wizara yapokea malalamiko

WAZIRI wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdaalla Juma amewaambiwa wajumbe wa baraza la wawakishi kwamba wizara yake imekuwa ikipokea malalamiko na kuyashughulikia inayotokana na migogoro ya kazi ikiwemo mahoteli makubwa ya kitalii.

Akijibu swali la Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Amina Iddi Mabrouk aliyetaka kujua kamisheni ya kazi nahusika vipi katika ajira za wafanyakazi wa sekta binafsi hasa katika hoteli za kitalii na biashara nyengine za kitalii na wizara ina shughulikia vipi migogoro katika kazi.

Waziri Asha alisema kwa mujibu wa sheria ya ajira Nam. 11 ya mwaka 2005 wizara ya kazi kupitia kamisheni ya kazi imepewa jukumu la kusimamia ajira katika sekta zote ikiwemo sekta ya umma na binafsi.

Alisema kwa hali hiyo hoteli za kitalii na biashara nyengine zinazohusiana na utalii zote zinasimamiwa na wizara ya kazi kwa masuala yanahusiana na ajira katika sehemu za kazi.

Alisema jukumu la usimamizi wa ajira linahusisha ushughulikiaji matatizo na malalamiko ya kazi, na wizara ya kazi inaendelea kutoa elimu kwa waajiri na waajiriwa.

Waziri huyo alisema katika kuendeleza mikakati ya wizara hiyo pia wizara yake inafanya ukaguzi kazi na ukaguzi wa usalama na afya kazini mara kwa mara na kushauri utekelezaji bora wa kuwa na mazingira mazuri kazini ili kuepusha matatizo na malalamiko yanayotokea katika sekta ya kazi.

Aliwaambia wajumbe hao kwamba pia wizara yake inaendelea kuwa na mahusiano na mashauriano na wadau mbali mbali katika masuala ya kazi ambao ni shirikisho la vyama vya wafanyakazi na jumuiya ya waajiri ili wakae na wanachama wao kwa lengo la kupunguza migogoro inayojitokeza kila mara katika kazi.

Alisema wizara yake imo katika hatua ya kutengeneza kanuni za kazi ambapo katika kanuni hizo masuala ya utatuzi wa migogoro zimeweka utaratibu wa kufungua kesi katika mahakama ya kazi pale amabpo migogoro itashinda kupatiwa ufumbuzi katika hatua za mwanzo.

Katika hatua nyengine Waziri Asha amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya kuwaendeleza wajasiriamali maarufu kwa jina la mabilioni ya JK tayari zimeanza kutolewa kwa watu wanaohusika na fedha hizo.

Waziri Asha alisema fedha hizo katika awamu ya kwanza zitatolewa kwa ajili ya wajasiarimali wanaounda SACCOS na vikundi mbali mbali vya Unguja na Pemba.

Alisema maendeleo ya fedha za kuwawezesha kiuchumi wajasiriamali zilizotolewa na viongozi wakuu Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Abeid Karume zitawasaidia wananchi wengi kwa kujiendeleza kibiashara.

“Fedha ni kweli zilichelewa kwa sababu mbali mbali…moja ni kwamba ilikuwa tunafanya usaili wa kujuwa nani wanaohusika na kupatiwa fedha hizo na nani hahusiki lakini sasa tayari tumeshajua kwa hivyo mambo mazuri sasa”alisema Asha.

Alisema fedha zilizotolewa kwa ajili ya wajasirimali na kuwawezesha wananchi kukuwa kiuchumi kwa upande wa Zanzibar ni shilingi Millioni 800 ambazo zimetolewa na Rais Kikwete pamoja na Rais Karume.

Leave a comment