na tatizo hilo .

Balozi Seif alisema wakati hatua za kupambana na tatizo hilo zinachukuliwa, serikali ingependa kuona mahakama nazo na vyombo vingine vya sheria vinapunguza urasimu katika usikilizaji wa kesi za udhalilishaji wanawake, hasa za ubakaji wa watoto.

Alisema uzoefu unaonyesha kuwa uendeshaji wa kesi za ubakaji unafanyika kwa urasimu mkubwa na kusababisha waathirika wengi wa uhalifu huo kunyimwa haki baada ya kesi zao kucheleweshwa kwa kisingizio cha mahakama kusubiri uchunguzi.

Balozi Seif alisema baadhi ya kesi za uhalifu huo zinachelewa au kutokusikilizwa kabisa, licha ya kuwa na ushahidi wa kutosha, ikiwa ni pamoja na kujitokeza kwa watu wanaoshuhudia tukio na kushiriki katika hatua ya kumkamata mtuhumiwa.

“Katika baadhi ya matukio ya uhalifu huo, mbakaji anakamatwa akiwa juu ya mbakwaji na watu wanamwona,…huo unatosha kuwa ushahidi kamili, naomba mahakimu watusaidie kukomesha tatizo hili ,” alisema Balozi Seif.

Alisema ushughulikiaji wa kesi za ubakaji watoto na unyanyasaji wa wanawake kwa jumla, unaendeshwa kwa taratibu zilizojaa urasimu na hivyo kutoa nafasi kwa wahalifu kutamba.

“Hatuwezi kutoa nafasi kwa wabakaji kuzidi kuwadhalilisha watoto na kuachwa kutamba mitaani, naomba mahakama,.. mtu akikamatwa “live” – macho makavu, haki itendeke badala ya kusubiri uchunguzi kwa muda mrefu,” alisema.

Mapema Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Watoto na Wanawake, Zainab Omar Mzee alisema kituo hicho kimeanzishwa kwa ufadhili wa taasisi ya “Save the Children” ya Uingereza na UNICEF na kitafanykazi saa 24 katika Hospitali ya Kuu ya Mnazimoja.

Kituo hicho kitapokea moja kwa moja kesi za ubakaji wa watoto. Wafanyakazi wa kituo hicho ni wauguzi, polisi, madaktari, washauri nasaha, wanasheria na wanaendesha mashtaka kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, nia ikiwa ni kurahisisha upatikanaji wa ushahidi wa kesi hizo.

Juu ya matukio ya ubakaji na udhalilishaji wa watoto na wanawake, Waziri Zainab alisema jumla ya kesi 3,116 za uhalifu huo zimeripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi na idara ya ustawi wa jamii visiwani Unguja na Pemba kati ya mwaka 2006 hadi mwaka jana.

Hata hivyo, alisema hatua hiyo haijasaidia kupunguza tatizo kwa sababu ushughulikizaji wa kesi hizo haufanyiki kwa ufanisi unaotarajiwa.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s