Uhusiano wa katiba mbili

Mohammed Khamid Hamad ni mwanasheria kutoka afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar akitoa mada juu ya uhusiano katiba ya Zanzibar na katiba ya Muungano

UHUSIANO KATIBA YA ZANZIBAR NA KATIBA YA MUUNGANO

Utangulizi

Tukio moja muhimu katika maendeleo ya kikatiba ya nchi yetu ni kuundwa kwa Muungano kati ya Jamuhuri ya watu wa Zanzibar na Jamuhuri ya Tanganyika. Huu ulikuwa ni Muungano wa nchi mbili zilizohuru. Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Kikoloni hadi mwaka 1963 ambapo ilipata uhuru wake na Tanganyika ikapata uhuru mwaka 1961. Zanzibar ilifanya Mapinduzi Januari 1964 na miezi mitatu baadae, April, 1964 iliingia katika Muungano na Tanganyika baada ya viongozi wawili yaani J.K Nyerere na A.A.Karume waliposaini Mapatano ya Muungano (Articles of Union).

Mapatano ya Muungano

Kabla ya kuanza kuelezea uhusiano uliopo kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya Muungano ni vyema kidogo kuelezea Mapatano ya Muungano na uhusiano wake na katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar. Suali kubwa la Kujiuliza ni waraka gani kati ya hizi unakua juu ya mwenzake?

Waraka pekee ulioziunganisha nchi hizi mbili na kuunda Muungano ni Mapatano ya Muungano. Mapatano haya yalielezea mambo ambayo nchi hizi mbili ziliungana pamoja na mambo mengine muhimu yanayohusu namna ya muungano huo. Mapatano haya ndio Katiba mama ya Muungano huu. Ndio sheria kuu katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo kutoka kwake ndio Katiba ya Zanzibar na ile ya Muungano imepata mamlaka. Kwa maneno mengine katiba hizi mbili zimetokana au ni viumbe vya Mapatano ya Muungano. Kwa hiyo Mapatano ya Muungano ndio waraka uliopo juu ya katiba hizi na sheria nyengine zozote. Hakuna sheria au chombo chengine chochote kitachokuwa juu ya Mapatano ya Muungano.

Kwa msingi huo Mapatano hayo ya Muungano hayawezi kubadilishwa na chombo chochote hata Bunge au Baraza la Wawakilishi isipokuwa tu kwa makubaliano ya nchi mbili zilizoungana.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Zanzibar

Baada ya Uhuru wa Tanganyika 1961, Tanganyika ilikuwa na Katiba yake, Katiba ya Jamuhuri Tanganyika. Zanzibar nayo baada ya uhuru wa 1963 ilikuwa na Katiba yake, Katiba ya Zanzibar ya 1963. Hata hivyo Katiba hii ilidumu kwa muda wa mwezi mmoja tu. Mwezi January, 1964 Mapinduzi ya Zanzibar yalitokezea na kuondoa serikali iliyokuwepo na kuwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi pia ilifuta Katiba iliyokuwepo ya mwaka 1963 na Zanzibar kuongozwa bila ya Katiba hadi mwaka 1979 ambapo Katiba ya kwanza baada ya mapinduzi ilipoundwa ambayo nayo ikafuatiwa na Katiba ya mwaka 1984.

Kwa vile Muungano ulianzishwa kwa haraka sana, Mapatano ya Muungano yalielezea  kuwa Katiba ya Kudumu ya Jamuhuri ya Muungano itayarishwe na iyanze kutumika baada ya mwaka mmoja. Mapatano hayo yakeleza kuwa kwa kipindi hicho cha mwaka mmoja mpaka hapo katiba ya kudumu itakapoundwa Muungano utaongozwa na katiba ya muda ambayo ni Katiba ya Tanganyika. Katiba ya muda ilichukuliwa kama ndio katiba ya kudumu na ilifanyiwa marekebisho kadhaa ambayo hayakuwa sahihi. Baada ya kuchukuwa mwaka mmoja Katiba hiyo ilichukuwa miaka kadhaa hadi hapo katiba ya kudumu ilipoundwa mwaka 1977, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Baada ya kuona kidogo historia fupi ya mpaka nchi zetu kuwa na katiba mbili hizi, sasa tuje katika kile hasa tulichokusudia. Kumekuwa na hoja nyingi zinazotolewa na watu wa kawaida na hata wasomi ambao wakati mwengine hatutarajii kusikia kutoka kwao baadhi ya hoja ambazo hazina msingi wowote wa kisheria. Hoja hizo zinahusiana na; ni katiba ipi kati ya ile ya Jamuhuri ya Muungano,1977 na ile ya Zanzibar, 1984 iko juu ya mwenzake?

Tumesikia kutoka baadhi ya wasomi wanasheria wakidai kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano ndio katiba mama na ile ya Zanzibar ni mtoto wa katiba hiyo. Hoja hii haina msingi hata kidogo kutokana na hoja zifuatazo:

Hoja ya kwanza ambayo ndiyo kuu inatokana na muundo wa Muungano wenyewe. Ni vyema ifahamike kuwa nchi mbili hizi hazikuungana kwa mambo yote. Zanzibar na Tanganyika ziliungana kwa baadhi ya Mambo tu. Kuna mambo bado yapo katika mamlaka ya Zanzibar ambayo si ya Muungano. Mambo hayo hayawezi kuingiliwa na chombo chochote cha Jamuhuri ya Muungano. Si Bunge wala Serikali ya Jamhuri ya Muungano kinachoweza kuyaingilia mambo hayo. Kuthibitisha hayo ibaya 64 (2) ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano 1977 inaeleza wazi kuwa mamlaka yote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza La Wawakilishi. Ibara ndogo ya 3 ya ibara ya 64 inaeleza wazi kuwa endapo Bunge litatunga sheria yoyote ambayo iko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi sheria hiyo itakuwa batili na itatenguka. Hoja inaonesha wazi kuwa hizi ni mamlaka mbili tofauti ambapo kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ni sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi tu ndio yenye nguvu. Katiba ya Zanzibar imetungwa na Baraza la wawakilishi hivyo ndio katiba iliyojuu kuliko ya Jamhuri ya Muungano kwa mambo hayo ambayo yako chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Hoja ya pili inatokana na hoja inayoelezwa na baadhi ya wasomi kuwa Zanzibar na serikali yake imeanzishwa na katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977. Hoja hii nayo si sahihi. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, 1977 Sehemu ya Nne imeelzea kuhusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi. Kuelezewa katika katiba hiyo hakumaanishi kuwa Katiba hiyo ndio inayoanzisha vyombo hivyo. Vyombo hivyo vimetajwa na katiba hiyo kama ni taarifa tu. Suali la kujiuliza ni kwamba Jee Zanzibar isingeliweza kuanzisha vyombo vyake kama mamlaka hayo hayajaelezwa na Katiba ya Jamuhuri? Jibu ni hapana. Suala la kuanzisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vyombo vyengine vinavyohusu mambo yasiyo ya muungano vya Zanzibar viko katika mamlaka ya Zanzibar kama tulivyoona hapo juu. Kilichofanya katiba ya Muungano kuvitaja vyombo hivyo ni kuvitambua kuwepo kwake tu nasi kuvianzisha kwani vyenginevyo ingelikwenda kinyume na matakwa ya ibara ya 64 kama tulivyoona hapo juu.

Hoja nyengine ni ya kihistoria. Kama tulivyoona hapo juu Zanzibar ilikuwa na katiba baada ya Uhuru wa 1963 na katiba hiyo ilifutwa mwaka 1964 mara tu baada ya mapinduzi ya 1964. Zanzibar haikuwa na katiba hadi mwaka 1979. Kati ya kipindi chote cha 1964 hadi 1979 Katiba ya Jamuhuri ya Muungano siyo ilikuwa ikitumika Zanzibar. Zanzibar iliongozwa na Sheria zilizotungwa na Baraza la Mapinduzi(Decrees). Hii inathibitisha kuwa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano haihusiki na mambo ya Zanzibar. Asili ya katiba ya Zanzibar ni kama ilivyoelezwa katika tamko la kuunda katiba ya Zanzibar, nayo ni mamlaka ya watu wenyewe wa Zanzibar.

Hoja nyengine inatokana na uzoefu kutoka nchi nyengine zenye Muungano wa nchi mbili au zaidi. Muungano wa Marekani na ule wa Uswizi (Switzerland) unatupa uzoefu kuwa licha ya Katiba ya Muungano kila mshirika wa Muungano anakuwa na katiba yake. Katiba ya Muungano haielezei mambo yasiyo ya Muungano. Mambo hayo huelezewa na katiba za washirika wa Muungano huo ambazo katika mambo hayo zinakuwa na nguvu kuliko hiyo Katiba ya Muungano. Na hivyo ndio Muungano wetu ulivyo. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano, 1977 haiwezi kulazimisha muundo wa serikali wa Zanzibar uwe vipi. Hilo ni jambo ambalo liko katika Mamlaka ya Zanzibar na vyombo vyake. Kutafautiana na katiba ya Muungano haiwezi ikaelezwa kuwa Zanzibar imekiuka katiba ya Jamuhuri ya Muungano kama inavyosemwa sasa hivi juu ya Muundo wa serikali mpya ya Zanzibar.

Hitimisho.

Hoja zote zilizoelezwa hapo juu zinaelekeza hitimisho moja tu ya kwamba, hakuna katiba iliyokuwa juu ya mwenzake katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa katika mambo yaliyo katika  mamlaka yake. Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania ina nguvu katika mamlaka yake na ile ya Zanzibar ina nguvu kuliko ya Muungano katika mambo yaliyochini ya mamlaka yake. Katiba ya Muungano inahusu mambo ya Muungano na yale yanayohusu Tanzania Bara. Katiba ya Zanzibar ina mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano ambayo yako chini ya Zanzibar. Katika mambo haya Zanzibar haiwezi kuwa mtoto wa Katiba ya Muungano na pia Katiba ya Muungano kuwa mama juu ya mambo haya. Zanzibar haiwezi kuelezewa kuwa imekiuka katiba ya Muungano kwa kufanya mabadiliko ambayo yako kinyume na TAARIFA tu ziliyomo katika Katiba ya Muungano. 

Mohammed Khamis Hamad

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s