Wazanzibari wasibezwe

Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia akiongea katika mkutano wa Chama Cha Wananchi (CUF) Kibanda Maiti Mjini Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka watanzania kutowabeza wazanzibari kutokana na maamuzi yao ya kubadilisha katiba na kuchagua mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa kwani maamuzi hayo ndio yaliosababisha mageuzi ya kuwepo mchakato wa majadiliano ya katiba ya Tanzania yanayoendelea hivi sasa nchini.

MWENYEKITI wa Chama Cha NCCR-MAGEUZI Taifa, James Mbatia amesema mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar ndio yaliochochea mabadiliko ya katiba ya Tanzania.

Akihutubia mkutano wa hadhara ulifanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Mjini Zanzibar, Mbatia alisema mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ndio yalochochea vuguvugu la wananchi kudai katiba mpya Tanzania kwa kuwa kwa hali yoyote katiba ya Zanzibar imeiathiri katika ya Tanzania.

Alisema mabadiliko ya katiba yaliofanywa Zanzibar na kuundwa Serikali ya umoja wa kitaifa yameleta changamoto kubwa kwa watanzania nao kudai katiba yao ibadilishwe kwa kuwa huwezi kubadilisha katiba ya Zanzibar bila ya kubadilisha katiba ya Tanzania.

“Haya mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar ndio yalioleta vuguvugu kwa watanzania kudai katiba mpya kwa sababu ndugu zangu katiba ya Zanzibar inaigusa sana katiba ya Tanzania kwa hivyo …lakini sasa unasikia sisi ndio tulioanzisha ehhh sisi hakuna haja ya kujua aliyeanzisha mchakato huu wa katiba watanzania hawahitaji kujua nani ni muazilishi wanataka mabadiliko ya katiba mpya” alisema Mbatia.

Alisema Maalim Seif na rais mstaafu, Amani Karume wamefanya jambo la maana sana kukubaliana kutokumwagika damu ya wazanzibari hivyo kuna kila sababu ya kuwapongeza viongozi hao pamoja na wananchi waliokubali kura ya ndio ya maoni na kuchagua mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Mbatia historia ya Zanzibar ni kubwa ambapo aligusia suala la ushindi wa Maalim Seif jambo ambalo liligusa hisia za wengi na alisema mwaka 2001 Zanzibar ilimwagika damu lakini sasa hivi amani imerudi kutokana na mfumo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa na kuwataka wale wenye kuibeza Zanzibar kupuuzwa.

Mbatia alisema maadiliko hayo ndiyo yameigusa katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na yamechochea kwa kiasi kikubwa kutaka kuandikwa kwa katiba mpya ya Tanzania.

Amesema wazanzibari wasishughulikie maneno ya mitaani inayosemwa kwamba chama cha CUF ni CCM B bali wanaosema hivyo ndio CCM B hivyo wananchi waendeleze mshikamano na umoja uliopo hivi sasa ili kuleta demokrasia ya kweli.

Kwa pande wake Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF) Professa Ibrahim Haroun Lipumba amesema bandari ya Zanzibar inaweza ikatumiwa  na nchi za jirani itakapoanzishwa bandari huru visiwani hapa.

Alisema Zanzibar shughuli zake ni biashara kwa kuwa ni nchi ya visiwa na hakuna sababu isijikite katika bandari huru kwa vile nchi za jirani kama Burundi, Zambia na  Uganda hazina bandari ambapo zingeweza kutumia moja kwa moja bandari ya Zanzibar.

Kauli ya Professa Lipumba inakuja wakati tayari makamu wa kwanza wa rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameshafanya mazungumzo na washirika wa maendeleo juu ya suala la ujenzi wa bandari kuu hapa Zanzibar alipokuwa ziarani huko Sharajah.

Profesa Lipumba alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa imejipanga vizuri kushughulikia masuala ya Zanzibar ni vyema kuwe na ustahamilivu kwani mipango haiwezi kutekelezwa kwa mara moja.

Alisema serikali ya umoja wa kitaifa inaweza ikaongeza mipango yake kwani imetoa fursa kwa viongozi kuweza kutumikia wananchi walio chini yao na hivyo kuwaomba wananchi kuiunga mkono serikali hiyo ili iweze kuwatumikia.

“Nina imani viongozi wa Serikali ya umoja wa kitaifa wakiungwa mkono kwa ushirikiano wa wananchi wataweza kuleta mabadiliko makubwa jambo muhimu ni kuwaunga mkono “alisema Lipumba. Na kuongeza kwamba fursa hizo zinaweza zikatumiwa ili kuondosha matatizo ya wazanzibari

Aidha alisema serikali  inahitaji muda zaidi wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi  katika kipindi cha miezi minne bado ni kidogo kupima uwezo wa serikali wa kukabiliana na gharama za maisha na kuwataka wananchi kuvuta subra.

Samba na hilo Profesa Lipumba aliwataka  wananchi wasichoke kuihoji Serikali yao juu ya azma yake ya kuleta maisha bora kwa kila Mzanzibari kwani kuna fursa nyingi za kuendeleza uchumi ikiwemo shughuli za bandari, kilimo na sekta ya biashara na utalii.

Profesa Lipumba alisema anaimani Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar inaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kutatua tatizo la ajira kwa vijana, hivyo amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s