Vibaka Wote Tutawatafutia Kazi-Jahazi Asilia

CHAMA Cha Jahazi Asilia kimeahidi kuwasaka vibaka wote wazururaji kwa kuwakamata na kuwatafutia kazi za kufanya kwa kuwa wanafanya hivyo kutokana na kukosa kazi zinazopaswa kufanywa na vijana hao.

Ahadi hiyo imetolewa na Mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kwa tiketi ya chama hicho katika jimbo la Kwamtipura, Ali Mwadini Faki wakati akinadi sera za chama chake ili achaguliwe kuwawakilisha wananchi katika jimbo hilo.

Alisema iwapo atachaguliwa atahakikisha anawakusanya vibaka wote wanaoishi katika jimbo hilo na kuwatafutia mradi wa kufanya ili kuachana na kazi hiyo ya wizi ambayo imekuwa ikiwadharaulisha katika jamii na wengine kudhurika kutokana na kipigo cha wenye kuibiwa mali zao.

Faki alikuwa akiwahutubia wananchi wa jimbo hilo jana katika kiwanja cha Kivumbi wakati wa mkutano wa kampeni ambapo ahadi hiyo alisema ataietekeleza iwapo wananchi watampa ridhaa kwani amekusudia kumaliza vibaka katika jimbo hilo.

Alisema kwamba vijana wanaofanyakazi hiyo ni watoto wao, hivyo haitakuwa jambo la busara kuwaacha wanaendelea na kazi hiyo kwa vile wamekuwa wakijishughulisha na kazi hiyo kutokana na kutokuwa na nyenzo za kuweza kufanyakazi nyengine na kujiendeleza kimaisha.

“Hawa ni watoto wetu na wanafanya hivi kwa sababu lakini ikiwa utawakusanya na kuwatafutia miradi nina hakika wataacha tu kazi hii maana hawaifanyi kwa kupanda ila kwa kuwa hawana jambo jengine la maana”, alisema huku akipigiwa makofi na idadi kubwa ya vijana.

Ahadi nyengine aliyoitoa mbele ya wananchi wa jimbo hilo ni kuhakikisha kwamba mara tu atakapochaguliwa kuunda baraza la maamuzi ambalo litakuwa linashirikisha watu wote wa jimbo hilo ili ikitokea tatizo liweze kusuluhishwa.

Akielezea muundo wa baraza hilo Faki alisema uundwaji wa baraza hilo litawashirikisha wanachama 200 ambao wote watakuwa ni sawa bila ya kuwa mmoja ni kiongozi kwa kuwa watu wote ni sawa na pia litakuwa likikutana kila mwezi kujadiliana matatizo na mapungufu yaliopo katika jimbo hilo.

“Hivi sasa katika jimbo letu kuna watu zaidi ya 5,000 wanapiga kura lakini wanaofaidika na matunda ya kura zao ni wachachetu, hivyo nikichaguliwa hali hii itaondoka na simuahidi mtu mmoja mmoja kumpatia kitu bali kila mwananchi wa jimbo hili atafaidika na maendeleo ya jimbo hili…nakuahidini kwanza nichagueni hayo yote mtayaona”, alisema huku akishangiriwa.

Akielezea umuhimu wa kukaa pamoja mgombea huyo alisema suala la mjungu lisipewe nafasi na kuwataka watu wote kushikamana katika umoja na kukubaliana na mazuri yaliotangulizwa na wengine.

Faki alisema siasa za majungu zisipewe nafasi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ambapo kila mmoja anajilabu kutafuta wapiga kura wamuunge mkono huku akisisitiza wananchi wa jimbo hilo kuchagua kiongozi bora mwenye lengo la kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.

Alisema angependelea jimbo hilo la kwamtipura liwe mfano kwa majimbo mengine kwa kuendesha siasa za kistaarabu na mshikamano kwani kufanya hivyo kunaweza kusaidia kuendeleza maridhiano yaliofikiwa nchini.

Leave a comment