Tuwe na maamuzi yetu wazanzibari

Wakili Awadh Ali Said akichangia mjadala wa katiba mpya ya Tanzania katika kongamano lililofanyika kwenye ukumbi wa Eacrotanal Mjini Zanzibar

KONGAMANO la kudajadili katiba mpya ya Tanzania linaloendelea kufanyika Zanzibar limechukua sura mpya baada ya wanasheria na wananchi kuishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuunda tume yake ya kukusanya maoni badala ya kutumia tume ya pamoja ya Muungano.

Wito huo umetolewa jana washiriki mbali mbali wakati wakijadili mada kuhusu katiba za Tanzania na Zanzibar, changamoyo juu ya mianya na utata uliopo iliyowasilishwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee Ibrahim katika ukumbi wa Eacrotanal Mjini Unguja.

Mwanasheria maarufu Zanzibar, Awadh Ali Said amesema Zanzibar haitonufaika na mjadala wa marekebisho wa katiba ya Muungano kama tume itafanya kazi hiyo ya kukusanya maoni Tanzania bara na Zanzibar kutokana na wananchi wake ni wachache kulinganishwa na Tanzania bara.

Kwa msingi huo alisema ili haki itendeke na kupata maoni ya mustakabali wa muungano juu ya muundo na aina ya Muungano ni vyema kukawa na tume mbili zitakazofanya kazi hizo moja upande wa Tanzania bara na nyengine Zanzibar.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iunde tume yetu ya kukusanya maoni kwa sababu tupo wachache na tukiwa katika mkumbo wa pamoja hatutanufaika kulinga na mazingira ya Zanzibar” alisema Mwanasheria huyo huku akipigiwa makofi na washiriki wa kongamano kuonesha kuwa wanamuunga mkono.

Alisema Zanzibar ina mambo mengi ya kujadili kuhusu maslahi ya Zanzibar ikiwemo suala la jumuiya ya afrika mashariki kutokana na kuwa kuna mambo ambayo hayamo katika orodha ya mambo ya muungano kama afya, utalii na kilimo na ndio maana ipo haja kwa Zanzibar kuwa na ushiriki katika jumuiya hiyo ili iweze kutetea ipasavyo maslahi yake.

Naye Ahmed Omar Khamis alisema rais wa kwanza Zanzibar, Mzee Amani Karume hakuwa na mchango mzuri katika kuandaa makubaliano ya muungano na ndio maana kero nyingi zinajitokeza baada ya kutozingatiwa maslahi ya kisaisa na kiuchumi.

Hata hivyo alisema kwamba ili marekebisho ya katiba yalete faida na kuondoa kero zilizopo hivi sasa lazima kuwe na tume zitakazoweza kufanya kazi tofauti ikiwemo tume ya maoni ya Zanzibar na tume ya maoni ya Tanzania bara.

Alisema tume zilizopita ikiwemo ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali zilifanya kazi za kukusanya maoni kuhusu muungano lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote uliofanyika kutokana mambo hayo yalitawaliwa na ujanja ujanja na kutahadharisha lazima umakini uwepo katika suala hilo.

“Tunaweza tukaletewa tume hapa kama zile za kina Jaji Kisanga na Jaji Nyalali zikatembea Tanzania nzima kukusanya maoni na matokeo ya tume hizo tukaja kuuambiwa asilimia 80 wamesema hivi na asilimia ishirini ndio wamesema hivi kwa hivyo bila ya shaka kwa kuwa sisi kidogo tutaonekana ni wachache kwa hivyo jambo la msingi hapa kuundwe tume itakayokusanya maoni kule Tanzania bara na sisi tuwe na tume yetu ambayo ikusanye kwa mujibu wa idadi yetu” alisema kijana huyo. 

Akichangia katika mjadala huo Omar Mussa Makame alisema katiba ya muungano inahitaji kuangaliwa kwa umakini kwa vile sio mwafaka rais wa Zanzibar kula kiapo cha kutii na kulinda katiba ya muungano wakati amechaguliwa kwa katiba ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar mbali na kuapishwa kulinda katiba ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano hulazimika kula kiapo mara mbili cha kulinda na kutetea katiba ya muungano akiwa kama waziri asiyekuwa na wizara maalumu katiba baraza la mawaziri la Muungano.

Akiwasilisha mada yake Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Ibrahim Mzee Ibrahim alisema vifungu vingi vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vina kasoro na kutoa mfano Rais wa Jamhuri ya Muungano anateuwa mawaziri kwa kushauriana kwa kushirikiana na waziri mkuu bila ya kushauriana na makamu wa kwanza wa rais au rais wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha alisema kwamba katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano imempa uwezo rais wa Jamhuri ya Muungano kuteuwa mawaziri kutoka Zanzibar na kuwapa madaraka katika wizara ambazo hazihusiani na masuala ya Muungano jambo ambalo linahitaji kujadiliwa katika marekebisho hayo ya katiba mpya.

Mzee alisema utata wa katiba katika jamhuri ya Muungano pia upo katika ibara ya 64 wakati bunge la jamhuri limepewa uwezo wa kutunga sheria zitakazotumika hadi Zanzibar wakati katiba ya Zanzibar ibara ya 132 imeweka wazi hakuna sheria itakayotungwa ambayo haihusiani na masuala ya muungano kutumika Zanzibar hadi itakaporidhiwa na baraza la wawakilishi.

Katibu huyo wa baraza pia alitoa mfano wa wizara ya mambo ya ndani na wizara ya ulinzi kuwa yapo mambo ndani ya wizara hizi hayamo katika orodha ya mambo ya muungano kama vile kikosi cha zima moto, magereza, na jeshi la kujengwa taifa JKT lakini wizara hizo zimekuwa zikiongozwa na wazanzibari na kusimamia mambo ambayo hayamo katika orodha ya mambo ya muungano.

Alisema hizo ni kasoro za kikatiba ambazo zinahitaji kuangaliwa pamoja na kesi za uchaguzi zinazohusu wabunge ambapo masharti ya katiba yameweka kesi hizo zisikiliziwa na mahakama kuu ya Tanzania wakati suala la mahakama halipo katika orodha ya mambo ya muungano na kila upande ina mahakama kuu yake.

Mjadala huo wa katiba mpya unayatarishwa na jumuiya zisizokuwa na kiserikali na suala la urais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais wa muungano limekuwa likichukua nafasi kubwa katika mjadala huo kwa wajumbe baada ya wananchi wengi kupinga marekebisho ya 11 ya katiba yaliofuta wadhifa huo.

Jumuiya zisizokuwa za kiserikali zilizoandaa kongamano hilo ni jumuiya ya waandishi wa habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), jumuiya wa wanasheria Zanzibar(ZLS), Kituo Cha Huduma za Cheria Zanzibar (ZLSC) na Taasisi ya Utafiti wa Historia Ukanda wa Bahari ya Hindi Zanzibar (ZIORI)

Advertisements

One response to “Tuwe na maamuzi yetu wazanzibari

  1. Ni ukweli usiopingika kwamba Zanzibar imekua ikipoteza haki zake nyingi ndani ya makucha ya kinachoitwa MUUNGANO. Nasema hivi kwa sababu hicho kinachoitwa MUUNGANO kimekua ni zaidi ya silaha hatari ya kuikandamiza, na hatimaye kuimaliza kabisa Zanzibar.
    Suala zima la katiba; katiba ambayo ni ya jamuhuri ya muungano; jamuhuri ambayo isingekuwepo pasi na kuunganisha mataifa mawili yaliyokua huru; ambayo ni TANGANYIKA na ZANZIBAR, bila kujali ukubwa au udogo wa kijografia, au wingi na uchache wa watu wa mataifa hayo.
    Sasa iweje kuundwe tume moja ambayo itajumuisha maoni ya wakaazi wa jamuhuri hii kwa pamoja??????
    Bila shaka ipo haja ya wazi ya kuundwa tume mbili – ya Zanzibar na ya Bara na kukusanya mawazo ya watu husika na kuyapigia majumuisho kulingana na idadi ya watu husika ili tuweze kujenga taifa lenye katiba isiyoegemea upande mmoja.
    Kinyume cha hivyo katiba hiyo itakayotungwa italeta maana zaidi tukiiita katiba ya TANGANYIKA badala ya katiba ya Mungano.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s