Zanzibar kuwa gizani wiki tatu

WAKAZI wa Unguja watakosa umeme kwa tatu kutokana na kulipuka na kuungua kwa kifaa katika kituo cha kupokelea umeme wa gridi ya taifa kilicho eneo la Fumba.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Shangani wilayani Mjini Magharibi jana, Waziri wa Maji, Ujenzi, Ardhi na Nishati, Mansoor Yusuph Himid alisema kuharibika kwa mitambo hiyo kumesababishwa na kuzidiwa nguvu kutokana na kuongezaka kwa matumizi ya nishati hiyo.
Mansoor alisema Serikali ya Mapinduzi (SMZ) imechukua hatua madhubuti kurekebisha tatizo hilo na kuahidi kulimaliza ndani ya wiki tatu.
“Serikali inachukua juhudi kurekebisha tatizo hilo na tunawaomba wananchi wavumilie wakati mafundi wa shirika la umeme Zanzibar na wataalam kutoka Afrika Kusini wakijitahidi kurekebisha,” alisema Waziri Mansoor.
Alifafanua kuwa SMZ ina mpango wa kuagiza vipuri kwa ajili ya mitambo hiyo na kusisitiza kwamba vitawasili nchini ndani ya wiki tatu na kufungwa.
Kutokana na tatizo hilo shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotegemea umeme zimesimama, hali inayohatarisha uchumi wa visiwa hivyo.
Hii ni mara ya pili kwa visiwa hivyo kukaa gizani kwa mwaka huu. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi Mei wakati visiwa hivyo vilipokosa umeme kwa mwezi mzima mwezi kutokana na kuharibika kwa mitambo ya umeme.

Leave a comment