hatuna taarifa ya kuzagaa kondom-smz

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema kwamba haina taarifa za kuzagaa kwa mipira ya kondom katika maeneo ya shule zinazotumiwa na wanafunzi wa masomo ya ziada (tuitions)

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Jabir Makame alipokuwa akijibu maswali na majibu ya wajumbe wa baraza la wawakilishi waliotaka kujua iwapo kuna mafunzo maalumu ya kutumia mipira ya kondoma amabyo hupewa wanafunzi wa shule.

Makame alisema kwamba moja ya mafunzo wanayopewa wanafunzi ni kujiepusha na ngono za mapema na kujizuwia kufanya ngono wakiwa na umri mdogo na sio kutumia mipira ya kondom lakini suala hilo la utumiaji wa mipira ya kondoma serikali haijui wala wizara yake haina taarifa hizo.

Mwakilishi wa Jimbo la Koani (CCM) Haji Mkema Haji ndiye aliyeuliza swali hilo la nyongeza ambapo alitaka kuelezwa iwapo mipira ya kondom ni sehemu ya mafunzo yanatofundishwa mashuleni kwa vitendo au laa kwa kuwa baadhi ya shule zinazosomwa na wanafunzi wa kujiendeleza vimekuwa vikipatikana mipira ya kondom ikiwa nje ya shule hizo.

“Ukipita katika maeneo ya tuition utakuta mipira ya kondoma chungu mzima sasa nauliza hii ni moja ya mafunzo wanayopewa wanafunzi hawa namna ya kujikinga na maradhi ya ukimwi au vipi?” alihoji Mkema

Pia wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema imeanzisha mafunzo stadi za maisha na elimu ya ukimwi katika shule 120 kwa Unguja na Pemba kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kujiepusha na tamaa ya ngonio za mapema.

Akijibu maswali na majibu katika kikao cha baraza la wawakilishi baada ya kuulizwa swali na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini (CCM) Ali Abdallah Ali aliyetaka kujua kama mafunzo hayo hutolewa kwa walimu na wanafunzi na yameleta faida gani hadi sasa.

Mwakilishi huyo alisema wizara ya elimu kwa kushirikiana na taasisi za serikali na shirika la kuhudumia watoto (UNICEF) imekuwa ikielimisha jamii umuhimu wa elimu na athari za ngono kwa wanafunzi ili kuepusha mimba za mapema na utoro mashuleni jee ni walimu wangapi na wanafunzi waliofaidika na mafunzo hayo.

Naibu Waziri huyo alisema mafunzo hayo yanayotolewa kwa walimu na wanafunzi ni endelevu na siyo ya kupita ambapo walimu na wanafunzi wengi hivi sasa wameshafaidika na mafunzo hayo.

Alisema kwamba mafunzo hayo yanatolewa na yanaendelea kutolewa kwa shule mbali mbali za Unguja na Pemba na kuanzia mwaka 2004 hadi hivi sasa mafunzo ya stadi za maisha na elimu ya ukimwi yanayolewa kwa ujumla ni shule 120 kwa nchi nzima.

Naibu huyo aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba katika kipindi cha mwaka 2008/2009 jumla ya shule 20 za Unguja na Pemba zimepatiwa mafunzo ya stadi za maisha na ukimwi kwa walimu na wanafunzi kupitia tume ya ukimwi Zanzibar (ZAC).

Alisema kile shule ilitoa wanafunzi 50 na walimu watano kwa upande wa Unguja na shule zilizopewa mafunzo hayo ni pamoja na Jangombe msingi, Chumbuni, Bububu msingi A na B, Kusini, Kiongoni, Kiboje, Ghana, Nungwi, Mkwajuni, Mahonda na Kiwengwa.

Shule nyengine ni ambazo ni kwa upande wa kisiwani Pemba ni pamoja na shule ya Vitongoji, Michakaeni, Kangagani msingi, Mtambile, Ole msingi, Kangani msingi, Finya na Sizini.

Naibu Waziri huyo wa Elimu alisema wanafunzi waliopatiwa mafunzo amabo ni waelimishaji rika wanaendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi wenzao kupitia klabu za afya mashuleni.

Akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Matemwe (CCM) Ame Mati Wadi alitaka kujua kama kuna tathmini yotote iliyofanywa na wizara kujua upunguaji na ongezeko la mimba za utotoni na mimba za utotoni, Naibu huyo amesema mimba za utotoni zimepungua kwa kiasi kikubwa hivi sasa ikilinganishwa na siku za nyuma kabla ya mafunzo hayo.

Leave a comment