Umesikia habari ya sukari

Mwakilishi wa nafasi za wanawake Bi Mgeni Hassan Juma (kulia) akizungumza na naibu waziri wa Afya na mwakilishi wa kuteuliwa na Rais Bi Sira Ubwa Mamboya baada ya kutoka katika ukumbi wa baraza la wawakilishi leo

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema hakuna uzalishaji wa sukari unaofanyika kwa sasa tangu kiwanda cha sukari cha Mahonda kukabidhiwa kwa muwekezaji katika mwaka 2005.Tatizo kubwa ni kuchakaa kwa mitambo ukiwemo wa kutengeneza mvuke ambao huzalisha kiwango kidogo cha joto.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Thuwaiba Endington Kisasi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa jimbo la Kwahani Ali Salum Haji (CCM) aliyetaka kujuwa maendeleo ya kiwanda cha sukari tangu kuchukuliwa na muwekezaji.

“Nini chanzo cha migogoro kati ya wananchi wa Mahonda na Mwekezaji wa kiwanda cha sukari? Na kwa kuwa Mwekezaji huyo anaonekana ni mbabaishaji jee wizara haioni sababu ya kupitia upya mkataba wake na mwekezaji huyo na ikiwezekana kuuvunjwa? Alihoji Mwakilishi huyo.

Thuwaiba alisema wizara yake inafahamu kwamba kiwanda cha cha sukari Mahonda hakizalishi sukari kutokana na uchakavu wa kiwanda, kumekuwepo kasoro katika mtambo wa kuzalisha mvuke ambapo huyo kiwango kidogo cha joto ambacho hakifikii kiwango kinachotakiwa ili kukausha sukari ipasavyo.

Akitoa ufafanuzi zaidi Thuwaiba alisema kiwanda hicho kwa mara ya kwanza kilizalisha jumla ya tani za sukari 100 katika mwaka 2008 ambazo hata hivyo hazikuwa na ubora wa kiwango kinachokubalika katika soko la biashara kutokana an kasoro za huo mtambo wa mvuke ambao ni wa zamani na unaotumia nishati ya kuni nyingi na mafuta ya dezeli nzito ambayo ni ghali.

Alisema kwamba hivi sasa mwekezaji kwa msaada wa UNDP anaendelea juhudi za kutafuta mtambo mwafaka kwa ajili ya uzalishaji wa sukari huku akiendelea na uzalishaji wa spiriti pekee.

Akizungumzia migogoro ya mwekezaji au uongozi wa mradi na wananchi wa Mahonda pamoja na vijiji vyengine vinavyopakana na mashamba ya miwa, Naibu huyo alisema inatokana zaidi na masuala ya ardhi ya mashamba hayo ambayo ingawa mradi umekabidhiwa rasmi kwa ajili ya upandaji miwa baadhi ya wananchi nao huyavamia mashamba hayo na kulima bila ya ridhaa ya uongozi wa wenye mradi.

Thuwaiba alisema baadhi ya wakati zinajitokeza dalili za wazi za uchomaji moto wa miwa au uchungaji wa mifugo katika mashamba jambo ambalo linasababisha hasara kwa kiwanda na kuendeleza migongano zaidi na ni wananchi ndio wanaoshutumiwa kuhusika na hujuma hizo.

Alisema wizara yake katika kufuatilia kwa kina masuala ya kiwanda cha sukari Mahonda chini ya mwekezaji aliyepo sasa ni kwlei inaonekana kuna matatizo mengi lakini hakuna dalili yeyote inayoashiria kuwa mwekezaji huyo ni mbabaishaji.

Matatizo anayokumbana nayo, Naibu huyo alisema ni ya kweli na ya msingi ambayo yangeweza kuathiri mradi wowote wa aina hiyo.

Alisema serikali inaamini kwamba uendelezaji wa mradi wa kuzalisha sukari katika kiwanda cha Mahonda ni jambo la faida kwa taifa kwa mwekezaji mwenyewe na kwa wananchi wa Zanzibar .

Na zaidi kwa wale ambao hupata ajira katika mradi huo ambapo jambo la msingi kwa sasa ni kuendeleza juhudi za kuziondoa kasoro zinazojitokeza na kutoa msaada unaohitajika kwa wenye mradi ili mradi uweze kuzalisha sukari kama ulivyotarajiwa.

Alisema katika kufikia hali hiyo mashirikiano ya viongozi na wananchi wanapakana na maeneo ambayo mradi huo upo ni muhimu sana na kwa hivyo serikali imewaomba viongozi wa ngazi zote wakiwemo wawakilishi, wabunge na viongozi wa serikali yam ka na wilaya ya kaskazini kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha na kuwashajiisha wananchi kuunga mkono juhudi zinazopelekea kiwanda kufanikiwa kwa faida ya wote.

MSWAADA WA MADAWA YA KULEVYA

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameelezwa kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekusudia kuwasilisha mswaada wa sheria ya madawa ya kulevya kuifanyia marekebisho makubwa ili iweze kukabiliana na wimbi la matumizi na uingizaji wa bidhaa hiyo.

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul-habib Fereji amesema hayo wakati akijibu swali nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni (CCM) Mahmoud Mohamed Mussa aliyetaka kujuwa serikali inadhibiti vipi tatizo la madawa ya kulevya wakati njia kuu zinazopitisha hazina udhibiti unaostahiki.

Fereji alisema sheria ya madawa ya kulevya no.9 ya mwaka 2009 itafanyiwa marekebisho ya sheria hiyo ili kuona inakuwa na meno ya kupambana na tatizo hilo kikamilifu.

“Mheshimiwa naibu spika hivi karibuni tutakuwasilisha mswada wa kupambana na madawa ya kulevya katika baraza la wawakilishi lengo ni kudhibiti wimbi la matumizi na uingizaji wa madawa ya kulevya hapa kwetu kwa sababu limekuwa kero kwa vijana wetu wengi wanaathirika” alisema Fereji.

Akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Matemwe (CCM) Abdi Mosi Kombo aliyetaka kujua kwa nini imeshindikana kuzuwia uingizaji, usamabzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya, Fereji amesema licha ya jitihada mabli mabli za serikali za kupambana na uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi katika njia kuu za usafiri bado uingizaji unaendelea kushamiri.

Waziri huyo alikiri kwamba duniani kote harakati mbali mbali za usafirishaji na uingizwaji wa madawa ya kulevya hufanywa katika njia na mazingira ya usiri mkubwa na wahusika hutumia kila mbinu ili kuhakikisha kwamba wanazorotesha harakati za mapambano dhidi yao na hivyo kudumisha na kuendeleza biashara haramu ya usafirishaji ya madawa kwa nguvu zote.

Zanzibar nayo ikiwa ni sehemu ya dunia nayo imejikuta kuwa na changamoto nyingi katika harakati za udhibiti wa uingizaji wa madawa ya kulevya nchini.

Huku sababu kubwa iliyopelekea kupata mafanikio makubwa ikielezwa katika harakati za kuzuwia na kukomesha uingizaji wa madawa nchini serikali inaamini ni kwa kukosekana muundo madhubuti wa tume ya kudhibiti madawa ya kulevya nchini.

“Muundo huo umezingatia zaidi kurekebisha tabia na kutoa taaluma kwa waathirika wa madawa ya kulevya kwa kuzingatia kuwa mapambano dhidi ya madawa ya kulevya yanahusisha taasisi mbali mbali imebainika kutokuwepo kwa ushirikiano wa dhati baina ya taasisi husika yaani tume ya kupambana na madawa ya kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama na mahakama” alisema waziri huyo.

Alisema kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo serikali ya awamu ya saba imeipa dhamana ofisi ya makamu wa kwanza wa rais kushughulikia na kuratibu masuala ya madawa ya kulevya nchini ili kupata nguvu ya kiutendaji na kisiasa.

“Nataka kukuhakikishieni kwamba ofisini yangu imejipanga vyema kupunguza ana kukomesha kabisa uingizaji wa madawa ya kulevya nchini, tunaamini kuwa Zanzibar bila ya madawa ya kulevya inawezekana” alisema Fereji.

Waziri huyo alisema ni dhahiri kwamba hakuna taifa lolote duniani lingependa kuona vijana wake wakijiingiza katika vitendo ambavyo vinawaletea madhara ikiwemo hilo la matumizi ya madawa ya kulevya ambalo limekuwa ni kichocheo kikubwa cha maradhi ya ukimwi na magonjwa ya akili na hata vifo.

Serikali imekuwa ikichukua juhudi za makusudi na kuongeza kazi katika kukabiliana na tatizo hilo baadhi ya mikakati ambayo serikali imekuwa ikifanya katika kukabiliana na tatizo hilo ni kuipa dhamana ofisi ya makamu wa rais kushughulikia suala zima la kupambana na madawa ya kulevya nchini, kufanya mapitio ya marekebisho ya sheria namba 3 ya mwaka 2003 ya udhibiti wa madawa ya kulevya Zanzibar ambayo imetoa msisitizo mkubwa katika kukabiliana na usafirishaji na utumiaji wa madawa hayo.

Alisema msisitizo mkubwa umewekwa kupitia mpango wa kuendeleza zoezi la uhamasishaji katika jamii, kupitia kamati za sheria za ulinzi shirikishi jamii, vipindi vya radio na televisheni na ziara za mashuleni.

Waziri huyo alisema serikali kupitia idara ya kupambana na madawa ya kulevya na kurekebisha tabia imeweza kuwa na mpango maalumu wa kuwashajiisha na kuwapatia mafunzo vijana walioachana na matumizi ya madawa ya kulevya ili kusaidia katika harakati za kuendeleza utoaji wa huduma za mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.

“Mpango huo ni mpango ambao umesaidia katika kuwatoa vijana zaidi ya 70 waliokuwa katika matumizi ya madawa hayo kupitia utaratibu wa mpango wa kuwafikia wale watumiaji waliopo nje ya mfumo wa huduma, vijana wanaoendelea kutumia madawa ya kulevya katika jamii.

Alisema mpango maalumu wa kuwaendeleza vijana walioachana na madawa ya kulevya umeandaliwa ambapo jumla ya vijana 20 wamo katika mafunzo ya awali ya compyuta chini ya ushiriki wa taasisi ya International Youth Challenge ya nchini Canada ambapo vijana 17 tayari wameshahitimu mafunzo hayo hivi karibuni.

Fereji alisema msisitizo pia umewekwa katika kuwa na mpango maalumu unaowalenga wazee parent’s Support Programme wenye vijana wanaotumia madawa ya kulevya ambao mara nyingi hujikuta katika hali ya mfadhaiko na kukabiliana na changamoto nyingi wanapokuwa na kijana mtumiaji wa madawa ya kulevya.

Waziri huyo alitoa msisitizo maalumu kwa jamii ya Zanzibar kuungana katika kupiga vita harakati za uuzaji wa madawa ya kulevya katika maeneo yote, kwani imefika wakati kwa jamii kufahamu kwamba vijana wengi wanateketea huku ikishuhudiwa harakati za uuzaji wa madawa hayo zikiendeshwa jirani na makaazi ya watu.

“Ni wakati wa kuungana pamoja kuwa waadilifu, kuacha muhali, kuchukua kwa dhati vitendo hivyo na pia kuwafichua na kuwaona sio majirani wema na marafiki wa kweli wale wote wanaoendesha harakati za uuzaji wa madawa hayo katika maeneo yetu” alisema waziri huyo

Advertisements

One response to “Umesikia habari ya sukari

  1. Huyu naibu waziri ana uzoefu wa wizara husika au basi ndio mtu wetu tusimtupe kupeana vyeo kijomba jamani hivi kweli tutafika tumeifanya serikali kama ngarawa ya juma faraji kila ajae ingia hivi kweli ccm hawana mtu mwenye uzoefu wa biashara zaidi ya huyo GNU onesheni vitendo sio maneno mengii…..

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s