Tunamkumbuka Muasisi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Mrisho kikwete,akisalimiana na Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza hapa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,baada ya hafla ya hitma ya kumbukumbu yake iliyofanyika Kiswandui kwenye ofisi kuu ya CCM Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein jana ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.Hitma hiyo pia,  ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais msataafu wa Jamhuri ya Muungano Ali Hassan Mwinyi na wanafamilia ya marehemu mzee Abeid Amani Karume.

Wengine ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi pamoja na  Mabalozi wadogo  waliopo hapa Zanzibar.

Hitma hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu Suratul Fuswilat, iliyosomwa na Ustadh  Sharif  Abdulrahman na kuongozwa na Sheikh Mohammed Kasim kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Thabit Noman Jongo alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyewatetea wanyonge na aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Alieleza kuwa katika uongozi wake, marehemu mzee Abeid Karume aliwajali watu wote kwa nafasi zao wakiwemo wazee, vijana, walemavu, wavuvi na watoto mayatima ambapo pia alifanya juhudi za kuhakikisha wote hao wanaishi katika mazingira bora.

“Aliyoyafanya mzee Karume sisi hatuna cha kumlipa isipokuwa ni kumuombea  dua Mungu amlaze mahala pema peponi, Amin”,alisema Sheikh Jongo.

Aidha,  Sheikh Jongo alieleza kuwa  juhudi za viongozi waliotangulia nchini  ndizo zinazopelekea hadi leo Zanzibar kuweza kupata maendeleo makubwa na kusisiti za kuwa Zanzibar ni njema atakaye aje.

Viongozi wengine ambao pia, walihudhuria katika hitma hiyo ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali  Devis Mwamunyange, muwakilishi wa familia ya Baba  wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere, Madaraka Nyerere alihudhuria pamoja na Jaji Mkuu mstaafu, Agostino Ramadhan, mzee Kingunge  Ngombale  Mwiru, Naibu Kadhi Mku wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Naibu Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kabhi Sheikh  Mussa Salum kutoka Mkoa wa Dar-es-Salaam nae alihudhuria.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, April, viongozi hao na wananchi walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini mbali mbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Akitoa salamu na dua kutoka madhehebu ya Kanisa Katoliki Askofu Augostine Shao aliwataka wazanzibari watumuenzi kwa dua nzuri Mzee kwa Karume kutokana na mema yake aliyowatendea wazanzibari na kuwataka viongozi wapya wafuate mfano wake wa hamu ya kutaka kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema Mzee Karume aliipenda nchi yake na kuwa na kiu ya maendeleo ambapo alitaka wananchi wote wapate haki ya kuishi katika nchi yao bila ya vikwazo ikiwa pamoja na kupata huduma za kijamii ikiwemo maji, afya na elimu bila ya ubaguz.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Balozi Ali Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi .

Aidha mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, alishiriki katika hitma hiyo akiongozana na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete, Mama Asha Balozi na Mama Pili Balozi na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na risasi akiwa nje ya ukumbi wa afisi kuu ya chama cha ASP Kisiwandui Mjini Unguja na kukimbizwa hospitali lakini madaktari hawakufanikiwa kuokoa maisha yake.Marehemu Karume alizikwa Aprili 10 hapo hapo Kisiwandui.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s