Serikali ya umoja iwe wazi

Mwandishi Mwandamizi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Ally Saleh (Alberto)

Na Ally Saleh

Wiki iliyopita Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Muhammed Shein aliongoza
kikao cha watendaji na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kile kilichoelezwa kuwa ni semina elekezi ya Serikali hiyo.

Semina elekezi hiyo inakuja miezi sita tokea Serikali kushika
madaraka, na kwa hilo mimi sioni ubaya wake maana kila mara mwanadamu
anahitaji maelekezo. Kama maelekezo hayakuweza kutolewa mwanzo, basi
watendaji na viongozi walitumia uwezo na uzoefu wao na ndio maana
tukawa tuko hapa hadi sasa.

Lakini uwezo na uzoefu wao haina maana ndio matakwa au matarajio ya
taifa kwa sababu matarajio ya taifa hupangwa, huratibiwa na hutekelezwa
kwa pamoja na katu mtu mmoja mmoja hawezi kuyatimiza.

Kwa bahati katika kipindi hiki matarjio na matakwa ya taifa ni makubwa
zaidi kwa sababu ya kuja kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo
hadi hivi sasa kwa mtizamo wa wengi imeshindwa kufikia kiwango ambacho
watu walikitarjia.

Inawezekana matamshi haya yakaleta ubishi na hata kunyooshewa kidole,
lakini katika hili naweza kusimama kujibu hoja, maana tayari hata
viongozi wenyewe wakiwemo Makamo 1 na Makamo wa Pili wamelikiri hilo.

Na wasingewezaje kulikiri wakati tokea SUK kuingia madarkaani petroli
imepanda mara tatu na huku takriban bidhaa za vyakula zote zikipanda
na maisha kuwa magumu zaidi kuliko maelezo na wananchi wakihisi
wameangushwa kama si kubwagwa.

Ndani ya nchi kuna sheria inayosema kuwa ni kosa la jinai kutoa
maelezo ambayo yataelekea wananchi kuichukia Serikali yao na kwa hivyo
bora nisite hapo tu nikisema kua SUK inahitaji mapitio ya nguvu ya
kipindi chake cha miezi sita., maana kama kungekuwa na kura ya maoni
(opinion poll) basi ingepata alama dhaifu sana.

Inawezekana, kama ambavyo huwa tunaambiwa kuwa kuna mipango hii na
hii, inawezekana kama ambavyo tunaambiwa tuwe na subira mambo mazuri
hayataki haraka, inawezekana kama tunavyoambiwa kuwa safari za
viongozi huku na kule zina manufaa yake, lakini kwa ujumla ukimya na
ukosefu wa uwazi umekuwa mkubwa ndani ya SUK.

Dalili kwamba SUK haitakuwa na uwazi na mawasiliano niliiona mimi
mwanzo kabisa siku ambayo Dk Shein aliapisha mawaziri wake na nilifika
Ikulu mapema na wallahi nilirudishwa nikaambiwa kuwa sherehe ya
kuapishwa mawaziri itakuwa ni ya faragha.

Sikuwa na la kufanya zaidi ya kuthibitisha kwa mtendaji mmoja wa
Kitengo cha Mawasiliano na akaniambia ni kweli waandishi hawahitajiki,
lakini sa mbili baadae nikawaona waandishi wenzangu kadhaa wa kadhaa
katika viwanja vya Ikulu wakishuhudia na kuripoti viapo hivyo.

Nilichojifunza kwa wakati ule ule ni kuwa hizo zilikuwa ni dalili kuwa
hapatakuwa na uwazi lakini pia hakuna mawasiliano ndani ya Ikulu.
Maana kama mmoja anasema hivi na mwengine anasema kinyume chake ina
maana mbili tu.

Moja ni kuwa mmoja hapendi vyombo vya habari na kwa hivyo ni rahisi
kusema hawahitajiki lakini pili mwengine kila kitu cha Serikzli kwake
ni siri na kwa hivyo hapendi mambo yawe wazi. Wote wawili kwa lugha
nyepesi na ya kisiasa katika rubaa za siasa ni wahafidhina.

Na katika suala la uwazi na mawasiliano SUK inalalia zaidi katika
uhafidhina hata kuliko vyenginevyo. Na uhafidhina huu kwa fikra zangu
una sababu kadhaa za msingi na nyingi zake ni kutokana na muundo
wenyewe wa Serikali. Kama jina lake lilivyo basi Serikali imeundwa
katika kunusuru hali ya kisiasa ya Zanzibar na kwa hivyo dhana hii
imezama ndani ya vichwa vya watendaji na viongozi na kutupa hasara
nyingi.

Kwanza kukosekana kwa Sera ya Pamoja na badala yake kuendesha
Serikali kwa kutumia Sera ya CCM kama maelekezo ya kikatiba
yalivyotaka kumepunguza uwazi na mawasiliano kwa Serikali. Sijapata
kumsikia Maalim Seif akisema kuwa SUK inatekeleza Ilani ya CCM wakati
kauli hiyo hutolwa Nalozi Seif Idd kila anapopata fursa na mnasaba wa
majigambo kama hayo.

Pili, kila chama kimeingia Serikali na usuli wake CUF ikijulikana kwa
kupenda vyombo vya habari kwa sababu vilikuwa ni nyenzo muhimu wakati
SMZ ilipokuwa kandamizi na CCM imekulia kwa kutokuwa karibu na vyombo
vya habari zaidi kwa sababu haikuvihitajia sana kwa vile nguvu za dola
zilikuwa zikiwatosha.

Na ndio maana tukaona ingawa kumekuwa na ukuaji wa habari na
mabadiliko ya kisheria, lakini kasi imekuwa ndogo maana raghba ya
kufanya mabadiliko hayo haikuwa kubwa kulinganisha na mahitaji. Leo
Zanzibar si ya kuwa hapa tulipo kulingana na kiwango tulichokuwa nacho
kabla Uhuru na Mapinduzi.

Tatu, viongozi wa kisiasa wengi hasa waliotoka upande wa CUF ni wageni
katika ngazi za uongozi walizonazo hivi sasa na kwa hivyo wamependa
kuchukua hadhari lakini kwa bahati mbaya zaidi ni kuwa mfumo wenyewe
wa Serikali walioukuta ni usio wazi na usio na mawasiliano makubwa.

Mawasiliano makubwa yanayofanywa na Wizara za Serikali ni ziara za
viongozi. Naami katika hilo kwa hakika linafanywa mana kila kiongozi
anataka aonekane anafanya kazi hasa na watu wajimboni mwake. Lakini
jee taarifa za Serikali ni ziara tu? Jee wanachi watosheke na utendaji
wa Serikali yao kwa kuambiwa au kuarifiwa juu ya ziara zao na kufungua
semina au kuoanana na wageni wa nje au wafadhili?

Sina hakika, nini kimetokea katika semina elekezi lakini ningetaka
kuamini kuwa kimojawapo ambapo kimejadiliwa ni suala la uwazi na
mawasiliano ndani ya serikali kuelekea kwa umma. Kama hakikupewa
umhimu wake basi ni hasara na tusitegemee mabaiko makubwa katika eneo
hili.

Lakini hebu tuchukulie mfano wa Ikulu ambayo ina kitengo cha
mawasiliano lakini pia kwa kulinganisha ina rasilmali bora zaidi. Jee
Ikulu yetu iko wazi na ina wasiliana kiasi cha kutosha? Kwanini kama
ni hivyo Serikali haina Msemaji Rasmi au Msemaji wa Serikali ? Leo
ukitaka habari za Ikulu hujui umpigie simu nani, maana waandishi
wenzio unaowajua hawana uwezo wa kutoa kauli na aliye na uwezo Katibu
Mkuu Kiongozi huwezi kumfika.

Nina hakika habari haziwezi kushuka sawa sawa kwa waandihsi na hatimae
kwa umma katika hali kama hiyo ambapo pia katika mawizara kuna maafisa
wa habari ambao kuwepo kwao ni mapambo tu, maana hawahudhurii vikao
vya Wizara na kwa hivyo hawawezi kuwa ni weledi wa masuala ya Wizara
na ndio maana kuwepo kwao hakuna taathjira zaidi ya kuwaalika
waandishi kuhudhuria mikutano ya waandishi wa habari na kutoa taarifa
kwa vyombo vya habari mwaka kwa vuli.

Mtiririko wa mabadiliko kuelekea uwazi na kuasiliana ulipaswa pia
ushuke katika vyombo vya umma kama Televisheni Zanzibar, Radio
Zanzibar na Idara ya Habari maelezo kwa vyombo hivyo kuja na mbinu
mpya, za kisasa na zenye mvuto kwa wananchi juu ya Serikali yao.

Na hata wakiwa na mbinu hizo ni wazi kuwa wanghitaji fedha, utalamu na
rasilmali zaidi na sio hali ilivyo sasa ambapo Televisheni Zanzibar
ikiwa na uhaba mkubwa wa vitendea kazi, Idara ya Habari Maelezo haina
hata nguvu za mawasiliano na Radio Zanzibar ikihema kwa uhaba wa pumzi
na kwa hivyo haisikiki kwa nguvu zinazohitajika, lakini wakati huo huo
Serikali ikinunua magari ya fakhari kwa lukuki ya watendaji wake na
posho za vikao zikiwa pale pale.

Hapana shaka ni suala la vipaumbele? Jee uwazi na mawasiano ni vipa
umbele kwa Serikali? Kwa maneno mengine jee Serikali inataka kuwa wazi
kwa wapiga kura na jee inataka kuwasiliana nao na wao kuwasiliana na
Serikali yao? Maana uwazi na mawasiliano una pande mbili, moja
ikdhulumiwa basi huibuka hasira.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s