Muda wa wa mseto ni mdogo-Nahodha

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa hivi sasa sio rahisi kutokana na muda ulibaki ni mfupi.

Hayo yameelezwa jana na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio yaliopatikana katika kipindi cha miaka 46 ya mapinduzi katika ukumbi wa juu wa baraza la wawakilishi Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi.

Nahodha alisema huu ni wakati wa kuangalia uwezekano wa kutengeneza Zanzibar mpya na sio wakati wa kujadiliana masuala hayo ya kuunda kwa serikali ya pamoja.

Kauli hiyo ya Nahodha imefuatia maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatma ya mazungumzo ya viongozi wakuu wa vyama kati ya Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ambayo yamewapa matumaini makubwa wananchi wa Zanzibar.

Nahodha alisema mazungumzo ya viongozi hao yatasaidia zaidi katika kuinua nchi kimaendeleo pamoja na kuonesha njia nzuri ya kupita wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kauli hiyo ya Nahodha itaondosha matumaini makubwa walionao wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba ambao kwa takribani mwezi sasa wamekuwa na tamaa kubwa ya kuwepo kwa serikali ya pamoja kufuatia mazungumzo yalioanza febuari 5 mwaka huu ikulu mjini Unguja kati ya Rais Karume na Maalim Seif.

Waziri Kiongozi alisema kwamba makubaliano yaliofikiwa na viongozi hao ni sehemu moja wapo iliyoweza kuifanya Zanzibar kuwa mpya, hivyo kazi iliopo hivi sasa kuyajali na kuyathamini makubaliano yao kwa kuunga mkono katika utekelezaji wake.

“Kwa kweli makubaliano kati ya rais Karume na Katibu Mkuu wa (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, ni sehemu moja wapo kuonesha na kufungua milango ya maendeleo visiwani Zanzibar”alisisitiza Nahodha.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa dhati viongozi wakuu hao rais Karume na Maalim Seif kwa uamuzi wao wa kufufuwa mazungumzo hayo ambayo lengo lake kubwa ni kuleta maelewano na kuondosha migogoro ya kisiasa nchini.

Alisema mazungumzo hayo yamefunguwa ukurasa mpya wa maelewano ya kisiasa ambapo sasa hali ya kisiasa imekuwa shwari na kuwepo kwa utulivu wa hali ya juu.

”Tunawapongeza kwa dhati viongozi wetu wakuu mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa yamefunguwa ukurasa mpya wa amani na utulivu huu ni wakati wa kujenga Zanzibar mpya yenye utulivu na hakuna lisilowezekana” alisema Shamsi.

Nahodha alisema katika kipindi cha miezi miwili sasa amani na utulivu wa nchi umerudi kama zamani na zile vurugu za kisiasa zilizokuwepo katika kipindi cha uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa sasa hazipo tena.

Alisema kwamba ni kweli hatua ya viongozi hao wawili kukaa na kuafikiana kuzungumza pamoja kuleta faraja kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa kuwa kumeongeza suala zima la ushirikiano na umoja katika harakati za maendeleo.

Alifahamishwa kwamba licha ya kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa dini, taasisi na wananchi wengine kupendekeza kufanyika kwa serikali ya mseto Zanzibar lakini hatua hiyo bado haitokuwa ni nyepesi sana kwa wakati huu.

Alisema kwamba hatua ya pamoja ya mapendekezo hayo ya kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa bado Serikali kuu haijasikia wala kupata maoni yoyote ya kuunda Serikali ya Mseto hivyo suala hilo bado linazungumzwa na kupendekeza katika ngazi za chini.

Alisema kuwa Serikali ikipata taarifa zilizo sahihi juu ya uundaji wa Serikali ya mseto ni lazima kwanza taarifa hiyo ipitishwe katika baraza kuu na kutolewa mapendekezo yatakayofaa kwa maslahi ya wananchi wake.

“Sisi kama ni viongozi wakuu wa Serikali na ni watekelezaji wa majukumu yote bado hatujapata taarifa zilizo sahihi kutoka kwa vyama vya siasa wala viongozi wa kidini juu ya uundwaji wa serikali ya mseto pamoja na kuonea taarifa hizo lakini kwa upande wetu lazima tupate barua rasmi za kushauriwa hilo” alisema Nahodha.

Hata hivyo Nahodha alisema suala hilo linahitaji muda wa majadiliano na iwapo litajadiliwa katika vikao vyote vinavyostahiki na kupitishwa nae atakuwa miongoni mwa wenye kuliunga mkono.

Akizungumzia suala la kubadilishwa kwa katiba ili kumpa nafasi Rais wa Zanzibar kuendelea kuwepo madarakani Nahodha alisema suala hilo nalo sio jepesi kama inavyofikiriwa na wananchi kwa kuwa linahitaji majadiliano na maamuzi mazito.

Alisema suala hilo lazima lipelekwe na kujadiliwa katika ngazi tatu kwa kuwa kuna katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, katiba ya Zanzibar na katiba ya chama hicho hata iwapo katiba mbili zitakubali haitakuwa rahisi kukubalika katika katiba ya chama.

Alisema kwa upande wa serikali ya mapinduzi ya zanzibar umeyasikia maoni mbali mbali yaliyotolewa na taasisi mbali mbali ikiwemo za kidini na vyama vya siasa katika suala hilo ingawa haya maoni hayo hayajafikishwa rasmi serikalini.

”Tumeyasikia maoni mbali mbali na tofauti katika suala la kubadilisha katiba ya nchi na kuongeza vipindi vya muda wa rais kuwepo madarakani…lakini maoni hayo hayajatufikia rasmi”alisema Nahodha.

Alisema suala la kubadilisha katiba ya nchi linachukuwa mkondo mrefu ambapo kwa upande wa Zanzibar suala hilo linahitaji kupata baraka za baraza la wawakilishi pamoja na chama cha mapinduzi.

Akizungumzia mafanikio yaliopatikana katika katika kipindi cha utawala wa Rais Karume, Nahodha alisema kuwa ameweza kufanikiwa kuzipunguza kero za wananchi kwa asilimia tisini walizokuwa nazo wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Akizitaja kero hizo ni pamoja uimarishaji wa miundo mbinu kwa kiwango cha juu kabisa ikiwamo matengenezo ya Gati la Malindi, ambalo hivi sasa limekuwa likihudumia meli kubwa kwa ufanisi wa hali ya juu,Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, kusambaza umeme vijijini ukiwamo ule wa kutoka Tanga hadi kisiwani Pemba ambao unatarajiwa kukamilika Machi mwaka huu, maji safi na salama, pamoja na miradi mbali mbali ya kimaendeleo.

“Wakati tunaadhimisha miaka 46 ya mapinduzi ya zanzibar tunasema kwamba rais Karume amefanikiwa kwa asilimia 90% kutekeleza na kusimamia ilani ya uchaguzi ya CCM….leo hii zanzibar inatajwa kwamba imevuka malengo ya milenium katika sekta ya elimu”alisema Shamsi.

Alisema kazi kubwa inayofanywa sasa katika suala la miundo mbinu ni ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Zanzibar kuwa na hadhi ya kimataifa ambacho njia za kurukia ndege zitapanuliwa kutoka mitar 2,400 hadi kufikia 3,22 na hivyo kuziwezesha ndege kubwa ikiwemo zinazoleta watalii kufanya safari zake kuja Zanzibar moja kwa moja.

Aidha alisema ujenzi wa barabara unaofanywa Unguja na Pemba ikiwemo barabara za vijiji umerahisisha sana sekta ya usafirishaji pamoja na sekta ua utalii ambayo sasa imekuwa moja ya tegemo kubwa katika kuingiza mapato ya nchi.
Kufuatilia kuwepo kwa mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa kati ya CCM na CUF baadhi ya taasisi na vyama vya siasa vimekuwa vikitoa maoni tofauti kutaka kubadilishwa kwa katiba ya Zanzibar na kuongezwa muda wa rais kuwepo madarakani kwa ajili ya kusimamia maridhiano hayo.

Hata hivyo suala hilo kwa upande wa chama cha mapinduzi umelitolea ufafanuzi kupitia makamo mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Pius Msekwa na kusema haiwezekani kuichezea katiba na kuongeza muda wa rais Karume kuwepo madarakani.
Sherehe za maadhimisho ya miaka 46 ya mapinduzi ya zanzibar zinatarajiwa kufikia kilele chake januari 12 katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Leave a comment