Nimesikia kilio chenu

Makamu wa kwanza wa Rais na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akifungua mkutano mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Mjini na kuwataka wananchi kuwa na subira wakati serikali ya umoja wa kitaifa ikichukua hatua ya kupambana na tatizo la mfumuko wa bei za vyakula visiwani Zanzibar.

Maalim Seif bado mgonjwa, ajibu malalamiko ya wananchi

Makamo wa kwanza wa rais  Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad leo alijibu malalamiko kadhaa kutoka kwa wananchi dhidi yake, viongozi, na serikali ya umoja wa kitaifa kuhusu kupanda kwa maisha na kutokuwepo kwa serikali ya kitaifa katika ngazi za chini serikalini.

 Akizungumza katika Mkutano mkuu wa kawaida wa CUF wilaya ya mjini uliyofanyika Ukumbi wa Jamati-Khan mjini hapa, Maalim Seif pia alijibu malalamiko ya wafuasi wake kwamba baadhi ya wabunge na wawakilishi wa CUF hawaonekani katika majimbo tangu kuchaguliwa katika uchaguzi wa mwaka jana.

“Pia nimesikia malalamiko kwamba sionekani, na kwamba viongozi tumekaa kimya kuhusu operesheni ya Darajani ambapo wafanyabiashara waliondolewa. Nafikiri ni vizuri nyie viongozi mkafanya utafiti kabla ya kutulaumu,” Maalim Seif alisema.

Katika kujibu malalamiko hayo, Maalim Seif alisema aliahidi kupunguza bei ya bidhaa hasa chakula iwapo angechaguliwa kuwa rais wa zanzibar , “mimi si rais, ni makamo na ni mshauri tu wa rais. Lakini hata hivyo sisi viongozi tunafanya kazi ili kuleta unafuu kwa wananchi.”

Alisema tatizo la kupanda kwa bei si la zanzibar pekee, ni nchi mbali mbali mfano Kenya na Uganda, na kwamba limesababishwa na kupunguwa kwa uzalishaji duniani na pia tatizo la uharamia wa wasomali ambao wamekuwa wakiteka meli za usafirishaji.

Makamo wa kwanza wa rais ambaye alizungumza ikiwa ni mara yake ya tatu kuzungumza tangu kufanyiwa operesheni ya magoti nchini India, aliwataka wananchi kuondowa wasiwasi juu ya utendaji wa serikali ya umoja wa kitaifa na kwamba mipango inafanywa ili wananchi waishi vizuri.

Maalim Seif Alitaja baadhi ya mikakati ya kupambana na hali ngumu ya maisha kuwa ni kuwashawishi wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza zanzibar, na kuimarisha kilimo hasa cha mpunga wa umwagiliaji ili kupunguza kutegemea kununua kutoka nje.

Pia Maalim seif alisema miongoni mwa mambo mazuri ambayo serikali ya umoja wa kitaifa inaandaa ni kuzingatia swala la kubinafsisha soko la karafuu ili wakuliwa wawe huru kuuza wanapotaka.

Akijibu kuhusu muundo wa serikali ua umoja wa kitaifa (GNU), alisema katiba imeelekeza kuwa mgawanyo wa nafasi ni katika mawaziri na naibu mawaziri, “nafasi nyengine zote zipo chini ya rais kwa mujibu wa katiba. GNU katika kugawana nafasi imeishia juu tu na ndivyo katiba inavyosema.”  

Akijibu shutuma dihi yake za kutoonekana Maalim Seif alisema amepunguza kazi na amekuwa haonekani hadharani kwa sababu bado anaumwa, na kuwataka viongozi wengine wakiwemo wabunge na wawakilishi kuimarisha chama na kuwatumikia wananchi.

“Nasikitika, ni kweli viongozi tumelala, sioni harakati ndani ya chama. Vijana na akimama mmekaa kimya, afadhali ya akina mama. Lazima kazi ya kuimarisha chama ziendelee katika ngazi zote,” alisema Maalim Seif.

Alisema baadhi ya wabunge na wawakilishi wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika majimbo yao, lakini amewaonya wabunge na wawakilishi ambao bado hawajaonesha juhudi za kuwatumikia wananchi, “tutawabana watueleze kwa nini hawafanyi kazi kama wenzao.”

Kuhusu sakata za darajani, Maalim Seif alisema kuwa msimamo wake haujabadilika kuwa “serikali ikihitaji pahala popote ambapo wananchi wanafanya kazi ili kuendesha maisha, ni lazima serikali iwatafutie sehemu nyengine au eneo mbadala kabla ya kuwaondoa”

Makamo wa kwanza wa rais alisema kuwa msimamo wake huo anaendelea nao, na kwamba swala la darajani alisema hivyo. Lakini akasema kuwa katika utaratibu wa serikali kiongozi kama yeye ambaye yumo ndani ya serikali hawezi kutoka hadharani kupinga kinachofanywa na serikali.

Alisisitiza juu ya kuwatendea haki wananchi hasa ambao wamejiajiri katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar, na kwamba si vizuri kukurupuka na kuwatimuwa watu ambao wanapata riziki zao pahala bila ya kuwasaidia kupata sehemu nyengine.

Aidha Maalim Seif alisema katika mkutano huo kuwa serikali imejiimaisha katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya madawa ya kulenya na kwamba mafanikio yameanza kuonekana, na kuwataka wananchi kusaidia katika vita hivyo ili lengo la serikali lipatikane katika kupunguza na kukomesha madawa ya kulevywa kuingizwa nchini ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri nguvu kazi ya taifa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s