Bora mtusamehe hatuna pesa-SMZ

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed amesema wananchi wawasaidie wenziwao waliopatwa na maafa kwa kuwa serikali haina uwezo kwa sasa

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeshindwa kuwalipa fidia watu waliopatwa na maafa ya upepo mkali uliovuma hivi karibuni kwa sababu idara ya maafa haina fedha za za kutosha za kulipa familia hizo.

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali yalioulizwa ndani ya ukumbi wa baraza la wawakilishi baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hijja Hassan Hijja aliyetaka kujuwa watu waliopata maafa ya upepo mkali uliotokea mwezi febuari mwaka huu kama wamelipwa fidia na kiasi gani walicholipwa pamoja na familia ngapi zilizofaidika na malipo hayo.

Aboud alisema ni kweli maafa yalitokea na kuathiri baadhi ya familia lakini kwa bahati mbaya serikali haina fedha za kuwalipa wananchi waliofikwa na maafa hayo na kuwataka wananchi majirani, ndugu na jamaa kuzisaidia familia zilizokumbwa na maafa hayo.

Alitaja hasara ya shilingi milioni 147.4 imepatikana kwa wananchi mbali mbali kupata matatizo ya upepo huo ambao uliathiri pia majengo ya jeshi la kujenga uchumi (JKU) Bambi.
   
Idara ya maafa ambayo miongoni mwa majukumu yake kukabiliana na majanga mbali mbali na kuweza kuwasaidia wananchi lakini hadi sasa haina fedha za kulipa fidia wananchi waliopata matatizo kama hayo lakini kwa kuwa serikali haina fedha kwa sasa wananchi wasitarajie kulipwa chochote ktoka serikalini.

Aboud alisema katika mkoa wa mjini magharibi Unguja hasara iliyopatikana kwa wananchi kufuatia upepo huo ni shilingi milioni 40.4, na katika mkoa wa kaskazini Unguja ni shingili milioni 74.5 wakati mkoa wa mjini ni shilingi milioni 32.5 ambazo zote hizo hazitalipwa kutokana na serikali kutokuwa na fedha.

Aidha alikiri kwamba upepo mkali uliovuma tarehe 9-2-2011 katika kisiwa cha Unguja maeneo ya mjini magharibi kama ulisababisha maafa makubwa ikiwemo nyumba kuezuliwa mabati na matatizo mengine yaliotokea siku ya upepo huo.

Alisema wizara yake haina uwezo wa kuwalipa waliofikwa na maafa ingawa inatambua maafa hayo yaliotokea mnamo febuari mwaka huu wakati wa mvua na upepo mkali uliovuma hapa Zanzibar.

Alisema janga ni kitendo chenye uwezo wa kusababisha matokeo yanayoleta madhara kwa maisha ya binadamu na mali zao hivyo wananchi kwa kushirikiana na serikali yao  hawana budi kusaidiana katika suala hilo.

Aboud alisema maaafa ni tukio kubwa linalotokea na jamii kushindwa kuendelea na utaratibu mzima wa kazi zao tukio mabalo husababisha vifo mateso au upotevu wa mali na uharuibifu wa miundo mbinu na mazingira.

Alisema uharinbifu huo unazidi uwezo wa jamii katika kukabiliana na maafa hayo kwa hivyo tukio la upepo uliotokea February 9 mwaka huu na kuleta hasara kwa jamii ilikuwa ni janga na serikali kwa kushirikiana na wananchi  ilichukua hatua mbali mbali  kukabilianan na hali hiyo.

Waziri huyo akijibu suala la msingi aliloulizwa na Hija Hassan Hija wa Jimbo la Kiwani aliyetaka kujua ni kwa nini Mamlaka ya hali ya hewa haikutoa taarifa tahadhari ya ukubwa wa upepo huo katika siku ya tukio na kutaka ajulishwe upepo huo ulivuma kwa ukumbwa wa kiasi gani.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba kwa mujibu wa hali ya hewa hapa Zanzibar zilitangaza kwamba upepo huo ulivuma kutoka muelekeo gani na ulikuwa na ukubwa wa kiasi gani, Aboud alisema serikali inachuka tahadhari sana katia kukabiliana na maafa kama hayo.

Mwakilishi huyo alitaka kujua ni nyumba ngapi za wananchi zilizopatwa na maafa kwa kuwa muda huo madereva walikimbia kwa mwendo wa kasi na kusababisha ajali huku akitoa mfano wa gari ya Toyota Prado lililowagonga na kusababisha vifo vya watoto wawili katika maeneo ya Welezo mjini Unguja lakini hakuna taarifa za kusaidiwa familia hiyo na kuuliza ni kiasi gani kilichotolewa kwa ajili ya familia hiyo.

Akijibu swali la kutoa taarifa za hali ya hewa Aboud alisema mamlaka ya hali ya hewa kanda ya Zanzibar ina utaratibu kupitia vipindi vyake vya televisheni Zanzibar (TVZ) Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) kwa kutoa utabiri wa hali ya hewa nchini kila siku.

Kuhusu suali la utabiri wa hali ya hewa alisema kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini upepo huo ulivuma kutoka kaskazini hadi kaskazaini Mashariki kwa kasi ya kilometa kumi hadi ishirini kwa saa na baadae uliongezeka na kufikia kilomita thalathini na tano kwa saa.

Hata hivyo siku ya February 8 indhari ya kutokea mvua itayoambatana na ngurumo za radi ilitolewa na kutolewa tahadhari ya muelekeo ya ongezeko la kazi ya upepo kwa visiwa vyote vya Unguja na Pemba hadi February 19 ilitolewa pia mamlaka iliwataka watumiaji wa vyombo vya baharini kuchukua tahadhari katika kipindi chote hicho.

Kutokana na taarifa hiyo kamati za maafa Wilaya jumla nyumba 216 ndizo zilizoathirika kutokana na janga hilo kati ya hizo nyumba 206 ni za watu binafsi na majengo 10 ni mali ya JKU katika kambi ya Bambi.

Ni kawaida kuwa yanapotokea majanga mbali mbali watu hupatwa na mishtuko kuhusu ajali iliyotokea welezo, taasisi zilizohusika na ajali ya barabarani zilichukua hatua kwa taartibu zao, hata hivyo taasisi ya maafa inaendelea kufuatilia suala hilo ili kuona haki ikitendeka.

“Naomba kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari katika matumizi ya barabarara hasa katika nyakati za mvua zinazoambatana na upepo mkali” alisema Aboud.

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUFUTA KESI MAHAKAMANI

 

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wafanyabiashara wa eneo la Darajani waliofungua kesi yao mahakamani kuindosha kwa kuwa serikali imeamua kuchukua eneo lake kwa ajili ya kutenenezea bustani na maegesho ya magari.

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwinyihaji Makame Mwadini ameyasema hayo wakati akijibu maswali katika ukumbi wa baraza la wawakilishi ambapo alisema wafanyabiashara wakaifute kesi kwa sababu uamuzi wa kuondolewa ni uamuzi wa serikali kuu.

“Nawasihi wafanyabiashara waliokwenda mahakamani waiondoke hiyo kesi yao na wataona matunda yake yake hapo Darajani, kwa sababu eneo la Darajani serikali iliwapa wafanyabiashara na sasa serikali hiyo hiyo inalitaka eneo lake” alisema waziri huyo.

Kauli hiyo alitoa katika ukumbi wa baraza la wawakilishi wakati akijibu suala la msingi aliloulizwa na Ali Salum Haji Jimbo la Kwahani aliyetaka kujua kuna sababu ipi inayokwamisha kuondolewa kwa makontena ya Darajani ili kuweza kuliacha eneo hilo kuwa wazi na kufanyiwa shughuli nyengine za serikali.

Waziri Makame alifahamisha kuwa sababu inayokwamisha kuyaondoa makontena hayo ni suala la baadhi ya wenye makontena hayo kuweka pingamizi Mahakamani ambapo kwa mara ya mwisho kesi hiyo ilisikilizwa Machi 13 mwaka huu na inatarajiwa kusikilizwa tena Machi 29 mwaka huu .

“Hakuna mpango mpya wa serikali kwa sasa zaidi ya kuendeleza ule uliopo wa kulifanya eneo hilo kuwa wazi kwa ajili ya Bustani na maegesho ya magari (Green belt area) kwa mujibu wa mpango wa hifadhi ya mji Mkongwe”alisema waziri Makame.

Alisema eneo hilo limewekwa kwa ajili ya bustani na maegesho ya magari na ni mpango mpya wa serikali katika eneo hilo kwa lengo la kuimaisha mji wake.

Waziri makame alisema eneo la darajani limekuwa likitumiwa vibaya na wafanya biashara na wasio wafanya biashara kwa vitendo mbali mbali vya kihalifu kama vile uuzaji wa mihadarati,wizi wa mifukoni,utapeli,udhalilshaji wa kijinsia,uzwaji wa bidhaa zilizokwisha muda na usumbufu kwa wanafunzi wa skuli ya Darajani na Vikokotono.

Alidha alisema lengo la Serikali katika eneo lile ni kulifanyia kuwa ukanda wa kijani (Green Belt) na sio biashara kama ilivyo hivi sasa.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba mwaka 2007 Serikali iliwaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo na kuwapeleka Saateni, lakini wafanyabiashara hao walirudi kwa kisingizio kuwa watakwenda saateni endapo makontena ya Darajani yataiondolewa.

Aidha waziri huyo alisema Serikali haikupenda kuchukua nguvu kwa kuwaondosha wafanyabiashara lakini baadhi yao wamefahamu na wameshaondoka katika eneo hilo.

Alisema kwa kuwa eneo hilo wafayabiashara waliruhusiwa na serikali si mtu binafsi sasa wakati umefika serikali inataka kupaendeleza hivyo inawata wafanyabiashara hao kuondoka katika eneo hilo la biashara maarufu darajani.

FEDHA ZETU MZIREJESHE MKIPATA AJIRA-SMZ

WANAFUNZI wanaosomeshwa na serikali watakaopata fedha za mikopo watalazimika kuzirejesha fedha hizo wakati watakapomaliza masomo yao na kupata ajira imeelezwa.

Hayo yamo katika mswaada wa sheria wa kufuta sheria ya mfuko wa elimu ya juu namba 6 ya mwaka 2011 na kuweka sheria mpya itakayojulikana kama sheria ya kuanzisha bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar iliyowasilishwa katika kika cha baraza la wawakilishi hapo jana.

“Sheria mpya itakayoanzishwa inakusuda kuweka utaratibu wa wazi kuwataka wanaofaidika na mikopo hiyo kurejesha fedha hizo wakati wanaomaliza masomo na kupata ajira lengo la kufanya hivyo ni kujenga uwezo mfuko wa bodi ya mikopo kuwafikia wengine wenye sifa kwa ajili ya kuwasaidia katika maendeleo ya upatikanaji wa elimu ya juu nchini sheria ya mfuko wa elimu ya juu iliyopo imeonekana kuwa na mapungufu juu ya suala hilo” umesema mswaada huo.

Mswaada huo umezingatia mapendekezo ya maeneo muhimu ikiwa pamoja na kuweka wazi majukumu ya muajiri na mdhamini pamoja na na adhabu kwa mtu yeyote atakayeshindwa kuandaa utaratibu wa malipo na mkopaji yenye lengo la kuhakikisha kuwa fursa ya upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu na urejeshwaji wake vijana wetu inaleta ufanisi katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Akiwasilisha hutuba ya kamati ya maendeleo ya wanawake n ustawi wa jamii kuhusu mswaada wa sheria ya uanzishwaji wa bodi ya mikopo na elimu ya juu Zanzibar, Amina Iddi Mabrouk alisema kamati yake inasisitiza kuwa sheria mpya itakayopitishwa ni vyema ihakikishe kuwa inadhibiti vyanzio wa upatikanaji wa mapato ya bodi ya mikopo ili kuwepo na uhakika kwa maendeleo ya baadae ya mfuko wa mikopo.

Alisema suala la upatikanaji wa elimu ni muhimu katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa watu wake kwa kuzingatia hilo hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa fursa mbali mbali za Elimu kwa vijana wake wenye sifa wanaomaliza elimu ya Sekondari ya juu kwa kuwapatia Mikopo ya fedha za kulipia ada na huduma nyengine muhimu za kuwawezesha kusoma.

Alisema tokea kuanzishwa sheria ya Mfuko huo idadi ya vijana wenye sifa ya kujiunga katika elimu ya juu imekuwa ikiongezeka hali ambayo pamoja na mambo mengine kamati yetu inaipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwa na chombo cha kisheria kitakachosimamia mabadiliko hayo kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Kwa mfano sheria mpya itakayoanzishwa itatoa uwezo kwa bodi ya mikopo kujitegemea zaidi na kwamba bodi hiyo itaongozwa na mkurugenzi ambaye atakuwa katibu wa bodi.

Hatua hiyo imefikiwa kutokana na kuonekana kwamba imekuwa ni vigumu kwa mkurugenzi wa mfuko wa elimu kuweza kuhudumia sambambana taasisi zilizokabidhiwa kwa maana ya idara na mfuko wa elimu kama inavyoelekeza sheria iliyopo.

Aidha kamati imefurahishwa kuongeza  uwakilishi wa wajumbe wa bodi ya mfuko katika sheria mpya itakayoanzisha hoja ya serikali juu ya ongezeko hilo la wajumbe wa bodi ni kwamba bodi itakuwa na uwakilishi mpana wa waombaji kupitia tasisi zao za utoaji elimu, fedha na mipango ya maendeleo.

“Hoja hiyo tumeiona ni ya msingi kwa vile uwakilishi mpana waombaji kupitia tasisi zao za utoaji elimu fedha na mipango ya maendeleo vile uwakilisihi huo unaweza ukachangia kuleta ufansi katika maendeleo ya mfuko” alisema Mwenyekiti huyo.

SERIKALI YAHIMIZA NIDHAMU

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kuhimiza nidhamu na tabia njema kazini kwa wafanyakazi wake wote ili waweze kutoa huduma safi na zenye viwango.

Hayo yamelezwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar wakati akijibu maswali katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini hapa, Dk Sira Mamboya wakati akijibu suala la msingi aliloulizwa na Hija Hasan wa Jimbo la Kiwani juu ya nidhamu kwa wafanyakazi wa hospitali za serikali ambapo wanaonekana nidhamu zao ni tofauti na nishamu zinazooneshwa na hospitali za kijeshi.

Naibu huyo alikiri kuwa hospitali za kijeshi zinaongozwa kwa misingi ya nidhamu za kijeshi zaidi kuliko hospitali za uraiani kutokana na miongozo yao ya utendaji kazi kwa kuwa hufunzwa heshima zaidi kwa wakubwa zao na wanaowahudumia.

Hata hivyo alisema wizara ya Afya imo katika mkakati zaidi ya kuinua kiwango cha nidhamu katika hospitali zake zote ili zitoe huduma kwa kuzingatia usawa na heshima kama inavyotakiwa na sheria.

Mwakilishi huyo pia alitaka kujua  suala la huduma bora zinazotolewa hospitali ya Jeshi katika kambi ya Vitongozoji ambapo usafi, maabara nidhamu na vitanda kwa wagonjwa zinatofautiana sana na hali  ya usafi zinazoikabili hospitali za Mkoani, Wete na Chake Chake na kuhoji wizara imejipanga vipi kuondokana na aibu ya hospitali zake.

Aidha mwakilish huyo aliuliza sababu ya wizara iliyopelekea kushindwa kutoa msaada wa madawa hospitalini hapo  huku ikifahamika kwamba huduma zinazotolewa zinazidi wagonjwa 2000 kwa mwezi .

Akijibu maswali hayo Naibu huyo alisema anakubaliana  na Mwakilishia huyo kuwa hospitali hiyo ya kijeshi ya Vitongoji ni safi na yenye barabara bora na huduma zitolewazo ni bora ubora ambao kwa ujumla zinatofautiana sana na hospitali za Mkoani, Wete na Chake Chake.

Alisema hospitali ya Vitongozi ni mpya kabisa na imefunguliwa hivi karibuni wakati hospitali za Mkoani, Wete na Chake kimajengo haziwezi kulingana hata kidogo kwa ubora na hospitali  zilizojengwa zaidi ya miaka  30 iliyopita ambazo zimechakaa na zinahitaji matengaenezo makubwa.

 Mwakilishi huyo pia alitaka kujua kwa vile jeshi limewapatia nyumba wafanyakazi wawili waliopatiawa na wizara ambao ni mtaalam wa mama na mtoto na mtaalam wa maabara kwa nini serikali haitoi mwongozo kwa vikosi vya SMZ kuiga mwenendo huo.

Akijibu hilo naibu waziri huyo alisema wizara ya afya haijashindwa kutoa dawa katika hospitali ya jeshi ilioko Vitongoji na hospitali nyengine zote za vikosi ila wanapaswa kufuata taratibu za maombi ya dawa hizo utaratibu ambao ndio unaotumika kwa maombi ya dawa kutoka vituo vyote vya Serikali 

Hata hiyo alisema alisema wizara yake inayo taarifa ya huduma zinazotolewa na hospitali ya Vitongji na jinsi inavyowasaidia wananchi pia tuna ushirikiano wa karibu katika kutoa huduma kwa wakina mama wajawazito na watoto wachanga ambao ni kutoka Wizara ya Afya pia tunawashirikisha kwenye Warsha semina na mikutani mengine.

Suala la uongozi wa jeshi kuipata nyumba , wizara kwa ajili ya kukaa wafanyakazi wa wizara hiyo alisema suala hilo linazungumzika na wizara itakaa na wenzao wa vikosi kuona jinsi gani wataweza kulifanikisha suala hilo.

BARABARA ZETU NI BOMBA

NAIBU Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasilano, Issa Haji Gavu barabara zote zilizojengwa na serikali zimefikia viwango vinavyokubalika.

Amesema si kweli kuwa bara bara ya Mtambile na Mwambe ilioko Kusini Pemba kuwa imejengwa chini ya kiwango na tathmini imekuwa ikifanyika kila muda wa ujenzi unapoendelea.Alisema tathmini ya mwisho iliyofanyika ilionyesha ubora wa hali ya juu wa barabara hiyo 

Hayo aliyaeleza wakati akijibu suala la msingi aliloulizwa na Mwakilishi wa Kiwani Hija Hassan Hija aliyetaka kujua ni kwa nini bara bara hizo zinaonyesha kujegwa chini ya kiwango na ni lini serikali itafanya tathmini za awali na kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya kampuni inayoendelea na ujenzi wa barabara.

“Kwa kuwa matuta yaliyowekwa katika bara bara ya Mtambile Mwambe husababisha ajali nyingi baada ya kuzipunguza na matokeo yake yamepelekea vifo vya baadhi ya watu  na zaidi ya 15 kulazwa hospitali, je Mheshimiwa haoni kuwa matuta hayo hayakuwekwa kwa kuzingatia ubora wa matuta ya kupunguza ajali” alihoji Hija. .

Pia alitaka kujua ni kampuni gani iliyopewa jukumu la kujenga barabara hizo sita na barabara zipi zimechukuliwa kama kigezo cha uzoefu na ufanisi wa Kampuni hiyo katika kanda ya Afrika ya Mashariki.

Alisema kuwa serikali ya Mapinduzsi ya Zanziba ilipata ufadhili kwa kujenga bara bara sita za vijijini kusini Pemba kupitia serikali ya Norway ambapo barabara zenyewe ni Mtambile, Kengeja, Mtambile, Kangani na Mizingani, nyengine ni Wambaa, Kenya Chambani, Chanjaani Tundauwa na Chanjaani Pujini.

Barabara hizo zinajengwa na idara ya UUB – Pemba kwa kusaidiana na Mshauri Muwelekezi – kampuni ya Poyry ya Uswiss mradi huu unatekelezwa kwa mfumo wa nguvu kazi (Labour based) ambapo wafanyakazi wa vijijni zinapopita barabara hizo hupata ajira na hivyo hutekeleza sera ya serikali ya kupunguza umaskini.

“Mheshimiwa hakuna kampuni iliyopewa kujenga barabara, hizo kampuni inayoleta lami hii ni AL_ AFRAD Trading CLC ya Oman kwa kushirikiana na kampuni ya kizalendo ya Nebeel –Enterprises lami hiyo inatoka Afrika ya kusini na Bahrain ”alisema waziri huyo

Alifahamisha kuwa ubora wake unalingana na matakwa ya lami inayotakiwa kutumika katika ujenzi kama ilivyoelezwa katika zabuni ya lami hiyo.

Matuta yaliyowekwa katika barabara Mtambile na Mwambe ni ya muda mrefu yaliwekwa kutokana na maombi ya kilio cha wananchi kutoka sehemu iliyopita barabara hii wakati ambapo ujenzi ulikuwa unaendelea.

Hata hivyo wakati utiaji wa lami ukiendelea bababara hiyo matuta hayo yamekuwa yakirekebishwa kulingana na ubovu na kiwango kinachohitajika.

Advertisements

3 responses to “Bora mtusamehe hatuna pesa-SMZ

  1. LOH LOH LOH LOOOOOOOOOOH!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    HASBIYALLAH LOHHHH MIJIZZI MIKUBWA HAINA PESA HAINA HATA HAYA LLOOOOOH POOOOOOO

  2. Baraza la Wawakilishi halionekani kua serious ni kama vile wanacheza drama tu. Wakiondoka hapo kila mmoja na lakwe.Baraza badilikane mtupe wananchi matumaini. Inaonekana mupo hapo kwa posho tu na sio jengine. Kama ni hivyo mimi naona hakuna haja ya kua na baraza. Wakurugenzi na makatibu wakuu na makimishna alochagua Dr Shein wanatosha kuisaidia Serikali. Serikali kubwa yenye magharama kibao lakini haina lolote inalolifanya.

  3. pesa mutakuwa nazo vipi na nyinyi mushawaka benki zenu huko swiss na kujinunuliya nyumba nchi za nje na kujirundikiya mali na kula uluwa na familiya zenu ndio maana munasema hamuna pesa maana mulizo ibi munataka kutumiya nyinyi na familiya zenu sio sawa tunavunja muungano ss na tutalana wenye kwa wenyewe au bora mukimbiye kabisa hapa znz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s