Umenifahamu babu Duni?

Waziri asiye na wizara maalum, Machano Othman Said (kulia) akibadilishana mawazo na Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mjini Zanzibar lililoanza leo.

MWENYEKITI wa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (PAC) Omar Ali Shehe ameishauri serikali kupitia upya sheria za fedha na kupewa uwezo “meno” ikiwa ni hatua ya kupambana na ukiukaji wa matumizi ya fedha za umma katika taasisi za serikali.

Ushauri huo umetolewa jana katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea huko Chukwani Mjini Zanzibar.

Shehe alisema sheria zilizopo ni dhaifu na hazisaidii  kukomesha makosa ya matumizi ya fedha za umma hivyo serikali kama inataka suala hilo likomeshwe lazima izitazame upya sheria zake.

Shehe alikuwa anatoa mapendekezo ya kamati yake katika kikao cha Baraza la Wawakilishi ambapo alisema ingawa kamati yake imegundua dosari nyingi katika mfumo wa matumizi ya fedha za umma, wanaohusika hawachuliwi hatua na serikali na hatua zinapochukuliwa wanaotiwa hatiani hutozwa faini.

Shehe ambaye ni Mwakilishi wa Chake Chake huko Pemba, alisema adhabu inayotolewa sasa kwa makosa ya ukiukaji wa sheria na kanuni za matumizi ya fedha ni ndogo kulinganisha na ukubwa wa makosa yanayofanyika kwa taasisi za umma za ubadhirifu wa fedha.

“Kwa mfano chini ya kifungu cha 38 cha sheria ya fedha za umma Na. 12 ya mwaka 2005, adhabu kwa anayekiuka sheria hiyo ni faini kwa kutozwa sh. 500,000 au kifungo cha miaska miwili baada ya kutiwa hatiani.”.alinukuu kifungu hicho cha sheria huku akisema adhabu hiyo haitoshi.

Akisititiza kwamba adhabu ya aina hiyo ni hairidhishi na ni kichekesho, kwa kuwa ni ndogo mno kwa mtendaji amma na mtu aliyejikusanyia mabilioni ya fedha za umma kwa manufaa yake binafsi.

“Sheria za fedha zipitiwe tena na ikiwezekana zitoe adhabu ya kila kifungu kinachohusika na isiwe kwa ujumla kama ilivyo sasa, ili adhabu inayotolewa ilingane na  wakati na uhalisia wa kosa lenyewe,” alisema Shehe ambaye pia ni Mwakilishi wa Chakechake.

Alisema taasisi nyingi za serikali haziwajibiki ipasavyo na kwamba nyingine zinafanya malipo bila vielelezo na zinapofanyiwa ukaguzi watendaji wake hutoa stakabadhi za udanganyifu.

Alisema taasisi zilizofanyiwa ukaguzi na kushindwa kutoa vielelezo na stakabadhi juu ya matumizi ya fedha za umma ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ofisi ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais na Wizara ya Kilimo na Maliasili.

Nyingine ni Wizara ya Afya, Wizara ya Ardhi, Maji na Nishati (Pemba), Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Baraza la Manispaa, Tume ya Ukimwi,  Shirika la Utalii, Shirika la Bishara la Taifa (ZSTC) Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi (ZIPA), Hoteli ya Bwawani na Chuo Cha Taifa Zanzibar (SUZA).

Hata hivyo alisema kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya mwaka 2008/2009 ambayo hivi sasa iko mbele yao haina tofauti na ripoti zilizopita na kusema kuwa imeonesha udhaifu uliozoeleka wa Taasisi za Serikali, huku hoja nyingi zikiwa zimejirejea kwa taasisi hizo.

Aidha alisema kuwa tatizo jengine linaloendelea kujirejea katika ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ni kukosekana kwa daftari la kuhifadhia mali za kudumu, ambalo linahusu afisi ya Baraza la wawakilishi kama ilivyoripotiwa na ripoti hiyo.

“Tatizo hili takriban linaendelea kuzikabili taasisi zote za Serikali, tunachotaka kusema ni kwamba baada ya kamati kukaa na ofisi ya rais, Fedha, Uchumi na Mipango na Maendeleo ilifahamishwa kuwa sasa lile daftari la pamoja ambalo lenye kutoa muongozo wa kuhifadhia mali limeshatayarishwa.

Hivyo imezitaka taasisi za Serikali zirekebishe kasoro hizo ili kamati ikifanyia kazi ripoti kusiwe na majibu yaliyozoeleka ya kukosa muongozo kutoka wizara husika.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa adhabu ya kutozwa faini isiyozidi 500,000 baada ya kutiwa hatiani kwa mujibu wa sheria za fedha ni ndogo ukilinganisha na makosa yanayofanyika, na kuiomba sheria hiyo ipitiwe tena na ikiwezekana zitoe adhabu ya kila kifungu kinachohusika na isiwe kwa ujumla kwa ilivyo sasa, ambayo ilingane na wakati na uhalisia wa kosa lenyewe.

MWISHO

Sheria ya afya ya kuwadhibii wazazi iko njiani

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuwasilisha mswaada wa marekebisho ya sheria serikali utakaowabana na kuwawajibisha wazazi ambao huwachukulia dhamana watoto wao wanaokwenda kusoma.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza juu ya madakatari wanaokwenda kusoma nje ya nchi na baadae kukataa kurudi kuitumikia nchi yao, katika ukumbi wa baraza la wawakilishi kaatika kikao kilichoanza jana Mjini hapa.

Duni alisema serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kwa ajli ya kuwasomesha wananchi wake lakini baada ya masomo hukata kurudi kutokana na mishahara midogo lakini wansahau kufanya kazi kwa uzalendo na kuitumikia nchi yao kitendo ambacho kinafaa kudhibitiwa ili kuwafanya wananchi waipende nchi yao na kuweza kutoa michango yao kwa serikali yao.

“Ni kweli tabia hii imekuwa ikifanyika serikali imekuwa ikisomesha wataalamu wake na baadae hukataa kufanya kazi kw akisingizio cha mishahara midogo, ni kweli kila mmoja anapenda alipwe vizuri lakini tatizo hili kuna wazazi walikuja kusaini mikataba kwamba watoto wao wanakwenda kusoma lakini wakimalzia masomo watarejea matokeo yake wote wamekwenda kufanya kazi Muhimbili, sasa tuwakamate wazee wao? Alihoji Waziri huyo.

Alisema kitendo cha madaktari hao kukataa kutoa mchango wao katika nchi yao sio kizuri na hakileti sura nzuri kwa Serikali kwa kuwa serikali imewasomesha kwa lengo la kusaidia wananchi wake wapate huduma nzuri.

“Tutarekebisha sheria wazee wawajibike, kwani suala la watu kusomeshwa na Serikali baadae wasirejee halitii moyo hata kidogo”, alisema Duni.

Naibu Wazira hiyo Dkt Sira Mamboya alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itamlipa daktari kiwango cha mshahara wake kutokana na uwezo wake ulionao na kuwataka madaktati wawe wazalendo wa kulipa fadhila za Serikali wanazopata wakati wanapokuwa masomoni.

Dkt. Sira alitoa kauli hiyo kufuatia suali mla nyongeza lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Rahaleo, Nassor Salum Ali, alietaka kujua sababu ya madaktari wengi kutorudi Zanzibar wanapoamaliza masomo yao, jambo ambalo linapelekea kuwepo kwa usumbufu mkubwa wa madaktari.

Alisema kuwa pamoja na Serikali kutumia fedha nyingi kuwasomesha madaktari lakini wengi wao wamekuwa wakishindwa kurudi nyumbani kufanyakazi jambo ambalo linaisononesha Serikali.

“Imani ya mtu huwezi kuibadili, lakini ni vizuri wakalipia fadhila kwa serikali kwa sababu serikali ndio iliowapeleka huko kusoma na kuwalipia gharama zote wakiwa masomoni hakuna anaesoma kwa kulipia pesa zake mwenyewe sote tumeanza kusoma hadi kumaliza kwa fedha za serikali” alisema daktari huyo ambaye ni mteule wa rais.

MWISHO

Zanzibar upo udhalilishaji watoto

WIZARA ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya vijana, Wanawake na Watoto, imekiri kuwepo kwa ongezeko kubwa la vitendo vya udhalilishaji wa watoto linaloendelea.

Waziri wa Wizara hiyo Bi Zainab Omar Mohammed aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba bado tatizo hilo licha ya serikali kulifanyia kazi na kuchukua hatua mbali mbali lakini bado vitendo vya udhalilishaji kwa watoto linaendelea

Awali mwakilishi wa nafasi za wanawake Amina Iddi Mbarouk alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo la udhalilishaji watoto kwa kuwa suala hilo limekuwa likizidi kila kukicha.

Waziri huyo alisema serikali katika kukabiliana na vitendo hivyo vya udhalilishaji watoto Wizara yake imeunda kitengo maalumu cha hifadhi ya mtoto ambacho kinaunganisha juhudi za wadau wote pamoja katika kushughulikia masuala ya watoto hapa Zanzibar.

Aisha alitoa wito kwa jamii kuwa wasisite kutoa taarifa za udhalishaji wa watoto kwenye taasisi zinazohusika na kushirikiana kikamilifu na vyombo vya sheria, na kuhakikisha kuwa hawapotezi ushahidi wa kesi hizo.

Aidha alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2009/2010 wizara yake imepokea malalamiko ya watoto waliodhalilishwa wapatao 363 kwa Unguja na Pemba huku kesi 870 zilizoripotiwa katika hospitali ya mnazi mmoja kesi hizo zilihusisha udhalilishaji wa kingono.

Alisema wizara yake pia kwa kushirikiana na shirika la kuwahudumia watoto UNICEF imetoa ripoti ya udhalilishaji ambapo tamwimu zinaonesha kwamba asilimia 9 ya watoto wa kike na asilimia ya watoto wa kiume waliohojiwa katika utafiti huo wamekiri kufanyiwa udhalilishaji wa kingono.

Katika suali lake hilo mwakilishi huyo alitaka kujuwa Wizara ina mikakati gani katika kupunguza tatizo la udhalilishaji wa watoto, ambalo limefikia asilimia 50 jamb ambalo waziri amesema sio kweli “wizara inapenda kujua taarifa hizo zimetoka wapi na zimetolewa na nani, hata hivyo naomba nikubaliane na ongezeko la vitendo vya udalilishaji kwa watoto hapa kwetu” alisema waziri huyo.

MWISHO

Sio wategemezi kwa kuwa na madaktari wa kichina -SMZ

NAIBU Waziri wa Afya Dkt Sira Mamboya amesema kuwa kuwepo kwa madktari wa Kichina katika hospitali zake hapa Zanzibar sio utegemezi kwa kuwa wanakuja kusaidia kutoa huduma.

Alisema wadaktari hao wa kichina wapo katika hospitali ya Abdallah Mzee ya Pemba na Mnazimmoja Unguja na jambo hilo haliwezi kuifanya wizara kuwa ni tegemezi kwani ni makubaliano baina ya nchi mbili hizo.

Akijibu swali katika kikao cha Baraza la wawakilishi la Mwakilishi wa Mkoano Abdallah Mohammed Ali, aliyetaka kujua ni madaktari wa kichina wanaokuja kufanya kazi na mara huondoka kwa sababu gani zinazopelekea madaktari wao kuondoka mara kwa mara na kukosekana huduma katika hospitali hizo.

Mwakilishi huyo alitaka kujuwa ni lini Serikali itaondokana na utegemezi wa madkatarii wa kichina wanaoingia nchini na kufnaya akzi na baadae kuondoka na kuwacha hospitali kutokuwa na wataalamu .

Naibu waziri alisema kuwa ni jambo la kawaida kwa hospitali kubwa na hasa zile za rufaa kuwa na wataalamu wa aina mbali mbali na kutoka nchi tofauti kwa utendaji uliosahihihi na huduma bora.

“Kuwepo kwa madaktari wa kichina katika hospitali zetu hizi si jambo la kuitwa kuwa ni utegemezi, bali ni makubaliano ya nchi hizi mbili, ambazo yanajenga uhusiano na udugu wa milele”, alisema naibu huyo.

Hata hivyo alisema kuwa hakuna kanuni wala sheria ila ni makubaliano na umoja uliojengeka katika kutekeleza uhusiano huo, na hiyo ni baadhi ya mikakati ya Serikali ya China kuzisaidia nchi masikini.

Aidha alifahamisha kuwa uhusiano huo sio tu kwa kuleta madaktari bali hata kuwasomesha vijana wao fani mbali mbali, ambapo hivi sasa kuna vijana wengi wako nchini huko wanasomeshwa.

MWISHO

Wanawake 267 wamepatiwa mikopo ya benki

JUMLA ya wajasiriamali wa kike 267 wamepatiwa mikopo kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar, ambapo ni sawa na asilimia 40 ya watu binafsi waliokopa katika benki hiyo, hadi kufikia Febuari 28 mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Mendeleo, Omar Yussuf Mzee katika kikao cha baraza la wawakilishi kilichoanza jana mjini Zanzibar.

Alisema kuwa kuwa mikopo hiyo iliyotolewa haijumuisha wajasiriamali wa kike waliomo katika vikundi vya SACCOS ambao wamekopa kupitia vikundi vyao.

Jibu la waziri huyo linatokana na swali la Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Mwanaidi Kassim Mussa alitaka kujua ni wajasiriamali wangapi wa kike ambao wameweza kupatiwa mkopo katika benki ya watu wa Zanzibar na Serikali imekusudia kulitekeleza kwa muda gani.

Aidha kuhusu kuanzishwa kwa benki ya kike hapa Visiwani Waziri huyo alisema kuwa inaweza kuchukuwa muda mrefu na pia inahitaji mtaji mkubwa lakini ni wazo zuri ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.

Alifahamisha kwamba kutokana na hali hiyo Serikali imeona ni busara kuanzisha tawi la benki ya wanawake Tanzania Bara hapa Zanziba, na kama shughuli zote zitakuwa sawa wanatarajia kulifunguwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa benki ya wanawake ni kuwawezesha wanawake ili kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na hatimae kuwapunguzia umasikini wa kipato.

Alisema suala la uanzishwaji wa benki za wanawake kuwepo Unguja bila ya kuanzishwa Pemba Waziri huyo alisema jambo lolote linapoanzishwa huanza sehemu moja na kutoa mfano hata beki ya wanawake wa Tanzania imeanza katika mkoa wa Dar es salaam na baadae ndio kufikishwa katika mikoa mengine.

Alisema hivyo ipo haja ya kufunguliwa tawi na Pemba ili kuwarahisishia wanawake wa Pemba kujiunga na benki hiyo itakapoanzishwa lakini kwa kuanzia itabidi ifunguliwe Unguja kwanza na baadae kupelekwa huko tawi lake.

Baadhi ya wajumbe walitoa ushauri wa kuaznishwa benki za kijamii ili ziwapunguzie mzigo mkubwa wa riba kwani mabanki makubwa huwa na riba kubwa jambo ambalo wananchi wengi hushindwa kujiunga nazo kutokana na mitaji midogo walionayo.

“Mabenki haya makubwa lazima uwe na fedha nyingi lakini riba yake ni kubwa jambo hili wananchi wengi hushindwa kwend akuchukua mikopo na kuanzisha biashara lakini kwa nini serikali isiwe na benki hizi za kijamii ambazo riba yake ni kidogo na wananchi wengi wataweza kujiunga nazo” alihoji Rashid Seif Mwakilishi wa Ziwani Pemba.

Waziri huyo serikali haimkatazi mtu kuanzisha benki ya jamii (Community bank) ni wazo zuri lakini ili uweze kufungua banki ya kijamii lazima uwe na mtaji wa shilingi milioni 15 na upate watu wa kununua hisa wapatao 20 wakati serikali haitakiwi kutia mkono wake katika ununuzi wa hisa hizo.

MWISHO

Kupatikana taarifa sahihi za fedha bado ni kikwazo

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri kuwepo kwa tatizo la kupata taarifa kamili juu ya ulipaji wa mapato ya fedha kutoka Ofisi za Ubalozi zilizonje.

Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, wakati akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Chonga, Abdallah Juma Abdallah, katika kikao cha baraza hilo kilichoanza jana.

Aboud alisema kuwa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawasiliana na Uhamiaji ili kupatikana taarifa juu ya wageni wanaoingia Zanzibar na kujua ni wangapi wanalipia fedha za VISA katika ofisi za balozi zao waliopo nje.

“Usahihi wa taarifa hii utapelekea Serikali ya Zanzibar kufuatilia fedha zinzaostahiki kulipwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuchukuwa hatua ipasavyo”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa Serikali haitaweza kukaa kimya na itaendelea kuhakikisha kuwa mapato baina ya Serikali yanapatikana kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na taasisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia kw aukamilifu ugawaji wa mapato baina ya Serikali mbili kwa ajili ya kuhakikisha kila upande unapata haki kwa mujibu wa sheria.

Katika suali lake mwakili Abdallah alitaka kujuwa Serikali itachukuwa hatua gani ili kuhakikisha pesa zalipa kodi wake hazipotei kiholela na suala la kunyamaza haino kuwa ni jambo la kutowajibika ipasavyo.

MWISHO

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s