Fungate ya SUK imekwisha kazi ianze

FUNGATE YA SUK IMEKWISHA, SASA KAZI IANZE

Wiki iliyopita Rais wa Zanzibar Dk Ali Muhammed Shein alifanya ziara
rasmi katika eneo muhimu la kiutawala yaani Mkoa wa Mjini na Magharibi
kutizama harakati mbali mbali. Ni ziara iliyokuwa ikitarajiwa ingawa
sisemi kuwa imechelewa.

Sijui kuwa muda wa ziara ile ulitosha au iwapo alitembelea maeneo
ambayo yalikuwa yana muhitaji sana au tu ilikuwa ni kupanga ziara
ambayo watendaji wake wameamua kumpeleka katika maeneo ambayo yana
maslahi yao zaidi.

Sisemi maslahi kibinafsi lakini ambayo si ya matatizo sana ili kutompa
Rais picha ya kukata tamaa au kumuoneysh maeneo ambayo hata hivyo yana
mafanikio zaidi kuliko matatizo.

Maana kama ingekuwa inaruhusiwa kutoa ushauri basi nina hakika watu
wengi wangemshauri Rais atembelee maeneo mengine kabisa kuliko hayo
aliyokwenda maana kwengineko ndiko macho yake na kauli yake
vingehitajika zaidi kuokoa hali mbaya ilivyo. Lakini hayo ndio
yamekwisha, tugange yajayo, pengine siku za mbele wananchi
watashauriwa.

Mwisho wa zaira yake Rais Shein alikuwa na mkutano ulioitwa wa
majumuisho ambao alikusanya watendaji wote na kutoa kile alichokieleza
kuwa ni tathmini ya ziara yake katika eneo hilo. Bila ya shaka alitoa
tathmini juu ya alichokiona na kuambiwa na kutakiwa kukwamua hapa na
pale.

Kwangu nilivutiwa na mambo mawili katika maelezo yake. Kwanza kuwataka
watendaji wasifiche habari na wawe wazi kwa umma kwa kupitia vyombo
vya habari jambo ambalo limekuwa sugu hata ndani ya Serikali na kuja
kwake madarakani hakujabadilisha hali hadi hivi sasa.

Akizungumza katika semina elekezi ya watendaji wa Serikali wiki moja
tu kabla ya hapo, pia Dk Shein alizungumzia suala hilo na kusema
watendajiw aache uhafidhina.

Pili alizungumzia suala la utendaji mbovu, utoro na utegeaji katika
ajira ya Serikali jambo ambalo pia atakuwa amelirithi na ambalo
halijabadilika hata kidogo tokea yeye na Serikali yake kushika
madaraka chini ya mfumo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye
muundo wa Umoja wa Kitaifa, jina lenyewe likiwa refu na lenye
kubabaisha bila ya sababu za msingi sana.

Tuanze kwanza kwenye suala la mawasiliano ambalo ni la msingi kwa
sababu bila ya mawasiliano hakuna Serikali. Serikali imechaguliwa na
watu watu wanataka kujua Serikali yao inafanya nini kwa niaba yao bila
ya hivyo Serikali inakuwa haitimizi wajibu wake.

Wala si sifa na utendaji bora Serikali kujifungia na kufanya
inayofanya. Hata yakiwa mazuri kiasi gani kama hayajulikani wala
hayaelezwi haitasadia kitu. Kueleza yaliofanywa haina maana ya
kujisifu bali ni kudhihirisha kutimiza kwa wajibu.

Lakini pia kuwepo mawasiliano hasa kutoka kwa wananchi kwenda kwa
Serikali kunasaidia kuipa Serikali hiyo kioo chake cha kujiona na
kujipima kwa sababu ni wananchi ndio wataojua makosa ya Serikali na si
Serikali yenyewe.

Kwa hivyo kama Dk Shein alizungumzia suala la mawasiliano natarajia
amekusudia njia mbili. Moja kutoka Serikali kwenda kwa wananchi,
ambayo kwa sasa ni mbovu lakini pili ni kutoka kwa wananchi kwenda kwa
Serikali ambayo kwa sasa haipo kabisa.

Angalau tunajua kuwa japo hivyo hivyo tunaweza kupata habasri za
taasisi za umma kutoka kwa wasemaji wake has Mawaziri na Makatibu
wakuu, ambao kwa hakika ni wazito katika kazi hiyo isipokuwa penye
maslahi yao, lakini mimi sijui njia yoyote ile mwananchi anaweza
kulalamikia Serikali au afsia wake.

Ni mawazo mengi kuhusu hili lakini kwa leo itoshe tu kumwambia Dk.
Shein kuwa hapatakuwa na mabadiliko katika suala la utoaji habari wa
watendaji wake na hata wansiasa wake kama hapatafanyika mabadilko
makubwa ya kimuundo na hata ya kisera.

Juu ya suala la pili la utoro, utegeji na uzembe makazini, Dk Shein
alifanya kila watu wa habari hupenda kusema kukunjua makucha yake kwa
kuwa mkali katika hili na bila ya kutafuna maneno.

Alisema Serikali haitaki utegeaji, utoro na uzembe kazini kwa sababu
hilo ni kinyume na mtakwa ya ajira na pia ni kinyume na utendaji wa
Serikali ambao unategemea mafanikio kwa kutokana na utendaji wa
wafanyakazi wake.

Naam, mpaka hapo Dk Shein yuko sawa kabisa, lakini nikaanza
kutofautiana nae wakati aliposema kuwa eti ambae hataki kazi asogee
kwenda kumnon’goneza ili sijui pengine amuondoe kwa stara na heshima.

Najua kwa lugha hii Dk Shein alijaribu kuwa mtaratibu na
kutodhihirisha mamlaka aliyonayo, lakini ni ukweli pia hakuna ambaye
atakwenda kumwambia kuwa amechoka kazi. Kwanza kwa kuwa hatamfika
lakini pili ni kwa kuwa Wazanzibari hawana utamaduni huo wa kusalimu
amri kwa kitu asichokiweza na badala yake atakishika na kukishikilia
mpaka ajue mwisho.

Badala yake Dk Shein anazo njia nyingi za kujua wafanyakazi wazembe,
wakorofi, watoro na wategeaji, taarifa ambazo anaweza kuzitumia
kufukuza au kupunguza wafanyakazi ambao hata hivyo tayari ni mzigo
mkubwa kwa Serikali. Umma katika hili hautamlaumu wala nafasi ya
kisiasa ya chama chake haitaharibika.

Mifano ya utendaji dhaifu iko mingi na naamini hata ndani ya ofisi
yake. Kwa mfano najua kuwa watu 700 na ushei waliokuwa wamevunjiwa
nyumba zao eneo la Mtoni mwaka 1996, ingawa hili ni shauri la muda
mrefu, lakini waliiandikia ofisi yake kuulizia juu ya fidia yao
mwanzoni mwa mwaka huu, na hadi naandika makala hii hata nobe jawabu
tu ya kuwa barua yao imepokelewa hawajaipata.

Au kwenye maamuzi ya kimahakama ndiko kugumu zaidi kwa watendaji wake
na nitatoa mifano miwili. Mmoja ni ule wa maamuzi ya Mahakama kuwa
wafanyakazi wa Benki ya Watu wa Zanzibar warudishwe kazini kwa sababu
ufukuzwaji au upunguzwaji wao ulikiuka taratibu na hivi sasa
wakiandika notisi ya kuishitaki Serikali, kwa kutotimiza amri hiyo, na
hapana shaka huenda Serikali ikaingia katika mgogoro mkubwa wa
kisheria.

Au taarifa niliyonayo kuwa wiki iliyopita Mahakama imetoa amri kuwa
Makontena ya Darajani yafunguliwe wakati shauri likiendelea
Mahakamani, lakini watendaji wa Manispaa wamekuwa wakikwepa kutekeleza
amri hiyo kwa kujiberuza huku na kule jambo ambalo naamini si tu
linakiuka utawala bura, lakini linaweza kuitia Serikali pia kwenye
mgogoro wa kisheria.

Najua Dk Shein kuna kitengo cha kufuatilia ahadi za Rais  lakini pia
kitengo hicho kifuatilia matamko ya Rais ambayo zama za utawla wa
mwanzo wa Abeid Karume yalikuwa ni sheria, lakini kwa sasa ni mwongozo
kwa watendaji na ni bakora kwa wananchi kuwarudishia viongozi wao
iwapo watashindwa kutekeleaelekezo ya Rais.

Miezi sita inatosha kutoa mwelekeo wa wapi Serikali inaelekea, na kwa
hivyo wananchi wanayo haki sasa kuhoji kwa nguvu zaidi utendaji wa
Serikali, ambayo wamekuwa na matumaini nayo makubwa na kwa kweli hadi
sasa matumaini hayo hayajapata sura waliokuwa wakitarajia.

Sasa fungate ya Serikali imemalizike na kazi ianze.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s