SAU Yashindwa Kurejesha Fomu ZEC

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) Haji Mussa Kitole jana ameshindwa kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo ni siku ya mwisho wa urejeshaji wa fomu hizo.

Kitole awali alikataliwa kupewa fomu ya kuwania nafasi hiyo na ZEC kutokana na kuwa chama hicho kimetoa wagombea urais wawili wenye kutaka kuwania urais wa Zanzibar wakati sheria za ZEC zinaeleza chama kitowe mgombea mmoja wa nafasi hiyo.

Haji Mussa Kitole na Haji Ramadhan Haji Agosti 16 walifika afisi za ZEC na kutaka wakabidhiwe fomu za kuwania urais wa Zanzibar amabpo kila mmoja akiwa na barua yake mmoja akiwa na barua kutoka kwa katibu wa chama hicho na mwengine akiwa na barua ya mwenyekiti wa chama hicho kuteuliwa kuwa mgombea.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi hizo za ZEC wiki iliyopita Mkurugenzi wa tume hiyo Salim Ali Kassim alisema haiwezekani kupewa fomu watu wawili kutoka chama kimoja na kuwashauri warudi kukubaliana kutoa mgombea mmoja ambapo baadae chama hicho kilimteuwa Kitolea kuwania nafasi hiyo.

Hata hivyo baada ya kuchukua fomu hizo za kuwania urais alitakiwa kupata wadhamini 200 wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba na kuwasilisha shilingi millioni mbili taslim kama wagombea wengine lakini hadi jana ambayo ni siku ya mwisho mgombea wa SAU ameshindwa kurejesha fomu hizo.

“Hatujui vipi lakini kwa ufupi ni kwamba wagombea wote wamrejesha fomu zao kwa tume isipokuwa mgombea wa SAU yeye hadi sasa hajafika na leo ndio siku ya mwisho kwa maana hiyo tunasema ameshindwa kurejesha fomu kwetu” amesema Mkurugezi wa ZEC, Kassim.

SAU ndio chama pekee kilichoshindwa kuwasilisha fomu zake kwa tume ya uchaguzi ambapo vyama vyengine vilivyorejesha fomu zake jana ni pamoja Juma Ali Khatib (46) -TADEA, saa 4:13 asubuhi, Said Soud Said (62) AFP,saa 5:00, Haji Ambar Khamis (44) NCCR–Mageuzi, saa 5:30, Kassim Bakari Ali (43) Jahazi Asilia, saa 7.06, na Haji Khamis Haji (60) NRA saa 8:20 mchana.

Wengine waliorejesha fomu zao kwa ZEC wa mwanzo ni ni Mgombea wa chama cha wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ((67) alirejesha Agosti 16 majira ya saa 9:00 mchana wakati mgombea wa chama cha mapinduzi (CCM) Dk Ali Mohammed Shein (62) alijesha fomu yake Agosti 18 majira ya saa 8:30 mchana.

Akizungumza katika kikao hicho baada ya kupokea fomu hizo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Khatib Mwinchande alisema kwao wao kujitokeza kwa wagombea wengi ni kupanuka kwa demokrasia nchini.

Mwenyekiti huyo aliwaomba wagombea wote ambao watateuliwa na tume kuingia katika mchakato wa kutaka urais baada ya kuhakikiwa fomu zao kuingia katika kampeni za kistaarabu zisizo na matusi ili kuepusha Zanzibar kuingia katika sura mbaya ya kukosekana amani.

Leave a comment