Tunaipongeza CCM

Mwasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mzee Hassan Nassor Moyo alisema ni mabadiliko yaliyokuja katika wakati muafaka kwa kuwa hivi sasa CCM lazima ijipange upya katika safu zake za uongozi ili kurejesha imani kwa wanachama wake kulingana na wakati husika

BAADHI ya wazanzibari wamefurahishwa na mabadiliko yaliofanyika ndani ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa ni hatua moja wapo ya kupanga safu ya uongozi makini hasa katika ushindani wa uchaguzi wa ujao wa 2015.

Mweka hazina wa CCM Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid amesema ameridhishwa na mabadiliko hayo kwa kuwa itasaidia kukiunganisha chama hicho ambacho kilikuwa na makosa madogo madogo katika uongozi.

“Mimi nimerishwa sana na mabadiliko yaliotokea kwanza ni kukiimarisha chama chetu, pili ni kujipanga upya lakini pia ni kurejesha imani kwa wanachama ambao walikuwa na wasiwasi wa hapa na pale kutoka na maneno mengi yaliokuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni…nimeridhishwa sana” alisema Mansoor.

Naye Mwasisi wa Chama Cha Mapinduzi Mzee Hassan Nassor Moyo alisema ni mabadiliko yaliyokuja katika wakati muafaka kwa kuwa hivi sasa CCM lazima ijipange upya katika safu zake za uongozi ili kurejesha imani kwa wanachama wake kulingana na wakati.

“Mimi binafsi nimefurahishwa sana na mabadiliko hayo…yamekuja wakati muafaka ambapo chama chetu kimeyumba tangu wakati wa uchaguzi mkuu kiasi ya wapinzani kujisifu na kupita kifua mbele lakini kwa sasa itasaidia zaidi kukiimairisha chama chetu” alisema Mzee Moyo.

Alisema CCM bado ni chama imara na kikipendwa na wafuasi wengi hivyo kinatakiwa kurudisha imani ya wanachama na wananchi kwa sababu kuendelea kulumbana kunaweza kuhatarisha uhai wa chama hicho kikongwe ambacho kilijipatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi.

Mzee Moyo aliupongeza uteuzi wa katibu mkuu Wilson Mukama na kusema ni kada hodari mwenye uwezo wa hali ya juu ambaye atasaidia kurudisha imani ya chama kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Mzee Moyo ambaye ni muasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar na aliwahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Mzee Abeid Karume alisema aliwaambia waandishi wa habari kwamba Mukama ni kada wa siku nyingi katika chama hicho na amekitumikia chama kwa imani kubwa sana hivyo matumaini yake makubwa kwamba ataweza kuhimili uendelezaji wa chama hicho na kukabiliana na mawimbi yalopo hivi sasa.

Alisema imani yake juu ya kiongozi huyo ni kubwa ambapo anaamini kwamba imani ya wananchi na wana CCM ambayo ilianza kutetereka kidogo kufuatia matatizo yaliojitokeza hivi karibuni itarudi na chama hicho kipevu kitatulia na kuwa shuwari kutokana na uongozi makini uliochaguliwa.

Akimzungumzia Vuai Ali Vuai ambaye ni naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Mzee Moyo alisema ana uwezo mkubwa wa kukabiliana na vishindo vya wapinzani na kamwe sio mtu moga na mwenye kushindwa katika kazi zake hivyo anaamini ataweza kazi aliyokabidhiwa na matarajio yake kuwa ataifanya vizuri zaidi.

“Nimefurahia uteuzi wa Vuai kwa sababu binafsi siku zote nilikuwa nikisema CCM Zanzibar ni sawa na iliyokufa….Vuai anakabiliwa na kazi kubwa ikiwemo kurudisha imani ya wanachama ambao walikuwa tayari wamekata tamaa baada ya kupuuzwa kwa maoni yao na mchangao wao na viongozi waliokuwepo’alisema Moyo.

Mwengine ambaye amekitumikia chama cha CCM kwa miaka mingi na aliyewahi kuwa katibu mkuu wa umoja wa vijana (UVCCM) Mzee Sukwa Said Sukwa alipongeza sana mabadiliko yaliofanyika na kusema kwamba sasa CCM itakuwa na mabadiliko ya kiutendaji kwa kuwa safi iliyochaguliwa ni mzuri na ya wachapa kazi.

Alisema viongozi wote walioteuliwa ni wazuri na ni wazoefu katika chama hivyo kwa kuwa chama kimekabidhiwa wachapa kazi kazi zitafanyika hasa kwa upande wa Zanzibar ambapo kwa muda mrefu kulionekana kusuasua na kuzorota ingawa sio kwa kasi ikilinganishwa na huko nyuma.

Sukwa ambaye alikuwa katibu mkuu umoja wa vijana katika mwaka 1990 alisema chama cha mapinduzi Zanzibar kimeyumba sana kwa sababu kimekuwa kikipambana na nguvu za upinzani za chama cha CUF kwa muda mrefu.

Hivyo kilikuwa kinahitaji nguvu za mtu ambaye atafanya kazi kubwa ya kuimarisha umoja wa wanachama pamoja na kukiimarisha chama kuanzia china huku wazee wakipewa nafasi kubwa ya ushauri na sio kupuuzwa.

“Tunampongeza sana Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi na timu yake ya wazee….uteuzi uliofanywa ni sahihi hauna matatizo …sisi wazee tulikuwa na kiu ya timu nzuri ndani ya chama ambayo itaweza kuhimili vishindo vya wapinzani kwa sababu miaka ya zamani na sasa ni tofauti wakati wetu na sasa so sawa zamani chama kilikuwa kimoja tu na hakuna upinzani lakini sasa lazima wapatikane viongozi mahiri sana ili waweze kukabliana na ushindani” alisema Sukwa.

Mwenyeiti wa baraza la waze la chama cha Mapinduzi Makao makuu CCM Kisiwandui Zanzibar, Makame Mzee amefurahishwa sana na mabadiliko hayo huku akisema chama ni watu na sio viongozi hivyo kubailishwa viongozi watakaoweza kufanya kazi kwa mashirikiano ni muhimu sana.

Makame ambaye alipata kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi katika miaka ya 1972, alisema mabadiliko yaliyofanywa zaudi kwa upande wa Zanzibar yatasaidia kuimaisha chama kwa kuwakutanisha makundi yote akiwemo wazee na vijana.

“Huyu Mukama namfahamu sana mie na huyo Vuai pia ni kijana wangu namfahamu sana ni matunda ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi…..tutakwenda naye sambamba sisi wazee pamoja na vijana tutawaongoza ili waweze kulipeleka jahazi letu vizuri” alisema Mzee Makame.

Katibu msaidizi mwandamizi wa chama cha mapinduzi idara ya itikadi na uenezi Zanzibar, Ali Mwinyi Msuko alisifu uteuzi wa Katibu Mkuu Mukama na kusema ni kada mahiri ambaye alikuwa akitoa mada mbali mbali zilizokuwa zikisaidia kuimarisha chama cha mapinduzi katika makongamano mbali mbali ya kisiasa.

Aidha alisema naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ni kada maarufu aliyefanya kazi katika umoja wa vijana (UVCCM) kwa muda mrefu.

Vuai alikuwa kaimu naibu katibu mkuu umoja wa vijana Zanzibar katika mwaka 1996,hadi katika mwaka 1998 ambapo alikuwa katibu Mkuu wa Umoja wa vijana (UVCCM) taifa.

Kwa sasa ni mkuu wa idara ya itikadi na uenezi ya kamati maalumu ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar,huku akiwa mkuu wa wilaya ya kaskazini B Unguja.

Kwa ujumla wanachama wa chama cha Mapinduzi wa kawaida wamesifu mabadiliko hayo ambayo wamesema yatakinusuru chama na kukubalika kwa wananchi.

Aidha wafanyakazi wa makamo makuu ya CCM Kisiwandui wote walionekana na nyuso zenye furaha na bashasha kubwa kufuatia mabadiliko hayo na kwa ujumla walisema wanamkaribisha naibu katibu mkuu mpya na wamepanga maandalizi ya kuwapokea viongozi wapya waliochaguliwa huko Dodoma hivi karibuni.

Wafanyakazi takriban wengi wakwemo wazee walikuwa wakilalamikia uongozi wa naibu katibu mkuu Saleh Ramadhan Ferouz kwamba hana mashirikiano na wazee wameshawahi kumuandikia bara Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kwamba wamechoshwa na uongozi wake na kumtaka amuondoshe katika wadhifa huo.

Licha ya barua hiyo aliyoandikiwa mwenyekiti na wazee hao kulalamika katika vyombo vya habari Ferouz alikuwa akikingiwa kifua na makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Amani Abeid Karume

Naibu katibu mkuu wa zamani Ramadhan Saleh Ferouz yupo katika hatua za mwisho za kukabidhi ofisi kwa naibu katibu mkuu mpya ambaye anatazamwa kuwasili hapa kutoka Dodoma leo.

Advertisements

One response to “Tunaipongeza CCM

  1. mimi sio hata mtu moja alaiyesema kuhusu wanachi wa znz mm naona watu tu wanalumbana kwenye vyio kila moja anataka uluwa huyu hamtaki yule na yule hamtaki huyu almuradi bala tu watu wanakufa kwa njaa znz huku viongozi wa chama wanavutiyana uluwa basi hakuna lolote njaa tu inawapeleka mbio na uluwa mwingi basi hakuna hata mtu moja aliyesema ss chama kimejipanga hawa ndio viongozi watakao saidia wanchi hakuna ni kingozi huyu hafai anatutharau na kiongizi yule anatamba kifuwa mbele nini jamaa mtakufa mtasahau hata kupiga shahada kwa kukumbuka vyeo vya chama wacheni hayo malumbano jengeni nchi kama alivyo fanya MZEE KARUME kajenga na watu wanaona sio domo tupu miaka nenda miaka rundi hakuna lolote munalolifanya.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s