Tahariri ya Mwananchi

Msimamo wa Gazeti la Mwananchi linalochapishwa hapa Tanzania ambalo hutoka kila siku na kusomwa na maelfu wa wananchi ndani na nje ya nchi kwa njia mbali mbali ikiwemo mawasilian ya internet

SMZ iwasake wahuni waliochoma vibanda, iwaadhibu

TUMESIKITISHWA na habari kuwa mabanda 73 ya wafanyabiashara, wengi wao kutoka Tanzania Bara, yaliteketezwa kwa moto mwishoni mwa wiki katika fukwe za Pwani Mchangani na Kiwengwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kati ya vibanda hivyo, 43 vilichomwa katika ufukwe wa Pwani Mchangani karibu na Hoteli ya Waikiki, na mabanda 30 yaliteketezwa Kiwengwa, karibu na Hoteli ya Ocean Beach Resort.   
Ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya wananchi wakiendelea kujichukulia sheria mkononi kwa visingizio mbalimbali. Katika tukio hilo la kutisha,  ambapo wafanyabiashara wapatao 40 walinusurika kifo, vijana wahuni wapatao 20 walivamia mabanda hayo wakati wa usiku na kuyachoma moto kwa kutumia petroli, huku wakitoa kauli za chuki na kibaguzi za kuwataka wengi wa wamiliki wake warudi makwao, yaani Tanzania Bara. Inadaiwa pia kuwa wakati wa kufanya uhalifu huo, vijana hao wahuni pia walitoa kauli za kupinga Muungano

.
 Itakumbukwa kwamba katika nyakati tofauti katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, makundi ya vijana wahuni yaliteketeza baa zipatazo saba hukohuko Zanzibar  eti kwa sababu baa hizo zilikuwa karibu na makazi ya watu, licha ya ukweli kuwa wamiliki wa baa hizo walikuwa wakifanya biashara halali na walipewa leseni za biashara hizo na Serikali ya Mapinduzi (SMZ). Inawezekana kwamba vijana hao wahuni walioteketeza baa hizo ndio haohao waliofanya uhalifu huo wa mwisho wa wiki.
   
Ni bahati mbaya kwamba wakati mwingine, SMZ imekuwa haichukui hatua kali na stahiki dhidi ya vitendo hivyo vya kiharamia na kinyume cha sheria. Wakati tukiamini kuwa SMZ inatambua hatari inayoweza kutokea iwapo wahusika wasipochukuliwa hatua, ni bahati mbaya kwamba SMZ haijaonekana ikichukua hatua za kutosha kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo hatari.

   
Ndio maana tunakilaani kitendo hicho cha vijana hao wahuni kilichofanywa mwishoni mwa wiki ambapo mabanda 73 ya wafanyabiashara yaliteketea na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha. Tunalaani kitendo hicho kwa nguvu zote kwa sababu kinatoa taswira potofu kuwa Zanzibar ni nchi isiyokuwa na utawala wa sheria na kwamba haina mazingira mazuri ya kufanya biashara, kwa maana ya kuwakatisha tamaa watalii na wawekezaji ambao wanategemewa sana katika kukuza uchumi wa Zanzibar.
   
Tumefarijika kusikia kwamba zamu hii vijana hao wahuni waliofanya uhalifu huo hawatasalimika. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Masoud Msellem Mtulya ametangaza kuwa hadi sasa watuhumiwa saba wanashikiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani, huku msako mkali wa kuwanasa wengine ukiwa unaendelea.
   
Tumefarijika pia kwamba SMZ imeapa kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika na imeviagiza vyombo vya usalama kulichukulia sualahilo kwa umuhimu na uharaka stahiki. Ndio maana tunampongeza Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi kwa kuyatembelea maeneo husika na kuwafariji waathirika wa uhalifu huo na kutathmini hasara iliyotokea. Tunampongeza kwa kauli yake iliyojaa ujasiri kuwa, pamoja na SMZ kusikitishwa na vitendo hivyo vya kijambazi, wafanyabiashara hao wajione wako nyumbani kwani Watanzania wana haki ya kikatiba kufanya kazi au kuishi mahali popote katika Jamhuri ya Muungano.

   
Kauli hiyo ya SMZ inatupa faraja kwa sababu tatu kubwa: Kwanza, ni ishara kuwa inaanza kutambua kuwa wapo wananchi wanaofanya uhalifu katika visiwa hivyo kwa kivuli cha kutoupenda Muungano. Pili, imetambua ukweli kuwa isipoingilia kati na kukomesha vitendo vya chuki dhidi ya wananchi kutoka sehemu nyingine ya Muungano, umoja wetu utakuwa hatarini iwapo wananchi wa sehemu nyingine hiyo ya Muungano wataamua kulipa kisasi. Tatu, SMZ imetambua kuwa vitendo vya makundi haya ya vijana wahuni mwisho wake ni kusimika vitendo vya kigaidi na uharamia.
   
Sisi hatutakiZanzibar ielekee huko. Na ndio maana tunaipongeza SMZ na vyombo vyake kwa kuapa kutokomeza vikundi vyenye mwelekeokama wa Al Shabab, Taliban na vingine vingi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s