Tusichague kiongozi mla rushwa

Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui aakifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Baraza la wasafirishaji wa mizigo Zanzibar kwenye hoteli ya Zanzibar Ocean View.

HOTUBA YA MGENI RASMI, MHE. NASSOR AHMED MAZRUI, WAZIRI WA BIASHARA, VIWANDA NA MASOKO KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA KWANZA WA BARAZA LA WASAFIRISHAJI MIZIGO, TAREHE 24 MARCH 2011 OCEAN VIEW HOTEL, KILIMANI ZANZIBAR

 

Mhe. Rais wa Jumuiya wa Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima;

Katibu Mkuu wa ISCOS;

Waheshimiwa Viongozi;

Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya Baraza la Wasafirishaji Mizigo;

Wanachama wa Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

Awali ya yote, naomba kumshukuru Mwenyeezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia kuamka salama na wenye afya na kutuwezesha kuhudhuria katika hafla hii ya leo.

Aidha, naomba pia  kuwashukuru waandaaji wa shughuli hii, Kamati ya Mpito ya Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar wakishirikiana kwa karibu na ISCOS (Intergovernmental Standing Committee on Shipping) kwa kuamua kunialika mimi kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwanzo wa Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar; Mkutano ambao utafuatwa na Uchaguzi wa Viongozi wapya wa Baraza hili. Kwangu hii ni heshma kubwa na nanaithamini sana. Ninamuomba Mwenyeezi Muumba ajaalie viongozi mtakaowachagua hii leo wawe chachu ya kuifungulia Zanzibar milango ya biashara na kuirudishia Zanzibar hadhi yake kama Kitovu cha Biashara cha Afrika ya Mashariki.

Ndugu Wanachama:

Mabibi na Mabwana:

Nimeelezwa kwamba ISCOS wamekuwa ndio kichocheo cha kuanzishwa kwa Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar. Hivyo, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi na kwa niaba ya Wazanzibari hasa wafanya biashara, naomba nichukuwe fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa, Katibu Mkuu wa ISCOS, Bwana Archie Chamungwana Mgondah pamoja na timu yake yote kutoka Mombasa, Kenya. Bila ya mchango wao muhimu leo tusingefika katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu wala Uchaguzi wa Viongozi wa Baraza hili.

ISCOS ni Taasisi ya Kikanda (Regional Organisation) inayojihusisha katika kuendeleza biashara katika nchi za Afrika Mashariki. Na kwa kutumia utaalam ilionao, ISCOS imeziwezesha nchi wanachama za Kenya, Uganda, Tanzania Bara na Zambia kunusuru mamilioni ya fedha zinazotokana na punguzo la gharama katika usafirishaji wa mizigo. ISCOS imezisaidia nchi wanachama kupata bei nzuri kutoka kwa wenye meli za mizigo na meli za mafuta. Punguzo hilo lisingepatikana kama kila mfanya biashara anakwenda kupatana bei kibinafsi. Faida inayopatikana kutokana na taaluma na umoja unaoletwa na ISCOS ni kubwa hasa kwa nchi zetu changa zenye uchumi tegemezi.

Ndugu Wanachama:

ISCOS inafanya kazi kwa kushirikiana na mabaraza ya wasafirishaji mizigo ya nchi wanachama; ni wazi kwamba walihitaji kuundwa kwa Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar (ZSC) ili waweze kuiingiza Zanzibar katika mtandao wake wenye maslahi na tija kwa wafanya biashara. Nimeelezwa kwamba ZSC imesajiliwa rasmi kama Kampuni isiyo na hisa tarehe 27 Mei 2010. Baraza hili linategemewa kuwaunganisha pamoja wasafirishaji mizigo wa Zanzibar katika kupata bei nzuri kwa kusafirisha mizigo kwa njia ya bahari. 

Ndugu Wanachama:

Mabibi na Mabwana:

Kuanzishwa kwa mabaraza ya wasafirishaji mizigo duniani kumekuja ili kupata sauti ya pamoja katika kukabiliana na wenye meli ambao bila ya kutafutiwa njia ya kuwazuwia, watapandisha bei kiholela kila wakati. Ni kutokana na sababu hizo ndio maana nataka nichukuwe fursa hii kuwahamasisha wafanya biashara wa Zanzibar kujiunga na Baraza la Wasafirishaji Mizigo.

Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar ambalo lilizinduliwa rasmi na Mhe. Hamad Masoud, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano tarehe 24 Novemba 2010, lina malengo kadhaa yaliyoorodheshwa katika Katiba yake; baadhi ya malengo hayo ni:

  1. kuwaunganisha wasafirishaji mizigo wa Zanzibar pamoja na kupata jukwaa la kukutana na kupanga masuala yenye maslahi kwao katika shughuli ya kuagiza na kusafirisha mizigo;
  2. Kulinda maslahi ya wasafirishaji mizigo wa Zanzibar katika mazungumzo yoyote baina yao na upande wa pili;
  3. Kuzileta katika meza moja sekta ya umma na sekta binafsi ambapo maslahi ya pande zote mbili yatasimamiwa ipasavyo;
  4. Kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kusaidia katika majadiliano baina ya wasafirishaji mizigo na wenye meli ili kupata bei muwafaka kwa wafanya biashara wa Zanzibar;
  5. Kubuni na kuanzisha taratibu za kuweka sheria nzuri za kusimamia masuala ya usafirishaji na ushughulikiaji mizigo kwa maslahi ya wadau wote;
  6. Kushirikiana na mabaraza mengine ya kusafirisha mizigo Afrika Mashariki na duniani kote kwa ajili ya kujifunza kutokana na uzoefu wao.

 

Ndugu Wanachama:

Haya ni baadhi tu ya malengo ya Baraza hili na ninaona kuna kila sababu ya wadau wa sekta hii kujiunga na Baraza hili haraka iwezekanavyo ili Baraza liweze kusimama kwa miguu yake wenyewe. Nimefurahishwa sana kupata habari kwamba Wazanzibari wameitikia vizuri wito wa kujiunga na Baraza hili la Wasafirishaji Mizigo. Kampeni ya kutafuta wanachama iliendeshwa kwa pamoja baina ya Kamati ya Mpito ya ZSC na Jumuiya ya Wafanya Biashara, Wenye Viwanda na Wakulima chini ya usimamizi na ufadhili wa ISCOS.

Napenda nikushukuruni kwa dhati kabisa wanachama nyote mlioweza kuamua kujiunga na Baraza hili na ninaamini kabisa mmefanya uamuzi wa busara na kamwe hamtajuta. Aidha ninaamini kwa dhati kwamba miongoni mwenu wapo watu madhubuti ambao mkiwapa nafasi ya kuwatumikia watafanya hivyo kwa ufanisi mkubwa.

Ndugu Wanachama:

Kabla ya kumaliza hotuba yangu, naomba kukuwaseni kwamba mchaguwe viongozi waadilifu na wachapa kazi. Hii ndio njia pekee ya kuthamini juhudi kubwa iliofanywa na Kamati ya Mpito pamoja na ISCOS kuweza kuwafikisha hapa tulipo. Kwa sababu kazi yenyewe ni ngeni, si sahihi kutafuta kiongozi mzee kwa umri au utumishi katika jamii kwani hata vijana na wale wasio na uzoefu wanao uwezo wa kuongoza pindipo watawezeshwa. Mimi naamini kabisa juhudi za pamoja za wanachama wote – vijana na wazee ndizo zitakazolifanya Baraza la Wasafirishaji Mizigo la Zanzibar kuwa ni chombo chenye kupata imani ya wanachama wake pamoja na Serikali ya Mapinduzi. 

Ndugu Wanachama:

Nimeambiwa kwamba Viongozi mtakaochagua leo kama memba wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza ni 7 kwa mujibu wa Katiba ya Baraza. Viongozi hao wanaochaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 13 ni:

  1. Mwenyekiti
  2. Makamo Mwenyekiti
  3. Mweka Hazina
  4. Viongozi wengine 4 kutoka miongoni mwa wanachama wa ZSC

 

Napenda kufanya ushawishi wa kukutakeni mgombee nafasi hizi. Kila mwanachama ana haki na wajibu wa kuhakikisha mnapata viongozi madhubuti. Kazi iliopo mbele yenu ni kubwa na inahitaji viongozi makini.

Ndugu wanachama, Mabibi na Mabwana pamoja na wageni waalikwa, baada ya kueleza hayo machache naona fahari sasa kutamka rasmi kwamba MKUTANO MKUU WA KWANZA WA BARAZA LA WASAFIRISHAJI MIZIGO LA ZANZIBAR UMEFUNGULIWA.

 

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s