Serikali haijafurahishwa na tukio hilo

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe, Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watu waliopatwa na mkasa wa kuchomewa moto maduka yao huko Pwanimchangani na Matemwe juzi ambapo vibanda vya biashara kadhaa viliteketea kwa moto baada ya watu wasiojulikana kuvichoma moto Mhe, Balozi alitembelea eneo katika maeneo hayo na kwa niaba ya Serikali aliahidi kuchukua hatua zinazofaa kuvikomesha vitengo kama hivyo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia watu waliohusika na matukio hayo ambapo hadi sasa jumla ya watu saba wanashikiliwa na jeshi la polisi

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeviagiza vyombo vya usalama Zanzibar kulishuhulikia ipasavyo suala la kuchomwa moto vibanda vya biashara katika fukwe za Pwani Mchangani na Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Agizo hilo lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika katika maeneo hayo kuangalia hasara iliyopatikana na kuwapa pole waliopatwa na mkasa huo wa kuchomewa moto madanda yao ya biashara.

Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba yake na Serikali kwa ujumla alieleza kusikitishwa kwake kuhusu vitendo hivyo na kuahidi kuchukua hatua zinazofaa kuvikomesha kabla ya kuathiri jamii.

Aliwataka wamiliki wa mabanda ya maduka hayo kutolihusisha suala hilo na ubaguzi baina ya Watanzania Bara na Visiwani kwa dhana ya kuwa wengi wao wanaasili ya Bara kwa kuwa wapo walioathirika ambao ni wazanzibari. Bali wajione kuwa ni Watanzania na wana haki ya kufanya biasharakamawenzao wanavyofanya kwao kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Kuhusiana na ombi la wananchi hao kutaka kupatiwa hifadhi ya muda Balozi Seif aliwapa pole kwa hasara walioipata na kuhusu pahali pa kujistiri kwa wakati huu, na kuwaahidi kwamba Serikali ya Mkoa itawapatia sehemu ya kulala kwa muda wakati serikali ikilishughulikia suala hilo.

Kabla ya hapo katika risala yao waathirika hao waliiomba Serikali kuchukuwa hatua zinazofaa dhidi ya wanaohusika badala ya kuwaona mitaani wakitamba na pia kuomba wapatiwe mahali maalum pa kujenga maduka yao ili waishi kwa amani na kuendelea na biashara zao kama kawaida.

Halikadhalika, katika shukrani zao zilizowasilishwa na mmoja wao  James Chales zilimpongeza Makamu huyo wa Pili wa Rais na Serikali kwa ujumla kwa kufika kuwafariji na hatua wanazochukuwa juu ya kadhia hio hasa kwa ahadi ya kwamba jeshi la polisi kuchukua hatua za kuwasaka wanaohusika na tukio hilo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Naye Charles Pendael Tito alisema wamekuwa wakiishi kwa khofu wakati huu kutokana na kuwa bado watu waliohusika wanaweza kuendelea vitendo hivyo wakati wowote na kuiomba serikali kulichukulia suala hilo kwa umakini kwani linaweza kujirudia tena iwapo serikali itasita kuwachukulia hatua madhubuti za kuwadhibiti wahalifu hao.

Tito aliiomba serikali katika kipindi hiki kuwapatia makaazi mazuri ambayo yatakatoweza kuwasitiri pamoja na watu wawili ambao wameathirika kupatiwa matibabu na wakaazi wengine kuomba kupatiwa magodoro kwa kuwa hivi sasa wanaishi katika maisha ya khofu na yasio na uhakika.

Akizungumza kwa njia ya simu mzee wa miaka 70 wa kijiji cha Pwani Mchangani Ame Haji Ame ameilaumu serikali ya wilaya ya kutokana na kupuuza madai ya wananchi ya muda mrefu ambapo wanalalamikia suala zima la kuwepo vitendo viovu vinavyofanywa na wafanyabiashara hizo alizoziita za kikahaba ambapo alisema vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri kila kukicha.

Alisema mbali ya vitendo hivyo kumekuwepo na uhalifu mkubwa na uharibifu wa mazingira yanayofanywa katika maeneo hayo na fukwe kwa wafanyabiashara hao kufanya vitendo vya biashara ya ngono waziwazi jambo ambalo limekuwa likiathiri jamii ya wananchi wa kijiji hicho ikiwa pamoja na mipira ya kondom kuzagaa na kuchezewa na watoto wadogo ambapo serikali ilishauriwa kukomesha vitendo hivyo lakini imekuwa ikisitasita kuchukua hatua.

“Ndio wananchi wamekasirika kwa sababu kumekuwa kukifanyika vitendo viovu vya biashara ya ngono na hili tumelitamka muda mrefu kuiomba serikali yetu ya wilaya kuichukua hatua lakini serikali imeshindwa kuchukua hatua madhubuti kukomesha vitendo hivi, sasa huwezi kuwalaumu wananchi kwa sababu ndio wanaothirika na madhila haya na jamii inaendelea kuharibika” alisema Mzee huyo.

Kamanda wa polisi mkoa wa kaskaskazini Unguja, Masoud Msellem Mtulya aliwaambia waandishi wa habari kwamba hadi sasa jeshi la polisi limewashikilia watu saba kuhusiana na tukio hilo na wakati wowote watapandishwa mahakamani kujibu shutuma hizo.

Alisema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kuwatafuta wengine wanaohusika na tukio hilo huku akiwaomba wananchi kutoa mashirikiano na jeshi lake ili kuwakamata watu wanaowatilia wasiwasi kuhusika na tukio hilo huku msako mkali ukiendelea ili kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena katika mkoa huo.

Akizungumzia chanzo kinachozungumzwa na wananchi wa mkoa wa kaskazini Kamanda Mtulya alisema baadhi ya wananchi wanadai kulalamikia vitendo vinavyofanywa na wafanyabiashara hizo za vinyago na mama ntilie ukiwemo kuuza madawa ya kulevya, kuuza na uvuta bangi pamoja na biashara ya umalaya katika maeneo hayo ya fukwe na wanafanya biashara maeneo bila ya vibali vya kisheria katika maeneo hayo.

Aidha alisema upande wa walalamikaji waliochomewa moto mabanda yao Kamanda Mtulya alisema wanadai kwamba wamechomewa biashara zao kwa kuwa wao ni watu kutoka Tanzania bara na wananchi wa hapo wamechoshwa na watu hao kuwavamia katika maeneo ya wananchi kwa kufuata biashara za kitalii.  

Kamanda Mtulya alisema madai yote hayo hayana ukweli kwa kuwa maeneo yanayoendesha uhalifu sio hayo pekee katika mkoa wa kaskazini lakini pia suala la kufukuzwa watu wa Tanzania bara halina ukweli kwa kuwa wapo walioathirika katika kuchomewa moto ambayo ni wazanzibari ingawa watu wa Tanzania bara ni wengi katika tukio hilo.

Hata hivyo Kamanda Mtulya alisema suala hilo bado wanalichukulia kama ni la kihalifu na hawawezi kuliwacha likamalizika hivi hivi lakini jeshi la polisi litawakamata wale wote wanaohusika na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria ili iwe funzo kwa wengine wenye kufanya vitendo kama hivyo.

 

Kiasi cha watu 40 wamechomewa mabanda ya maduka yao juzi ambapo mabanda 43 yalichomwa katika ufukwe wa Pwani Mchangani karibu na Hoteli ya Waikiki na 30 yalichomwa Kiwengwa karibu na Hoteli ya Ocean Beach Resort. 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s