Jaji soma vizuri vifungu hivi:

Rais wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Yahya Khamis Hamad

Our Ref: ZLS/Council/07/2011 29th March, 2011

Katibu Mkuu Kiongozi
Baraza la Mapinduzi
Ikulu – Zanzibar

KUH: INDHARI YA KUISHTAKI SERIKALI NA MAJIBU YA
JAJI MKUU WA ZANZIBAR

Tarehe 21 Februari 2011 tulitoa indhari juu ya nia yetu kutaka kuishtaki Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na uteuzi wa Jaji Mkuu ambao sisi tunaamini haukuwa halali kikatiba. Nakla ya indhari hiyo ilitumwa kwa Mhe. Jaji Mkuu. Kwa barua yake ya tarehe 17 Machi, 2011 Mhe. Jaji Mkuu ameamua kuijibu indhari hiyo na barua hiyo imeingizwa katika gazeti la Zanzibar Leo ili Wazanzibari wapate kujua yanayoendelea katika nchi yao. Kutokana na majibu ya Jaji Mkuu kujenga taswira isiyo sahihi kikatiba ndio na sisi tumeamua kuzijibu hoja za Jaji Mkuu, Mhe. Hamid Mahmoud.

Hoja yake ya kwanza kuhusu kuendelea na Ujaji Mkuu wakati ameshastaafu, tena kwa hiari na kabla ya kufikia umri wa kustaafu kwa lazima, anadai ni halali na kwamba kunapata baraka za Katiba kifungu cha 95(1) na 95(3). Kwa ufupi mambo yafuatayo hayana ubishi na yanakubaliwa angalau kupitia barua ya Mhe. Jaji Mkuu:

a) Kwamba alistaafu alipotimia miaka 60 ambao ni umri wa kustaafu kwa hiari na akachukuwa mafao yote ya kustaafu;

b) kwamba baada ya kustaafu akaingia katika mkataba wa miaka miwili wa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa Mkataba;

Sasa tuangalie vifungu vya Katiba ya Zanzibar ya 1984 (Katiba) vinavyoongoza suala la kustaafu kwa Majaji wa Mahkama Kuu:

95(1) Bila ya kuathiri masharti ya kifungu hiki, Jaji wa Mahkama Kuu ataendelea kushika wadhifa wake hadi kufikia umri wa miaka sitini ambapo anaweza kustaafu kwa hiari ama kuendelea hadi kufikia umri wa miaka sitini na tano ambapo atastaafu kwa lazima.

(2) ……………

95(3) Licha ya kuwa Jaji amefikia umri ulioainishwa katika kijifungu cha (1) hapo juu, Jaji wa Mahkama Kuu ataendelea katika wadhifa wake huo hata baada ya kufikia umri huo mpaka pale atapomaliza shughuli zote ambazo zilimfikia yeye kabla ya kutimiza umri huo. [Msisitizo ni wetu]

Ukivisoma vifungu hivyo kwa pamoja utagundua kirahisi kwamba kifungu cha 95(3) kinazuwia utekelezaji wa kifungu 95(1) hata pale ukomo wa umri unapofikia endapo Jaji husika ana majukumu yaliyomfikia kabla ya umri huo na bado hajayamaliza. Hivyo Mhe. Hamid Mahmoud alikuwa na fursa ya Kikatiba ya kuendelea kumalizia shughuli zake mpaka atakapozikamilisha. Hakukuwa na haja ya kustaafu na baadae akachukuwa mkataba kwa kile kinachodaiwa kumalizia shughuli zilizobakia. Neno lililotumika ndani ya Katiba ni “ataendelea” mpaka amalize shughuli zake na akishakamilisha shughuli zake ndio atastaafu. Huwezi kustaafu kwanza na baadae ndio umalizie shughuli zilizobaki. Katiba inazungumzia “ataendelea”.

Tumalizie hoja hii kwa kujibu yale madai kwamba kifungu cha 95(3) hakikuweka ukomo wa Jaji kumalizia shughuli zake. Na hapa ieleweke wazi kwamba shughuli zinazolengwa na Katiba ni shughuli za kuamua kesi. Ifahamike kwamba Jaji anapokaribia umri wa kustaafu anakuwa hachukuwi kesi mpya kwani uzoefu unaonesha kwamba kesi zinachukuwa muda mrefu kumalizika. Lakini kwa kesi ambazo hazijafika mbali basi Jaji anaekaribia kustaafu kesi hizo huzirudisha kwa Jaji Mkuu ili zipangiwe Majaji wengine. Yote hayo hufanywa ili Jaji anapostaafu awe anamalizia tu kuandika hukumu au kusikiliza mashahidi wa mwisho. Na haitegemewi kabisa kwamba baada ya miaka miwili tokea atimize umri wa kustaafu bado Jaji atakuwa “anamalizia” shughuli zake tu!

Hata tukiacha maelezo yote ya hapo juu suala linabaki jee Mhe. Jaji Mkuu alikuwa na kesi gani na ngapi zilizohitaji miaka miwili ya kuzimalizia kwa mujibu wa Katiba? Kwa uzoefu wetu, Mhe. Jaji Mkuu alikuwa akifanya zaidi kazi za utawala tu na hakuwa na kesi yoyote wakati anastaafu kwa hiari.

Lakini na kwa ajili ya kujenga hoja tu iwapo Mhe. Jaji Mkuu alikuwa na kesi na alihitaji kuendelea kuzimalizia, maelezo ya kifungu cha 94(6) ya Katiba yanatupa jawabu:

a) Rais anaweza kumteua mtu yeyote kuwa Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu kwa kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili na Jaji wa mkataba wa kipindi maalum kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi ya Mahkama.

b) Masharti ya kazi, marupurupu na kiinua mgongo cha Jaji wa mkataba wa kipindi maalum yataamuliwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama.
[Msisitizo wote ni wetu].

Ni tafsiri ya wazi kwa mujibu wa vifungu hivyo kwamba Jaji wa mkataba lazima afuate utaratibu ulioelezwa hapo juu. Kwamba uteuzi wake lazima upendekezwe na Tume ya Utumishi ya Mahkama lakini mkataba wake utaamuliwa na Tume. Kwa kifupi hakuna mkataba wowote wa Jaji ambao utakuwa halali bila ya kuamuliwa na Tume ya Utumishi. Hivyo kwa maelezo yake mwenyewe, mkataba wa miaka miwili wa Jaji Mkuu haukufuata utaratibu wa Katiba kwa hivyo ni batili na si mkataba aslan. Na hakuna kabisa mazingira yoyote ya kuhalalisha mkataba wa Jaji kwa kuikiuka Tume ya Utumishi ya Mahkama.

Hoja yetu ya pili katika indhari yetu kwamba Mhe. Jaji Mkuu anachukuwa mamlaka ya Tume ya Utumishi ya Mahkama na kujipa mwenyewe au kutoa maamuzi ambayo Tume haikuyatowa au kufanya uteuzi bila ya kupitia katika Tume hiyo, hili tunaona Mhe. Jaji Mkuu hakulijibu katika barua yake. Tuchukulie kuwa analikubali au tuseme uchunguzi ndio utakaothibitisha ukweli.

Hoja ya mwisho ya Mhe. Jaji Mkuu inahusu nafasi ya Kaimu Jaji Mkuu. Tulitowa tahadhari kwamba uendeshaji kiholela wa mahkama zetu umefikia hadi hata Mahkama ya Rufaa ya Tanzania kutupilia mbali rufaa ambazo zimehukumiwa na Majaji waliopewa kesi na “Kaimu Jaji Mkuu”. Mhe. Jaji Mkuu ametoa ufafanuzi mrefu kuhusu namna wateule wake (isipokuwa Jaji Mshibe) walivyofanya kazi hizo vizuri huko nyuma. Ni ukweli ulio wazi kwamba katika miaka yote 22 ya utawala wake, hata mara moja Mhe. Jaji Mkuu hajamtanabahisha Mhe. Rais wa Zanzibar wa wakati uliopo kwamba Kaimu Jaji Mkuu huteuliwa na Rais, tena huapishwa. Wote waliotajwa na Mhe. Jaji Mkuu kwamba waliwahi kukaimu nafasi yake hakuna aliyewahi kuapishwa. Kwa kifupi mahkama zetu zinaendeshwa kienyeji kupita kiasi na hili ndilo

tunalojaribu kuieleza Serikali yetu tukufu. Wananchi hawana imani ya kupata haki katika mahkama zilizokosa misingi ya utawala bora na utoaji haki usio na woga wala upendeleo.

Tunaomba kuwasilisha.

………………………….
Yahya Khamis Hamad
Rais – ZLS

Nakala:
1. Mhe. Jaji Mkuu, Zanzibar

2. Mhe. Mwanasheria Mkuu, Zanzibar

3. Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, Zanzibar

4. Katibu Mkuu, Wizara ya Utumishi na Utawala Bora

Advertisements

2 responses to “Jaji soma vizuri vifungu hivi:

  1. Aslam aleikum,
    Ndio tunawapongeza kwa kumpa kwali huyo jaji na hiyo serikali yake kwa hao viongozi wa Zanzibar washaifanya nchi kama daladala kilamtu anaendesha. Nilazima nchi iendeshwe kisheria.

  2. hao washazowea kuburura hawana uzoefu wa kuwa challenge ndio ukaona fujo lote hili sawa maloya wetu msimamo huo huo al

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s