Tamko letu ni hili

Mwenyekiti wa MUWAZA, Dk Yussuf Saleh Salim.Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA) ni jumuiya iliyo ughaibuni inayowaunganisha Wazanzibari wa ndani na nje ili kuleta utambulisho wa Wazanzibari na kuleta umoja baina yao kwa kupigania mustakbali wa Zanzibar kama nchi, pamoja na kulinda maslahi yake ya kidola, kitaifa na uhuru.

 

TAMKO KUHUSU KATIBA MPYA

MUWAZA inawapongeza wanaharakati, wadau na wananchi kwa ujumla

waliotoa msukumo wa kuelekea kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania.

Wakati huo huo, inaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuukubali wito huo.

 MUWAZA inaamini kwamba suala la katiba mpya limechelewa sana na inatoa

wito kwa serikali zote kulianzisha kwa haraka sana na kwamba lifanyike kwa

uwazi na ufanisi mkubwa. Aidha, Baraza la Wawakilishi (BLW) la Zanzibar

lichukue hatua za haraka kuwa mbele kwa maslahi ya Zanzibar katika

kupatikana kwa haraka katiba mpya ya Tanzania na hatimaye ya Zanzibar

kabla ya uchaguzi unaofuata.

MUWAZA inawapongeza wote waliotoa mawazo yao katika mustakbali wa

katiba mpya. Aidha, inampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Umoja wa

Kitaifa ya Zanzibar (SUK) kwa ujasiri na maelezo yake yanayotetea kupatikana

kwa katiba mpya.

MUWAZA inawaomba na kuwahimiza Wazanzibari wote kuungana na kuendelea

kutoa mawazo yao kwa nia ya kuipatia Zanzibar na Tanganyika serikali

zitakazoshirikiana katika muungano wenye haki sawa kwa washiriki wake.

Katika hatua ya sasa hivi, MUWAZA inapenda kutoa mapendekezo yafuatayo

kwa maslahi na mustakbali wa Zanzibar katika kuelekea kuipata katiba mpya

ya Tanzania:

1. Mchakato wa kuipata katiba mpya ya Tanzania uzingatie malalamiko,

kasoro (kero) na udhaifu wa muungano uliopo sasa ili katiba hiyo iweze

kuuimarisha muungano huo na kuufanya kuwa wenye uwazi, haki,

maslahi, kueleweka, kukubalika na kupendwa na washirika wake.

Mchakato huu uwe na uwakilishi wa serikali zote, wananchi, asasi za

kiraia, na wadau wengine na usiwe wenye kuendeshwa kwa utashi wa

chama fulani.

2. Katiba mpya ibadilishe mfumo mzima wa muungano na kuufanya kuwa

ni Shirikisho la Tanzania linalojumuisha Zanzibar na Tanganyika. Kwa

maana hiyo kuwepo na serikali tatu zenye marais wake kamili – yaani

Serikali za Zanzibar, Tanganyika, na Shirikisho la Tanzania.

3. Katiba ya Shirikisho la Tanzania itoe heshima sawa kwa Zanzibar na

Tanganyika kama nchi kamili ili kulinda mamlaka na haki za nchi mbili

hizo. Maamuzi yote ya Shirikisho yapitishwe kwa makubaliano ya kura

za kila upande bila ya mchanganyiko. Mamlaka na utendaji wa Shirikisho

uwe na uwakilishi sawa kutoka kila upande wa Shirikisho.

4. SUK pamoja na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) izingatie

jukumu zito iliyopewa na katiba ya Zanzibar la kuhakikisha kwamba

mipaka, mamlaka, rasilimali, heshima na utamaduni wa nchi ya Zanzibar

unalindwa kwa hali zote.

5. Katika kuyalinda mamlaka na haki za Zanzibar, BLW lipitishe kwa haraka

hoja/maazimio juu ya mambo mahsusi ambayo ni muhimu na lazima

kuwemo katika katiba mpya ya Tanzania. Pamoja na mengine, BLW

lizingatie kwa uchache mambo yafuatayo:

a. Zanzibar inaingia katika mchakato wa kupata katiba mpya ya

Tanzania ikiwa ni nchi kamili inayoshirikiana sawa kwa sawa na

Tanganyika katika mjadala huo. Kwa njia yeyote ile, Zanzibar

isiwe yenye kusukumwa katika majadiliano na maamuzi,

b. Serikali ya Zanzibar, rais wake, na bunge lake (BLW) ni sawa

sawa na serikali, marais, na mabunge ya nchi nyengine zilizo huru

duniani,

c. Rais wa Zanzibar pamoja na BLW wawe na mamlaka ya

kuyakataa maamuzi yeyote ya serikali ya Shirikisho la Tanzania

pale inapoona kwamba hayana mustakbali mwema kwa Zanzibar,

d. Kuyapitia upya makubaliano ya muungano na kujadili kila

kipengele na baadae kuyapatia makubaliano hayo mapya ya aina

ya Shirikisho ridhaa ya wananchi wa Zanzibar,

e. Kuhakikisha kwamba hata katika mambo ambayo yanabakia

katika mamlaka ya Shirikisho, Zanzibar inakuwa na kielelezo

chake kinachotambulika, (kwa mfano (a) maaskari/majeshi

waliopo Zanzibar wawe ni Wazanzibari na hawahamishwi kikazi

kwenda upande wa pili wa muungano au kinyume chake, (b)

mtiririko wa wageni wanaongia Zanzibar uwe unadhibitiwa kwa

njia na hati zinazokubalika, n.k.),

f. Shirikisho la Tanzania liwakilishwe katika Umoja wa Mataifa kwa

viti vya Zanzibar na Tanganyika. Kwa maana hiyo, Zanzibar

irejeshe kiti chake katika umoja huo na hivyo hivyo kwa

Tanganyika,

g. Zanzibar itambulike kama nchi kamili katika mikataba na

makubaliano yote ya kimataifa. Aidha, Rais wa Zanzibar awe ndie

mwenye mamlaka ya juu kwa Zanzibar ndani ya Shirikisho na

kimataifa,

h. Mambo yote yanayohusu uhuru wa kiuchumi na kisiasa yabakie

ndani ya mamlaka ya Zanzibar. Aidha, mamlaka ya kuteua

wagombea uongozi na kuchagua yawe ni ya Wazanzibari

wenyewe. Kwa njia yeyote ile, masuala haya yasiingiliwe na

upande wa pili wa Shirikisho,

i. Urais wa Shirikisho uwe wa mtindo wa kupokezana baina ya

marais wa Zanzibar na Tanganyika katika kila muhula mmoja wa

uongozi. Kwa mfano, katika kipindi cha uongozi cha miaka 5,

miaka miwili na nusu iwe kwa Zanzibar na mengine miwili na nusu

iwe kwa Tanganyika,

j. Zanzibar ipate haki zake zote kutoka Benki Kuu ya Tanzania

(BOT) kulingana na mtaji wake wa uanzishwaji wa benki hiyo.

Aidha, Zanzibar iwe na kiwango cha ushiriki katika benki hiyo

kinachojuilikana kwa wastani wa asilimia kulingana na mtaji wake

wa uanzishi,

k. Mchakato na makubaliano ya katiba mpya ya Shirikisho la

Tanzania yafanyike kwa uwazi, haki, na ufanisi mkubwa na

kukamilika haraka iwezekanavyo kabla ya mwezi Juni 2012.

6. Katika kipindi chote cha mpito wa kuipata katiba mpya, ihakikishwe na

ionekane kwamba kanuni ya kupitisha sheria bungeni inayotaka thuluthi

mbili ya kura za wabunge wa Zanzibar inaheshimiwa ipasavyo. Vile vile,

mamlaka ya BLW kutoka ndani ya katiba ya Zanzibar juu ya kuidhinisha

au kukataa mabadiliko yanayohusu muungano inaheshimiwa.

7. Katiba mpya iwaelekeze marais wote kujiengua kutoka katika vyama

kabla ya kuapishwa ili wawe huru na misukumo ya vyama vyao na

wawajibike kwa mabunge yao. Kwa kufanya hivyo wawe na mrengo wa

ki-nchi badala ya ki-chama na waepukane na ukiritimba wa siasa za

chama kimoja.

8. Katiba mpya iondoe ulazima wa vyama kuwa vya kitaifa ili itoe uhuru wa

kuundwa vyama vya siasa vya aidha Zanzibar, Tanganyika, au Tanzania.

Sambamba na hilo, katiba mpya itoe uhuru wa kuwepo wagombea

binafsi wa kujitegemea.

9. BLW lihakikishe kwamba makubaliano ya mwisho ya katiba yanapitishwa

kwa kura huru za maoni kutoka kwa wananchi. Kura hizo mbili ziwaulize

Wazanzibari masuala ya (i) kuukubali muungano au kuukataa, na (ii)

kuikubali katiba mpya au kuikataa.

10.Mara baada ya mafanikio ya kupatikana kwa katiba mpya ya Shirikisho,

na kupatikana pia ridhaa ya Wazanzibari juu ya katiba ya Shirikisho

jipya, SUK kupitia BLW iipitie katiba ya Zanzibar na kuiandika upya ili

iendane na wakati. Kwa kufanya hivyo, SUK na BLW izingatie pamoja na

mengine mambo yafuatayo kwa nchi ya Zanzibar:

a. Katiba ya Zanzibar iende sambamba na demokrasia ya vyama

vyingi na iwe yenye mwelekeo wa mabadiliko ya kuijenga

Zanzibar mpya yenye nguvu, maadili, utamaduni, amani na haki

sawa kwa wananchi wake,

b. Kutoa njia na fursa ya kusameheana na kusahau maonevu na

makovu yaliyopita katika historia kwa kuijenga Zanzibar mpya

yenye nguvu na upendo,

c. Kuzieleza, kuzitekeleza, kuzilinda na kuziheshimu haki za raia wa

Zanzibar bila ya kujali tofauti zao za ama itikadi, dini, rangi, asili

au jinsia,

d. Kutoa maelekezo ya kupata mahkama huru na tume huru ya

uchaguzi itakayowajibika katika mahkama iliyo huru,

e. Kuweka sheria imara ya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na

uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari za ndani na nje kwa

wananchi wake,

f. Kuweka bayana haki ya Wazanzibari kushika nyadhifa za nchi yao

kulingana na ujuzi na uwezo wao bila ya upendeleo,

g. Kubainisha na kusimamia kisheria kwamba uongozi na utendaji ni

dhamana ya utumishi wa umma iambatanayo na uadilifu na

uwajibikaji, na kwamba dhamana hiyo sio haki miliki ya

mwananchi au kikundi fulani,

h. Kuzidisha mshajiisho wa kuyapa nguvu zaidi maridhiano na

kuboresha uendeshaji wa SUK pale panapostahiki,

i. Kuweka sera maalum za Zanzibar ambazo zitalindwa na kila

mwananchi au kiongozi bila ya kujali itikadi za ki-chama,

j. Kuondoa mwanya wa rais kujilimbikizia madaraka yanayofanana

na udikteta,

k. Kuziheshimu na kuziimarisha asasi za kiraia zisizo za serikali, na

kuzishirikisha katika uendeshaji wa nchi pale panapostahiki,

l. Kuijengea Zanzibar njia za uchumi na biashara huru na kuzilinda

kisheria rasilimali za nchi kama vile mafuta, bahari, n.k. Pia, kuipa

Zanzibar uhuru wa kutumia bandari zake na viwanja vyake vya

ndege katika kuuhuisha uchumi wake,

11.BLW lihakikishe kwamba katiba mpya ya Tanzania inajadiliwa na

kukamilika ifikapo mwezi wa Juni 2012. Endapo muda huo

hautazingatiwa, au maagizo ya BLW hayatopewa kipau mbele, au

mustakbali mwema kwa Zanzibar hautaonekena katika mchakato mzima

wa katiba mpya ya Tanzania, BLW lichukue hatua ya kuiandika upya

katiba ya Zanzibar na kuyaingiza angalau mambo yaliyomo katika

mapendekezo haya kabla ya uchaguzi unaofuata.

MUWAZA inaihimiza serikali adhiimu ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK)

pamoja na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa kisiasa

hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya ya Tanzania.

Aidha, MUWAZA inaipa hadhari SUK na BLW kukwepa mtego wowote

utakaotokea wakati mjadala wa katiba mpya utakaposhika kasi, kama vile

kutiwa katika mazonge au mgogoro utakaowagawa Wazanzibar kwa njia

yeyote ile.

MUWAZA inaziomba asasi za kiraia kuwaelimisha Wazanzibari ili waungane kwa

kauli moja katika kutetea haki za nchi yao. Elimu hiyo ni muhimu ili kutoa

nafasi nzuri kwa Zanzibar kujikita katika kulishughulikia ipasavyo suala

muhimu la katiba mpya ya Tanzania.

MUWAZA inaamini kwamba mjadala wa kuipata katiba mpya ya Tanzania ni

fursa muhimu katika kuuzaa upya na kuudumisha muungano wa aina ya

Shirikisho na kuupatia ridhaa ya washirika wake.

Hivyo basi, ni wajibu wa kila Mzanzibari mwenye kuipenda nchi yake kujidhatiti

katika kuilinda nchi yake kwa sababu pindipo Wazanzibari tutaipoteza fursa hii

adhiimu, tutakuwa hatuna wa kumlaumu wala njia ya kujinasua kwani

muungano huu tunaoulalamikia siku zote utaonekana kama kwamba

umehalalishwa na wananchi wenyewe.

MUWAZA inaamini kwamba Zanzibar inahitaji kujiimarisha ndani ya muungano

wa Tanzania sambamba na kujiimarisha kimataifa katika mamlaka na haki

zake za kitaifa. Mwanzo wa safari hiyo ni kuirudisha serikali ya Tanganyika

ndani ya muungano huo.

Kama ilivyo kawaida yake, MUWAZA itaendelea kutoa maoni yake kuhusu

mustakbali wa kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania kadri mchakato wake

utakavyoendelea.

Kwa niaba ya MUWAZA, imetolewa na:

Dr. Yussuf Saleh Salim

Mwenyekiti wa MUWAZA

Copenhagen, Danmark

Februari 5, 2011

Advertisements

One response to “Tamko letu ni hili

  1. wallah nimefurhai kweli kuna nakala hii nimeisoma na kuifahamu japo kuwa sina upeo zaidi wa kisiasa kwani imi ni mwanafunzi wa mambo ya uhandisi ama engineering lakini kama kawaida ya wa Zanzibar siasa imo ndani ya damu yetu na inatuuma nchi yetu kuliko yoyote. Inatupa moyo kuona motion kama hizi zikifnayiwa kazi na wahusika wa mambo ya siasa kwani it’s about time kusimama na kudai haki zetu ambazo tumefungwa mdomo kwa miaka mingi kabisa na majirani zetu kuzigombea viongozi wetu wamefungwa na siasa za vyama na kusahau kabisa kuhusu nchi nimeone jinsi gnai muandishi ali point out kuhusu rais kujitoa katika chama anapoingia madarkani hilo ni wazo zuri na naamini litaepusha mchezo wa kuogopa wale waliojuu kwenye chama .
    Ila kama mimi kijana wa ki Zanzibar ningeomba kuongezi japo kitu kidogo sisi kama vijana tunaosoma nje ya nchi tunakuwa tunamigongano na wenzetu wa bara pale tunaposema sisi ni wazanzibar wao huwa inawauma nainafikia wakati tunafikishana sipo kiso kukana kuwa sie ni wazanzibar na tuna haki kama nchi japokuwa tuko katika kauli sahihi ila wenzetu ama ndugu zetu wanatuzidi kauli wanaposema kama kweli nyinyi ni nchi iko wapi “passport” yenu hii kauli yani inaweza kukuvunja kabisa ukiwa katika mabishano yakihoja mana tunakuwa hatuna hoja ya kujibu kwani kwa kweli hatuna na ndo mana unakuta vijana wenzetu ni mahodari wa michezo kama mpira wa miguu unakuta lakini hatuna timu inotuwakilisha bali tunabaki kuanglaia wenzetu wa bara waanpata faraj ya kuende sehemu tofauti na naamini tukiangaliwa kati ya vijana wetu na wao hawatufiki katika kiwango kama hivo, tunawaogeleaji mahiri sana kwani sisi ni watoo wa visiwani ila unakuta mahsindano ya naman hayo yakifanywa wenzetu hawapati nafasi kwani bara waantunyima kisa wao wanasema wantuwakilisha hii kwlei inatuuma ningeomba jambo hili liangaliwe kwani kama hatuna passport za kwetu iyo serikali ya Zanzibar itakuwa ni sawa sawa na kazi ya bure mana we will still be under the shadows of Tanzania na Interanationaly hatutotambulikana bali tutabakia kushangaza watu kwa kutaja jina linalovutiwa kisauti kwa mgeni ila halitambuwi kwa kuwa hajawahi kulisikia kama nchi.
    Sitaki kuongea mengi natumai utanifikiria mchango wangu kwani hilo si langu peke yangu tu bali ni haki yetu sote wa Zanzibar kuwa na kitambulisha kinotambulikana Duniani .
    Naomba radhi kwa kuchanganya lugha mbili wakati moja ila nina upungufu wa kutumia maneno ya kiswahili katika baadhi ya sehemu

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s