Upepo mpya, zama mpya, kizazi kipya

Jabir Idrissa Yunus Ni Mwandishi Mwandamizi na sasa ni Mhariri wa gazeti la kila wiki liitwalo Mwanahalisi linalochapishwa huko Tanzania Bara.

NI dhahiri sasa muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefikia kiwango cha juu kabisa cha kudhoofika. Kama ilivyo ngoma inapolia sana, uko nchani kuvunjika.Huko nyuma waliokuwa wakiusema muungano, hata kama ni kwa nia njema ya kuuimarisha, walikuwa ni wale walioitwa wapinzani wa serikali.

Wengine walitambuliwa kama wapinzani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachoshika madaraka tangu Februari 2, 1977 kilipozaliwa kutokana na TANU na ASP kuunganishwa.

Hali ni tofauti leo. Mawaziri wawili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, waziri wa zamani na mwakilishi wa CCM, wanataka ujadiliwe.

Na mtihani mkubwa unaojitokeza katika tarehe hasa ambazo muungano ulikuwa unaandaliwa kwa siri kubwa – Aprili, miaka 47 iliyopita, umechochewa na CCM wenyewe.

Muungano uliasisiwa rasmi Aprili 26, 1964, zilipounganishwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.Tatizo kubwa la wakuu wa CCM ni kutosikiliza. Kama wanasikiliza, basi hawazingatii wanachosikia. Wanapuuza maoni ya watu wanaouangalia tofauti na vile wanavyoangalia wao.

CCM wamekuwa wakiamini kile tu wanachokiamini wao. Kwa muda wote wa uhai wake, chama hiki kimeshindwa kutambua hisia za wananchi, wale wa Zanzibar ambao imekuwa kawaida kuonekana wapingaji wakubwa, bali pia Bara.

Ushahidi. Serikali yake – inaundwa na wanachama wa CCM tu – imeleta muswada wa sheria kwa haraka isivyo kawaida kama vile jambo la katiba ni la dharuraIngawa wanasema mabadiliko ya katiba si ajenda yao ndio maana hawakuweka katika Ilani ya Uchaguzi 2010, walipoamua kuichukua ili kuifanyia kazi, wamekuja na muswada unaokera wengi – Bara na Zanzibar.

Zanzibar wanaona wameguswa zaidi. Katika kujadili muswada wa sheria ya marejeo/mapitio ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 2011, viongozi wa serikali na wanaharakati, wanaonyesha hasira na wanashuhudisha malalamiko yao.

Mawaziri wawili wanasema serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeandaa muswada bila kuishirikisha Zanzibar. Kwao ni dharau.Mansour Yussuf Himid na Abubakar Khamis Bakary, wanasema muswada haufai, umeandaliwa katika utaratibu usiokubalika kisheria na uondolewe bungeni.

Mansour ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kiembesamaki, Unguja. Ni waziri wa kilimo na maliasili na kijana wa CCM.
Abubakar ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Mgogoni, kisiwani Pemba. Ni waziri wa katiba na sheria na mwanasiasa mkongwe wa Chama cha Wananchi (CUF).

Si kawaida Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar kuzungumzia muungano hadharani. Leo, aliyepo baada ya kuteuliwa hivi karibuni, Othman Masoud Othman, anathubutu.
Othman, aliyetoka kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2002, akijadili muswada huo ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani, alisema maandalizi yake hayakufuata sheria.

Anasema Bunge lililopo haliwezi kutunga Katiba mpya, bali kurekebisha vifungu vya katiba iliyopo. Kazi ya kutunga katiba kwa mujibu wa sheria itafanywa na bunge maalum litakaloundwa kwa ajili hiyo.Ni msimamo wa serikali maana yeye ni mshauri mkuu wa masuala ya kisheria wa serikali inayoundwa na vyama viwili, CCM na CUF, vilivyoingia katika maridhiano yaliyoidhinishwa na wananchi Julai mwaka jana.

Kama Mansour, Hamza Hassan Juma, waziri wa serikali iliyopita na mwakilishi wa Kwamtipura (CCM), naye anaupinga kwa kuwa SMZ haikushirikishwa kuuandaa.

Mansour: “Kitendo cha kamati (Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge) kuwaita watu kuja kutoa maoni, ni sawa na kuwadanganya. Zanzibar watapinga muswada iwe katika Baraza la Mapinduzi (BLM), hadharani au katika kikao cha faragha.”

Hamza: “Haufai maana haumtambui Rais wa Zanzibar kama ni mamlaka ndiyo maana anatajwa kama anayeweza tu kushauriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hii ‘anaweza’ (may) ina maana si lazima, ingekuwa ‘shuruti’ (shall) ingeeleweka.”

Abubakar, mtaalamu wa sheria aliyeandika Katiba ya Zanzibar, 1984, anasema uandaaji wa muswada umekiuka makubaliano ya msingi ya muungano.“Kwa mujibu wa makubaliano hayo, jambo lolote linalotaka kuongezwa au kuondolewa (katika orodha ya mambo ya Muungano) lazima pawepo makubaliano ya pande mbili, kwa hili la kuandaa muswada wa katiba, haikufanywa hivyo.

“Nasema serikali ya Zanzibar hatukushirikishwa. Muswada huu haufai. Uondoshwe kwenye meza ya spika,” anasema na kuchangamsha wasikilizaji alipoapa ataupinga na atashawishi wananchi wa Mgogoni waupinge.Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Omar Dadi Shajak, anasema, “Taratibu hazikufuatwa. Mchakato wa muswada huu haukubaliki.

“Muswada uko upande mmoja tu wa Tanzania Bara. Hii ni kudharau mamlaka ya Zanzibar … urejeshwe bungeni na utengenezwe tena… hivi ulivyo haukubaliki kabisa.”
Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee anasema wakati Katiba inatoa uhuru wa kujadili suala la Muungano, muswada unapendekeza muungano usijadiliwe. Anahoji: “Ipi yenye nguvu; Sheria au Katiba?”

Wanaharakati wanachanachana muswada. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), Sheikh Farid Hadi Ahmed, anataka SMZ iupuuze; iitishe kura ya maoni kuwauliza Wazanzibari wanautaka au laa.

Mwanazuoni huyu anainua muswada na kuuchana mbele ya waheshimiwa wakiongozwa na Samia Suluhu Hassan, mbunge wa Makunduchi, waziri wa Muungano, na mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge.

Yupo pia Samuel Sitta, mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), Waziri wa Afrika Mashariki na Mjumbe wa Kamati ya Bunge. Akiwa ndiye aliyeusoma muswada ili ujadaliwe, Sitta alipata huzuni na hofu kubwa kuona unachanwa. Mjadala uliishia hapo, naye akalazimika kusindikizwa na polisi kutoka ukumbini.

Samia, aliyeingia katika siasa mwaka 2000 kama mwanamke wa harakati wa haki za binadamu, akawaita waliochana muswada “wahuni” walioandaliwa makusudi.Ni muungano unaopata mtihani huu. Kwa miaka yote umekuwa ukiendeshwa kwa vitisho na ubabe. Hata baada ya Zanzibar kukoseshwa rais wao mwaka 1984, Mzee Aboud Jumbe, kwa kuuhoji, watawala wanaendelea kuahidi kuulinda kwa gharama na nguvu zote.

Mzee mmoja alipochangia mjadala wa muswada kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita, alisema, “Hapa hakuna sababu ya kutajwa Rais wa Zanzibar. Wenzetu wana katiba yao, sawa! Ile ni ya mambo yao. Hii ni katiba ya Muungano. Tuacheni.”

Mchangiaji mwingine alijadili kifungu cha 16 cha muswada na kusema: Hakuna sababu ya kumpa ripoti Rais wa Zanzibar. Si yupo Makamu wa Rais anayewakilisha Zanzibar, apewe huyo inatosha.Kipengele cha pili cha kifungu hicho kinasema akishapokea ripoti ya tume, Rais atakabidhi nakala kwa Rais wa Zanzibar.

Huu ni upepo mpya ndani ya zama mpya na kizazi kipya. Kinataka muungano wake si wa wazee wale. Zanzibar wanataka au hawataki muungano huu. Wanaitaja Tanganyika ndio mshirika wao. Hawamuoni.Bali Bara ambao ungetarajia wakawa mbele kuidai Tanganyika, wala hawaitaji kwamba iwepo. Wanajadili katiba ya Tanzania.

Lakini muungano hautakiwi kujadiliwa kulingana na muswada. Ushahidi wa CCM kutosikiliza, au kutozingatia maoni ya watu. Itabakia na muungano chuki tupu.

Advertisements

One response to “Upepo mpya, zama mpya, kizazi kipya

 1. Naungana na maneno yako kwamba kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho. Haswa pale ambapo jambo hilo huwa halileti haki sawa au lina ukandamizaji ndani yake. Mfano mdogo ni huu wa Mkoloni Mweupe, vugu2 lilipoanza halikusimama tena hadi nchi zote za Africa kupata uhuru.

  Na hii miungano sio siri tena bali sasa umekuwa ukiwakera hata wana CCM. Na hii nikutokana na kwamba Wazanzibari wengi wanaelewa ni wapi Tanganyika inataka kutupeleka. Na hapa tulipo kila mtu hamiliki hata kijio chake cha siku moja kama ni mwananchi wa kawaida. Wakati wenzetu bara wanachezea pesa. Na maisha yamekuwa 80% better than the way Zanzibaris normal life is.

  Wakati umefika wakutumia siku hii ya Sherehe ya Muungano 26.4.2011. Kama tunavojua kwamba Wazanzibari walikua wanataka kutuma ujumbe azimu unaohusu Uchoshwaji wa Muunano hewa. Lakini walinyimwa kibali cha kufanya maandamano hayo. Sasa namweambia shekh Farid na wazalendo wengine walioko nyumbani kwamba.

  1. Tarehe 26.4.11 sherehe zinafanywa Unguja, na kutakuwa na wageni kutoka balozi mbali mbali kujionyesha kwamba Tanzania /Tanganyika ina muungano unaopendwa na watu. Sasa Ujumbe wetu nikuchukua mabango yenye ujumbe wa kupinga Muungano.Yatakayoandikwa kwa lugha mabali2 kwamba: hii ni mifano ya lugha ya Ki-swahili, Ki Danish na Kingereza

  1.Muungano sio halali.
  a). Vi kan ikke lige udloulig uniun mellem Tanganyika og Zanzibar.
  b). The Unioun between Tanganyika & Zanzibar its illegal.

  2.Wazanzibari wanataka mjadala wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika, na sio marekebisho ya katiba.
  a). Zanzibaris need to discuss the Uniun between Zanzibar & Tanganyika & not the Constitution Ammandement.
  b). Zanzibaris vil gerner diskuter Uniun mellem Zanzibar ogTanganyika, end det ikke Tanganyikans Magt.

  3. Ukowapi Mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tunataka uwekwe wazi.Muungano huu una uhalali?
  a). Where is the Tanganyika & Zanzibaris Uniun Agreements, we need to see it, if this uniun are still legal.
  b) Vhor er Uniun kontrakt hen? Zanzibaris ville gerne at se den. hvis ar lovglig

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s