Jahazi kuwasilisha rasimu ya katiba

Jamila Abeid ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Jahazi Asilia anasema katika rasimu ya katiba mpya ya Zanzibar wamependekeza Umoja wa Mataifa waitambue Zanzibar kama nchi kamili

Jahazi kuwasilisha rasimu ya katiba

KAMPENI ya baadhi ya wazanzibari kutaka Zanzibar iwe na mamlaka zaidi ndani ya Muungano, ziliendelea baada ya Chama Cha Jahazi-Asilia kuwasilisha rasimu ya katiba mpya ikipendekeza rais achaguliwe na bunge la Zanzibar badala ya mfumo wa sasa na kutaka Zanzibar itambuliwe na Umoja wa Mataifa.

Rasimu hiyo inayojulikana kwa jina la “Katiba ya Zanzibar Huru,” ilizinduliwa na katibu mkuu wa chama hicho Jamila Abeid katika mkutano na waandishi wa habari hapo jana uliofanyika katika ukumbi wa jumuia ya walemavu Zanzibar, mtaa wa Kikwajuni- Welesi.

Rasimu mpya ya katiba ya Zanzibar iliyotayarishwa na chama hicho chenye makao yake makuu mjini Zanzibar , inapendekeza kufuta utaratibu wa rais wa Zanzibar kuchaguliwa na Wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari kiongozi huyo alisema katiba ya 1984 inapaswa kuangaliwa upya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 kwa kuwa kuna kasoro nyingi katika katiba hiyo ambazo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa.

Katibu Mkuu wa Chama hicho Jamila Abeid amesema kwamba nafasi ya rais wa Zanzibar achaguliwe kwa kura za siri na baraza la Taifa badala ya kupigiwa kura na wananchi kama utaratibu unaofanyika hivi sasa.

Alisema kwamba watu wanaotaka nafasi hiyo waombe kwa kuzingatia sifa na masharti na baraza hilo la Taifa lichague nani awe rais badala ya kuendelea na mfumo wa sasa ambao hauna faida.

Aidha amesema kwamba wanapendekeza Zanzibar iwe na waziri mkuu kama mtendaji mkuu wa serikali badala ya kuwa na makamo wa kwanza wa rais na makamo wa pili lakini waziri mkuu huyo achaguliwe na baraza la Taifa akitoka nje ya wajumbe wa baraza hilo kwa utaratibu wa kupigiwa kura ya siri na kuthibitishwa na rais.

Mapendekezo hayo ya rasimu ya katiba yameweka utaratibu mpya wa kumpata mwanasheria mkuu, jaji mkuu mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wote wachaguliwe na baraza la Taifa (National Assembly) na wapatikane kwa kupigiwa kura za siri na chombo hicho badala ya kuteuliwa na rais.

Katibu mkuu huyo alisema sheria ya kuwapata wajumbe wa baraza la wawakilishi iangaliwe upya na inapendekeza wapatikane kwa kupitia mikoa badala ya majimbo kwa kulingana na kura.

Marekebisho hayo ya rasimu ya katiba yanatetea Zanzibar kuwa dola huru ili iweze kuwa na nafasi ya kuwa mwanachama wa umoja wa Mataifa na kuwa na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kama ilivyokuwa kabla ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1963 nchi hizo zilipoungana.

Akisoma rasiku hiyo katibu mkuu huyo alisema kwamba sheria ibadilishwe ili Mtanzania aweze kuwa na uraiya wa zaidi ya nchi moja ndani ya Muungano wa serikali tatu badala ya kuwa sheria iliyopo sasa ambayo inawanyimwa wananchi kuwa na uraia kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja.

Aidha alisema kwamba waziri wa mambo ya ndani apewe uwezo wa kutangaza hali ya hatari kwa kushauriana na rais wa Zanzibar, Waziri mkuu na mkuu wa jeshi la Polisi badala ya nafasi hiyo kubakia kwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania pekee.

Mapendekezo mengine yanazungumzia mtu atakaewekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani isizidi miezi mitatu na baada ya hapo ni lazima afikishwe katika vyombo vya sheria na iwapo atapatikana na hatia muda aliwokaa kizuizini kabla ya kuhukumiwa utafidiwa katika adhabu hiyo.

Akizungumzia sheria ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar alisema wamependekeza kuundwe kamisheni ya uchaguzi na wajumbe wake wachaguliwe na baraza la Taifa na kuthibitishwa na waziri mkuu wa Zanzibar kabla ya kupata baraka za rais badala utaratibu wa sasa ambao rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteuwa.

Jamila ambaye aliwahi kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia chama hicho aliwaambia waandishi wa habari kwamba wajumbe wa tume ya uchaguzi chama chake kimependekeza wachaguliwe kutoka serikalini na kambi ya upinzani na kama kutatokea kutokufahamiana katika masuala ya uchaguzi maamuzi ya mahkama kuu yawe ya mwisho badala ya tume ya uchaguzi ya Zanzibar pekee.

Aidha rasimu hiyo ya katiba mpya ya chama hicho inapendekeza nafasi za viti maalum za wanawake na za kuteuliwa na rais kufutwa kabisa na badala yake watu wote warudi katika kugombea na kuchaguliwa na wananchi ili kujenga msingi wa kweli wa demokrasia hapa nchini.

Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa chama hicho, Amour Rajab Amour alisema kwamba jahazi asilia inampongeza rais wa Zanzibar kwa hatua mbali mbali anazozichukua kwa kujenga umoja na kufanikisha serikali ya umoja wa kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza mivutano ya kisiasa iliyokuwepo huko nyuma.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba baada ya rasimu hiyo ya katiba mpya ya Zanzibar kukamilika wataiwasilisha serikalini lakini watakusanya maoni ya wananchi mbali mbali wa Unguja na Pemba ili kupata maoni yao kabla ya kuiwasilisha katika taasisi zinazohusika.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s