Shein unazijua hoja za Mambo Msiige?

Dk Shein unazijua vyema hoja za Mambo Msiige?

Na Ally Saleh

Wiki iliyopita Rais wa Zanzibar alirudi kutoka ziara ambayo tumesikia
kuwa ilikuwa ya mafanikio wakati alipoweza kufanikiwa kupata furushi
la mambo kadhaa wa kadhaa kutoka nchini Uturuki.

Uturuki ni moja ya nchi za Ulya zinazpopiga hatua kubwa sana na hivi
sasa ikiwania kuingia katika Umoja wa Ulaya inafanya kila bidii
kuzifikia nchi changa, kama juhudi inayofanywa na Brazil, Inida na
China.

Katika Uwanja wa Ndege wa zanzibar Dk Ali Muhammed Shein, Rais wa
Zanzibar alizungumza na waandishi wa habari na moja ya suala
aliloulizwa lilikuwa ni kuhusu Jengo la kihistoria la mambo Msiige
lilioko katika eneo la Shangani na ambalo limekodishwa kwa ajili ya
kujengwa hoteli y nyota tano ya Kempinsky.

Wakati akiondoka kwenda Uturuki kulikuwa na malalamiko mawili dhidi y
ujenzi huo. Moja wapo ni wa chama cha siasa wakidai juu ya usiri na
uharamu wa ukodishwaji wa jengo hilo ikiwemo kukiukwa taratibu na
kinara wake alikuwa Juma Ali Khatib wa chama cha TADEA.

Kwa upande mwengine yalikuwa ni madai ya wananchi 300 wakiongozwa na
Abubakar Shani ambao walisaini madai yao baada ya kukaribishwa kutoa
maoni na Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa mujibu wa sheria za ujenzi.

Akijibu suala hilo katika mkutano huo Dk Shein ameelezewa kusema haoni
sababu ya kwa nini watu wanahoji ukodishwaji wa jengo hilo kwa sababu
ni mali ya Serikali na Serikali yenyewe ndio inayokodisha na kwa hivyo
kwa nini ihojiwe kukodisha kitu chako wenyewe.

Kwa hakika kwanza nilipigwa na butwaa niliposikia kuwa Dk. Shein
amesema hivyo lakini pili nikashangazwa sana kusikia amesema hivyo.
Kwa sababu nyingi sana sikutarajia kuwa angesema hivyo, lakini pili
sikutarajia kabisa pia angedharau kabisa umma ambao ndio ulio mtia
madarakani na ambao ndio wenye Serikali.

Haikumpasa kabisa, nionavyo mimi, Dk. Shein kusema kuwa kuuza kitu cha
Serikali ni maamuzi yanayoweza kufanywa na Serikali bila ya kufuata
taratibu ambazo Serikali yenyewe imejiwekea, na kama imefuata jawabu
yake ingekuwa kuelezea hizo taratibu na namna zilivyofuatwa, ndio
utawala bora.

Niliwahi kumsikia mtetezi mmoja wa Serikali akisema tenda ingehitajika
kutangazwa iwapo jengo linauzwa lakini kwa kuwa limekodishwa hapakuwa
na haja ya kufanya hivyo. Huu ni upotoshaji mubwa na kujaribu
kudanganya umma.

Kama kuuza au kukodisha tayari kuna sheria inayoelezea taratibu zake
na yote ni kwa ajili ya kuondosha dhana na tuhuma kwa nini ikapewa
kampuni hii na si nyengine katika kuweka uwazi kama ambavyo hivi sasa
hoja zinazuka kuwa mpaka Oktoba 2010 Serikali ilkuwa na muelekeo wa
kutoa eneo hilo kwa Kampuni ya Serena lakini dakika za mwisho ikapewa
Kempinsky.

Moja ya jambo ambalo Kampuni ya Serena ilitoa ahadi ya kulifanya ni
kuwajengea jengo jipya Ofisi ya mambo Msiige ktika eneo ambalo
litachagua Serikali, lakini kwa kupewa Kempinsky tunaona Ofisi hiyo
ilivyokwenda kujibana katika jengo la zamani la Benki ya Watu wa
Zanzibar.

Pia Dk. Shein tunajua anajaribu kulinda maamuzi yaliofanywa na
Serikali iliyopita ambapo tunajua kuwa ukodishwaji huo ulifanywa siku
chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 na kwa hivyo maamuzi
yaliharakishwa na kwa hivyo ndio umma unahoji uhalali wake.

Mbali ya TADEA na Juma Ali Khatib, kwa upande wa kundi lilojitokeza
jengine la Abubakar Shani hilo madai yake na hoja zao ni tofauti
kabisa na hili pia Dk. Shein naamini analo taarifa nalo kwa sababu
ofisi yake ilipelekewa nakala ya madai yao, lakini nalo pia amelipiga
kumbo.

Kundi hili lilichukua fursa ya mwanya wa kisheria wa kutoa maoni
kuhusu ujenzi huo ambapo Mamlaka ya Mji Mkongwe ilitoa wiki tatu kwa
ajili ya umma kutoa maoni kuhusu ujenzi huo.

Kundi hilo limelalamika kuwa Mamlaka ya Mji Mkongwe amepiga ngea kwa
kufanya ujanja kwenye tangazo hilo kwa kulibandika kwenye eneo la
ujenzi April 19 wakati tangazo likiwa na tarehe 8 April, kwa maana
nyengine kupunguza muda wa kuonekana na umma.

Kama hiyo haitoshi muda wa siku 21 za kutoa maoni ililiwa na tarehe
kadhaa za mapumziko kama vile Ijumaa Kuu, Jumatatu ya Pasaka, Sherehe
za Muungano na pia swiku za Jumamosi na Jumapili ambazo si siku rasmi
za kazi. Umma ulitakwa kuongezwa muda ambalo jambo halijafanywa hadi
leo.

Lakini pili Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe imewataka wananchi
watoe maoni juu ya ujenzi huo bila ya wananchi kuwa na fursa ya kuona
ramani au mchoro wowote ule na kwa hivyo kuyafanya maoni yao yasiwe na
maana yoyote ile. Barua ya kundi hilo ililalamikia hilo.

Kwa hivyo hapakuwa na mchoro au ramani kuhusu vipi jengo la Mambo
Msiige litakuwa hoteli na wakati huo huo kuhifadhiwa, hapakuwa na
mchoro vipi eneo lilokuwa na Starehe Club litavyopata sura mpya na
hapakuwa na mchoro ni vipi eneo wazi la Shangani litageuzwa kuwa
bustani ya umma.

Kubwa pia ni kwamba umma haujaonyeshwa mchoro ni vipi matumizi ya
ufukwe yatakuwa na haki za wananchi kuweza kufikia ufukwe huo ambao
pia kuna suala la haki ya wavuvi ikijulikana eneo hilo limekuwa
likitumika kwa kazi hiyo kwa miaka na dahari.

Wananchi hawajui chochote juu ya utafiti wa kulinda mazingira
(Enviromental Impact Assesment) wala utafiti wa hali ya kijamii
(Social Impact Assessment)  ambapo lazima kuwa na hoteli ya kiwngo
kinachoelezwa kati kati ya mji kutaleta mabadiliko makubwa ya kijamii
na kimazingira.

Si haki na si halali na wala si utendaji wa utawala bora kuyafanya
hayo yote dhidi ya umma kwa kuwa tu Serikali inataka au imeshaamua
kuwa ujenzi huo ufanyike katika eneo hilo. Zaama za kusema maamuzi ya
Serikali lazima yawe zimepitwa na wakati, ila Dk Shein atakuwa anajua
kuwa hapana wana harakati wa Zanzibar watakaokwenda Mahakamani kwa
ajili ya unyonge wao lakini si kwa kuwa ni waoga.

Ila ni wazi kuwa taratibu zinazopaswa kwa ukodishwaji hazikufanywa na
wala umma haukutendewa haki katika suala la utoaji wa maoni. Hilo
Serikali inapaswa ilijue hata kama itakataa kulikiri.

Pia sijui iwapo Dk Shein anajua kwamba wakati Mamlaka ya Mji Mkongwe
ikisubiri kutolewa kwa maoni na umma, basi wakati huo ikatoa vibali
vya ujenzi kwa Kempinsky jambo ambalo limeonyesha dhahiri kuwa maoni
ya wananchi yasingekuwa chochote kile kuathiri kubadilishwa hata
dirisha seuze muelekeo wa jengo.

Matokeo ya haya ni nini? Maotkeo ni kuwa hoteli itajengwa wananchi
mwisho wa ujenzi hawatajua iwapo ramani na michoro imefuatwa au la ila
Serikali itajua. Mwisho pia wananchi hawatajua iwapo eneo lilotumika
kujenga bustani ndilo kwenye michoro au la, lakini Serikali itajua.
Sasa kama ni hivyo kulikuwa na maana gani kutaka maoni ya wananchi?

Kitu kimoja muhimu katika barua ya kundi la Abubakar Shani ni kutaka
kukutanishwa na Kampuni ya Kempinsky kuzungumza nao juu ya uhifadhi wa
Mji Mkongwe na pia suala la ajira kwanza kwa vijana wa Mji Mkongwe
lakini pili kwa Wazanzibari na kutoa rai ya kuanzisha mfuko wa
kusomesha vijana kuanzia sasa.

Mfuko huo rai ni kuchangiwa na Kampuni ya Kempinsky, Serikali na
wakaazi wa Mji Mkongwe. Lakini hilo pia limesukumwa kando na kesho na
kesho kutwa tutasikia watu wakilalamika kuwa kazi zinachukuliwa na
wageni, na nitapomsikia kiongozi akisema hivyo nitamshindilia tambara
la mdomo.

Ninavyoamini kuwa Dk. Shein ameteleza katika hili na sbabu kubwa ni
kutopata taarifa za kutosha. Ajue haki mbili hazikutendeka. Ya kwanza
ni ya taratibu za kutoa mali ya Seriali na pili taratibu za maoni ya
wananchi.

Inawezekana leo akapuuza hoja zote hizo mbili, lakini umma kama umma
utakuja kupata nafasi ya kumkumbusha, kama sio leo kesho na kama si
kesho mtondogoo. Umma una kawaida ya kuto sahau hasa unapodogoshwa au kutengwa katika haki zake.

Advertisements

One response to “Shein unazijua hoja za Mambo Msiige?

  1. Hii yooote inachangiwa na kwamba Zanzibar haina Sheria yoyote inayohusiana na Suala la manunuzi na uuzaji(Public procurement ) kwahyo macorrupter ndo njia wanayotumia kula mali za wananchi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s